Tafuta

Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Panama kwa ari na moyo wao wa ukarimu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019. Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Panama kwa ari na moyo wao wa ukarimu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019. 

Papa Francisko anawashukuru wananchi wa Panama!

Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mungu kwa yale aliyoona na kushuhudia nchini Panama; ukarimu ni tunu ambayo ni sehemu ya amana, utajiri na urithi wa watu wa Mungu. Panama na watu wake ni nchi inayoheshimiwa. Anamshukuru na kumpongeza Rais wa Panama na Maaskofu waliojichanganya na kuandamana na vijana kama kielelezo cha heshima na upendo kwa watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 13 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na mahujaji kutoka nchini Panama waliokuwa wameandamana na Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama, waliofika kumshukuru kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu  “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, aliwataka vijana kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, kusema “Ndiyo” ili kukumbatia Injili ya uhai; kusema “Ndiyo” katika ujenzi wa Jumuiya, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vijana waseme “Ndiyo” ili kulinda na kudumisha mila, desturi na tamaduni njema, tayari kuleta mabadiliko katika maisha ya jamii kwa mwanga wa Injili ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wa Mungu nchini Panama waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019!Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, waamini mara nyingi ni wepesi sana kuomba, lakini, wagumu kushukuru lakini ikumbukwe kwamba, falsafa ya neno asante ni kuomba tena! Baba Mtakatifu anawashukuru sana wananchi wa Panama kwa sadaka na majitoleo yao, kwa hakika wenye macho waliweza kujionea wenyewe jinsi ambavyo vijana walivyotimua vumbi nchini Panama wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Baba Mtakatifu anasema, ili wanandoa waweze kudumu katika maisha na ahadi zao, daima wakumbuke maneno makuu matatu: “Hodi, samahani na asante”.

Hii ina maana kwamba, wanandoa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana. Mama Kanisa kila wakati anapata mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu, ndiyo maana watu wote, familia pamoja na viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga tabia ya unyenyekevu uliopyaishwa, unaotamani kufundwa vyema; kuelimishwa ili uweze kuelimisha; kusaidiwa ili uweze kusaidia; kusindikiza, kung’amua, kuwaingiza na kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho na ushuhuda wa mradi mkubwa wa upendo wa Mungu kwa binadamu unaofumbatwa katika Injili ya familia!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, anamshukuru Mungu kwa yale aliyoona na kushuhudia nchini Panama; ukarimu ni tunu ambayo mtu hawezi kununua dukani, bali ni sehemu ya amana, utajiri na urithi wa watu wa Mungu, unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao. Panama na watu wake ni nchi inayoheshimiwa. Anamshukuru na kumpongeza Rais wa Panama pamoja na Maaskofu waliojichanganya na kuandamana na vijana kama kielelezo cha heshima na upendo kwa watu wa Mungu. Amerika ya Kusini inazo changamoto na matatizo yanayotaka kukwamisha heshima hii, lakini ukarimu na heshima hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya wananchi wa Amerika ya Kusini, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu anaendelea kuishukuru Panama kwa kuandaa Siku ya Vijana Kitaifa ili kuwajengea uwezo wa kujadiliana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja ya kuendelea kujenga uwezo na madaraja ya majadiliano kati ya vijana na wazee, ili vijana waweze kuzamisha mizizi katika kumbu kumbu hai za mila, desturi na mapokeo kutoka kwa wahenga wao, ili kuzikuza na hatimaye, kuzitolea ushuhuda. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa makini, ili kamwe wasitumbukizwe kwenye ukoloni wa kiitikadi unaoendelea kupamba moto kila kukicha! Vijana wasimame kidete kulinda na kudumisha utambulisho wao wa kitaifa!

Baba Mtakatifu amewashukuru wananchi wa Panama kwa maadhimisho mbali mbali yaliyofanyika kama sehemu ya maandalizi kwa Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019, kwa kutambua mizizi na asili ya watu wa Amerika ya Kusini, ili kuendeleza mapokeo, mila na desturi njema. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, ameridhishwa sana na hali aliyoikuta nchini Panama, kwani ameonja, hali na maisha ya kawaida ya wananchi wa Panama. Ameguswa na upendo kiasi kwamba, anaona ni wajibu wake kuwashukuru wananchi wa Panama ambao tangu sasa wanapaswa kujiandaa tena kwa maadhimisho yatakayofanyika nchini Panama kuanzia sasa hadi miaka 150 ijayo, kwa hakika, Kanisa litarudi tena Panama kwa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Papa: Panama
14 June 2019, 16:41