Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaishauri Jumuiya ya Kimataifa kufuata na kutekeleza kwa makini tafiti za kisayansi kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Baba Mtakatifu Francisko anaishauri Jumuiya ya Kimataifa kufuata na kutekeleza kwa makini tafiti za kisayansi kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mazingira: Fuateni ushauri wa wanasayansi!

Mambo msingi: Mosi, mabadiliko ya nishati; Pili, ni gharama ya makaa na; Tatu ni ukweli na uwazi katika kutoa taarifa za hatari kuhusu mazingira. Haya ni masuala mtambuka yanayopaswa kujadiliwa kwa kina. Mabadiliko ya kweli yanapaswa kuratibu jamii na athari za ukosefu wa fursa za ajira, ili kupunguza uzalishaji na hatimaye, kuwa na matumizi ya chini ya makaa ya mawe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha majadiliano na wadau mbali mbali ili kusaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 14 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na wakuu wa makampuni ya nishati ya mafuta kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama mwendelezo wa mkutano uliofanyika mwaka 2018, ili kukuza na kudumisha ari na moyo wa ushirikiano katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote! Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya nishati na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu anasema, majadiliano haya yanafanyika wakati muafaka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotishia maisha ya familia ya binadamu. Kwa miaka mingi, Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kusikiliza na kufuata matunda ya upembuzi yakinifu kutoka kwa wanasayansi.

Anasema, “Utabiri wa siku ya kiyama hauwezi kupuuzwa”. Majadiliano kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na mageuzi ya nishati yanapaswa kukita mizizi yake katika tafiti bora za kisayansi ili ziwaguse watu na kuwapatia watu msingi wa safari ya kimaadili na kiroho. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba, kuna hatari ya kuongezeka kwa nyuzi joto 1.5°C kiwango kilichokuwepo kabla ya Mapinduzi ya Viwanda. Ikiwa kama kiwango hiki kitaongezeka zaidi, kinaweza kusababisha maafa na majanga makubwa kama ilivyobainishwa kwenye Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21.

Bado kuna muda wa Miaka 10 kuweza kufikia utekelezaji wa makubaliano haya, vinginevyo, dunia itakumbwa na majanga na maafa makubwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, changamoto ya athari ya mabadiliko ya tabianchi inapaswa kuvaliwa njuga ili kudhibiti ukosefu wa haki unaoweza kujitokeza miongoni mwa maskini na vizazi vijavyo! Watu wanapaswa kuwajibika kwa kutambua madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kujitokeza katika kipindi kifupi au katika kipindi cha muda mrefu! Waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi ni maskini! Kumbe, ujasiri unahitajika ili kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia mama na maskini! Kizazi kijacho kina hatari ya kurithi dunia iliyochafuliwa sana na kwamba, watakao lipa gharama za uchafuzi wa mazingira ni watoto na vijana wa kizazi kipya. Kuna wimbi kubwa la vijana wanaodai mabadiliko.

Mkutano huu umejielekeza zaidi katika mambo makuu matatu: Mosi, mabadiliko ya nishati; Pili, ni gharama ya mkaa na; Tatu ni ukweli na uwazi katika kutoa taarifa za hatari kuhusu mazingira. Haya ni masuala mtambuka yanayopaswa kujadiliwa kwa kina na mapana. Mabadiliko ya kweli yanapaswa kuratibu jamii na athari za ukosefu wa fursa za ajira, ili kupunguza uzalishaji na hatimaye, kuwa na matumizi ya chini sana ya makaa ya mawe. Ikiwa kama zoezi hili litaweza kuratibiwa vyema, litaweza kutoa fursa za ajira; kupunguza pengo kubwa na ukosefu wa usawa kati ya maskini na matajiri na hivyo kuboresha maisha ya wahanga wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Jumuiya ya Kimataifa kwa kushindwa kudhbiti uzalishaji wa hewa ya ukaa, imeingia kwenye deni ambalo litalipwa na riba kubwa na kizazi kijacho. Gharama za kiuchumi na za kijamii za utumiaji wa rasilimali shirikishi wa mazingira, zinapotambuliwa kwa uwazi na kugharimiwa kikamilifu na wahusika na wala si na watu wengine au vizazi vijavyo hapo ndipo mambo haya yanapochukuliwa kuwa ni maadilifu. Baba Mtakatifu anasema, suala la tatu ni kuhusu ukweli na uwazi katika kutoa taarifa za hatari kuhusu mazingira, ili kwamba, rasilimali za kiuchumi ziweze kupelekwa mahali ambapo zinaweza kutumiwa vyema.

Ukweli na uwazi wa taarifa za kisayansi zinazokidhi viwango ni muhimu kwa ajili ya mafao ya wengi na hivyo kuwezesha rasilimali fedha kupelekwa katika uzalishaji mbadala unaotoa fursa mbali mbali ya ustadi wa kuunda na kuvumbua na wakati huo huo kulinda mazingira na kutengeneza vyanzo vingine zaidi vya ajira. Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, muda unakwenda mbio na sasa ni wakati wa kujikita zaidi kwa kile ambacho kinapaswa kutendeka kwa wakati huu na kwamba, Kanisa limejizatiti kutekeleza dhamana yake! Ustaarabu unahitaji nishati, kumbe, nishati isiwe ni chanzo cha kuharibu ustaarabu. Leo hii mabadiliko makubwa yanahitajika ili kuokoa mazingira nyumba ya wote. Bado kuna matumaini ya kuweza kudhibiti athari na majanga ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwa kama maamuzi haya yatatekelezwa kwa vitendo. Japo wanadamu wana uwezo wa kuchagua mambo mabaya, pia wana uwezo wa kuchagua yaliyo mema, na kuanza upya licha ya mazoea yao ya kifikra na kijamii!

Papa: Nishati

 

14 June 2019, 17:03