Tafuta

Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche, Italia, lina jumla ya Makanisa 521 na kati yake Makanisa 364 yamebomolewa na tetemeko la ardhi, 20 yamekarabatiwa na yanatumika! Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche, Italia, lina jumla ya Makanisa 521 na kati yake Makanisa 364 yamebomolewa na tetemeko la ardhi, 20 yamekarabatiwa na yanatumika! 

Papa Francisko Camerino: Makanisa 364 yamebomoka kwa tetemeko!

Kabla ya tetemeko la ardhi, Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche lilikuwa na Makanisa 521 na kati yake, Makanisa 364 yameharibiwa kiasi kwamba hata mengine hayafai tena kwa matumizi ya Ibada. Makanisa 20 tayari yamefanyiwa ukarabati kwa fedha iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI na tayari yameanza kutumika. Kanisa kuu la Camerino, bado halijafanyiwa ukarabati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 16 Juni 2019 wakati wa Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu amefanya hija ya kichungaji kama kielelezo cha mshikamano wa upendo wa kidugu, kwa kutembelea Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche, nchini Italia. Haya ni maeneo yaliyoathirika sana kwa matetemeko ya ardhi yaliyojitokeza kati ya mwaka 2016-2017, sehemu kubwa ya Italia ilipojikuta ikipoteza imani na matumaini ya leo na kesho iliyobora zaidi baada ya kuona na kushuhudia athari zilizojitokeza katika maisha ya watu na mali zao! Baada ya kuwasili Camerino, Baba Mtakatifu amepata fursa ya kutembelea baadhi ya familia zinazoishi katika makazi ya muda!

Baba Mtakatifu anasema, anatamani sana kutembelea kila nyumba na kusalimiana na wakazi wake, lakini haiwezekani  ndiyo maana amewapatia baraka zake za kitume, kama kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa kila mmoja wao. Anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea, ili hatimaye, changamoto hii, iweze kupata ufumbuzi wa kudumu. Amewashukuru na kuwapongeza kwa uvumilivu na ujasiri wao katika maisha! Kwa upande wake, Askofu mkuu Francesco Massara wa Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche anasema, familia ya Mungu katika maeneo haya yaliyoathirika, imejiandaa kikamilifu kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao; ushuhuda wa ujirani mwema, umoja na udugu wakati wa shida na raha.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 4 Oktoba 2016, Baba Mtakatifu alifanya hija ya faragha katika maeneo haya, akaonesha uwepo wake wa karibu pamoja na kuwaombea waathirika wa matetemeko haya ambayo yameleta athari kubwa katika maisha ya wananchi walioko kati kati ya Italia. Ujio wa Baba Mtakatifu kwa wakati huu ni changamoto ya imani, ili kuanza tena ujenzi wa maeneo haya kwa ari, moyo mkuu unaosheheni matumaini kwa watu walioguswa na kutikiswa kutoka katika undani wa maisha yao! Watu wengi wamejikatia tamaa na hawana nguvu tena ya kuweza kusimama wenyewe na kusonga mbele ndiyo maana hija hii ya Baba Mtakatifu Francisko ina umuhimu wa pekee katika maisha ya watu.

Kanisa linataka kuonesha mshikamano katika tunu msingi za maisha ya kiroho zinazomwilishwa katika huduma ya upendo, ili kuendeleza ujenzi na ukarabati wa maeneo haya. Kanisa linashuhudia ile Injili ya Msamaria mwema kwa kuongozana na watu wenye shida na mahangaiko, ili hata Serikali kwa upande wake, iweze kutekeleza sera na mipango kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya kudumu kwa waathirika wa tetemeko la ardhi! Camerino ni mji wa kale ambao una historia ya ukarimu na upendo kwa vijana wanaotafuta hekima, ujuzi, maarifa na stadi za maisha kutoka katika Chuo kikuu cha Camerino. Lakini uhaba wa makazi ya wanafunzi na maeneo ya kujifunzia, kumeathiri si tu maisha ya wananchi wa Camerino bali hata uchumi wake.

Baadhi ya maeneo ya tafiti za kisayansi yalifungwa kwa sababu za kiusalama. Katika muktadha huu anasema Askofu mkuu Francesco Massara kwamba, hata Kanisa limeathirika sana. Kabla ya tetemeko la ardhi, Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche lilikuwa na Makanisa 521 na kati yake, Makanisa 364 yameharibiwa kiasi kwamba hata mengine hayafai tena kwa matumizi ya Ibada. Makanisa 20 tayari yamefanyiwa ukarabati kwa fedha iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI na tayari yameanza kutumika. Kanisa kuu la Camerino, bado halijafanyiwa ukarabati. Kanisa kuu la “San Venanzio”, kielelezo cha imani ya watu wa Mungu huko Camerino litafunguliwa mwezi Desemba 2019, mchango maalum kutoka kwa mwamini mmoja ambaye ameguswa sana na mahangaiko ya ndugu zake na kuamua kuwasaidia ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na mwanadamu kutakatifuzwa kwa mafumbo mbali mbali yanayoadhimishwa na Mama Kanisa!

Papa: Makazi ya Muda

 

16 June 2019, 15:12