Vatican News
Papa Francisko: waamini jengeni mshikamano wa dhati kwa kusaidiana na kutegemezana kwa hali na mali katika maisha! Papa Francisko: waamini jengeni mshikamano wa dhati kwa kusaidiana na kutegemezana kwa hali na mali katika maisha!  (Vatican Media)

Papa: Jengeni mshikamano kwa kusaidiana & kutegemezana

Papa Francisko anawasihi waamini kujenga: umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili kusaidiana na kutegemezana kwa hali na mali. Kimsingi, Jumuiya ya waamini inapaswa kukita mizizi katika amani na utulivu wa ndani; kwa kushuhudia imani katika matendo; kwa kuambata ufukara wa kiinjili pamoja na kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza katekesi yake, Jumatano, tarehe 26 Juni 2019, kuhusu mambo msingi yaliyoitambulisha Jumuiya ya kwanza ya Wakristo yaani: Jumauiya iliyokuwa inadumu katika mafundisho ya Mitume, katika ushirika, katika kuumega mkate na katika sala alipata nafasi ya kuwasalimia wagonjwa waliokuwa wamehifadhiwa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI mjini Vatican kutokana na jua kali! Baba Mtakatifu amewasihi waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kudumu katika imani, tayari kuitolea ushuhuda katika matendo adili, matakatifu kama mashuhuda wenye furaha ya ukweli wa Kristo Mfufuka!

Baba Mtakatifu amewataka waamini kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili kusaidiana na kutegemezana kwa hali na mali. Kimsingi, Jumuiya ya waamini inapaswa kukita mizizi ya maisha na utume wake katika amani na utulivu wa ndani; kwa kushuhudia imani katika matendo; kwa kuambata ufukara wa kiinjili pamoja na kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakati wa Katekesi yake, Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa kundi la Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki kutoka Burkina Faso. Wakristo watumie fursa hii kumwomba Roho Mtakatifu aweze kuzipyaisha Jumuiya za Kikristo ili ziwe kweli ni shuhuda wa umoja na mshikamano.

Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yanakuwa ni mahali pa kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa; Liturujia ya Kanisa ni mahali pa kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya waamini. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, Liturujia iwe ni daraja ya umoja na udugu katika Kristo Mfufuka, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yawawezeshe waamini kujenga umoja, upendo na mshikamano wa dhati kadiri ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

Papa: Ushuhuda

 

26 June 2019, 14:19