Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika mahubiri yake huko Camerino amekazia mambo makuu matatu: Kumbukumbu kama ufunguo wa maisha; Matumaini thabiti na Ukaribu wa Mungu kwa waja wake! Papa Francisko katika mahubiri yake huko Camerino amekazia mambo makuu matatu: Kumbukumbu kama ufunguo wa maisha; Matumaini thabiti na Ukaribu wa Mungu kwa waja wake!  (Vatican Media)

Papa Francisko Camerino: Kumbu kumbu, Matumaini na Ukaribu!

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche, nchini Italia. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amegusia mambo makuu matatu: Kukumbuka kama ufunguo wa maisha; Matumaini thabiti kwa Roho Mtakatifu ni endelevu na dumifu; Ukaribu wa Mungu unaofuliwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu! Kila mwamini anapaswa kutekeleza wajibu wake vyema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ukuu na utukufu wa Mwenyezi Mungu unaimbwa na Mzaburi anayesema mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Ni Zaburi inayogusa undani wa mahangaiko na mateso ya binadamu anayepigishwa magoti kutokana na majanga asilia, kiasi hata cha kukosa matumaini tena? Lakini, Mwenyezi Mungu anakumbuka na kuwafariji waja wake, kwa sababu amewahifadhi katika sakafu ya moyo wake! Ni kawaida watu kusahau na mambo mengi kupita kama ndoto ya mchana, lakini Mwenyezi Mungu anakumbuka. Binadamu si mali kitu, ardhi inapotetemeka na kusababisha maafa makubwa, lakini, ikumbukwe kwamba, binadamu ana thamani kubwa machoni pa Mungu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 16 Juni 2019 katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu wakati wa hija yake ya kichungaji katika Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche, nchini Italia. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amegusia mambo makuu matatu: Kukumbuka kama ufunguo wa maisha; Matumaini thabiti kwa Roho Mtakatifu ni endelevu na dumifu; Ukaribu wa Mungu unaofuliwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu! Papa anasema kukumbuka ni ufunguo wa maisha unaothibitisha na kuwakumbusha binadamu kwamba, wanapendwa, wao ni watu wa pekee na wala hawana mbadala.

Kumbu kumbu iwape waamini ari na nguvu ya kusonga mbele pasi na kukata tamaa, kwani kumbu kumbu ya mambo mabaya inakuwepo daima na ni chanzo cha majonzi na masikitiko katika maisha. Hapa waamini wanahamasishwa kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya kuwakomboa kama ilivyokuwa kule Misri alipowakomboa Waisraeli kutoka utumwani. Kumbu kumbu mbaya za mambo ya kale zinawateka, zinawafunga na kuwafanya wengi kupooza katika maisha, kiasi cha kuhitaji nguvu ya ziada inayoweza kumkomboa mtu kutoka katika undani wa maisha, kama anavyosema Kristo Yesu katika Injili ya Jumapili hii yaani kuna “mambo mengi ambayo hawawezi kuyastahimili hivi sasa”.

Si rahisi sana kukwepa udhaifu wa kibinadamu na kwamba, mara nyingi watu wanatafuta njia ya mkato katika maisha! Lakini, Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake Roho Mtakatifu, Mfariji anayewasimamisha tena baada ya kuelemewa na mzigo wa maisha. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kugeuza kumbu kumbu zao za utumwa na kuanza kupata mwelekeo mpya unaofumbatwa katika uhuru, faraja katika madonda na hivyo kuwakirimia kumbu kumbu ya wokovu! Roho Mtakatifu anaganga na kuponya madonda ya binadamu, kama ilivyokuwa kwenye Madonda Matakatifu ya Yesu, yakawa ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu unaoangaza na kuwanyanyua tena wale walioanguka kutokana na uzito wa ugumu wa maisha!

Hii ni changamoto kwa waamini kumkimbilia Roho Mtakatifu katika shida na mahangaiko yao kwani Roho Mtakatifu ni mjenzi wa matumaini! Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumaini thabiti kwa Roho Mtakatifu ni endelevu na dumifu kwani yanasimikwa katika uaminifu wa Mungu. Haya ni matumaini yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu kwa kutambua fika kwamba, wanapendwa na wana thamani kubwa machoni pa Mungu na daima Mwenyezi Mungu anapenda kuambatana na waja wake. Haya ni matumaini ambayo ni chemchemi ya amani na furaha ya kweli; matumaini ambayo yana mizizi imara sana na wala hakuna dhoruba yoyote ile inayoweza kuyang’oa, haya ni matumaini ambayo kamwe hayatahayarishi kwani yanampatia mwamini nguvu na ujasiri wa kupambana na dhiki yake.

Kwa kawaida mwanadamu katika shida, magumu na changamoto za maisha, hupenda kujijengea ngome kuzungumza hofu na huzuni, lakini Roho Mtakatifu “anavunjilia mbali ngome hizi” na kuwalisha kwa matumaini hai, changamoto kubwa ni kumwalika Roho Mtakatifu ili aweze kuwatembea na kuwa karibu nao katika hija ya maisja yao! Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukaribu wa Mungu umejifunua katika Fumbo angavu la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha umoja. Ni Fumbo la Mungu Baba aliyemtoa Mwanaye wa pekee, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akaonesha ukaribu wake kwa kumtuma Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia waja wake kubeba mizigo ya maisha.

Roho Mtakatifu ni Mfariji anayewakirimia waamini: nguvu na ujasiri;  upendo na huruma ya Mungu, na kuwarahisishia mchakato wa kubeba mzigo wa maisha. Huyu ndiye Roho Mtakatifu anayekumbukwa na waamini kila mara wanapofanya Ishara ya Msalaba. Roho Mtakatifu ni mtaalam wa kufufua, kusimamisha na kuumba upya. Baba Mtakatifu anasema, kunahitajika nguvu ya ziada ili kujenga, kuanza upya tena, kujipatanisha na hivyo kuwa na maelewano. Hii ndiyo nguvu ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake, ili kusonga mbele, tayari kuanza upya, kujaribu tena na kuanza ujenzi! Baba Mtakatifu Francisko anasema, yuko kati yao ili kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu anayekumbuka, ili asiwepo mtu ambaye anawasahau watu wanaoteseka na kuhangaika na maisha.

Amekuja kusali na kumwomba Mungu wa matumaini, ili kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho. Anamwomba Mungu ambaye ameonesha ukaribu wake, ili kufufua na kujenga ari na moyo wa ujirani mwema. Baada ya miaka minne tangu tetemeko la ardhi lilipoyakumba maeneo haya, kuna hatari kwamba zile ahadi zilizotolewa zikatoweka na kufutika machoni pa watu. Mwelekeo huu unawafanya watu kuchanganyikiwa na maeneo kukimbiwa na wenyeji wake. Mwenyezi Mungu anapenda kuwasukuma ili kukumbuka, kukarabati na kujenga; mambo yanayopaswa kufanywa kwa ushirika bila kuwasahau wale wote wanaoteseka!

Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, Mwenyezi Mungu anakumbuka, anaganga na kuponya kumbu kumbu za watu wake zilizojeruhiwa kwa kuwapaka kwa mafuta ya matumaini kwani Mungu yuko karibu sana na waja wake, anapenda kuwanyanyua kutoka katika undani wa maisha yao, ili hatimaye, waweze kuwa ni wajenzi wa mafao ya wengi na wafariji wa nyoyo za watu, kila mtu akijitahidi kutenda wema na kuwafariji wengine. Mwenyezi Mungu daima anawakumbuka waja wake na wao wanapaswa kukumbuka kwamba, wako ulimwenguni ili kuwapatia wengine matumaini, kwa kuwaonesha ukaribu kwa sababu wao ni watoto wa Mungu ambaye ni asili ya faraja zote!

Papa: Camerino
16 June 2019, 15:35