Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, changamoto za utume kwa vijana ni: Ukaribu na kuwasindikiza vijana unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Papa Francisko anasema, changamoto za utume kwa vijana ni: Ukaribu na kuwasindikiza vijana unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Utume kwa vijana: Ukaribu & Kuwasindikiza vijana

Vijana wanahitaji kuwa na mwenza wa safari ili kutafuta visima vya maji hai na kuzima kiu ya utimilifu wa maisha yao. Ukaribu usaidie kujenga na kudumisha mahusiano makini yanayofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya sala, udugu pamoja na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Vijana waoneshwe upendo na ushuhuda wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika Heri za Mlimani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 15 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirika la Familia ya Utatu Mtakatifu, Wahudumu wa watumwa pamoja na wasaidizi wao kama kielele cha maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika ambamo Padre Luigi Buccarelo amechaguliwa kuliongoza Shirika. Familia hii imejikita sana katika utekelezaji wa Injili ya huduma ya upendo na huruma; utume parokiani na shuleni pamoja na kuendelea kuwasaidia wale wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu wanashirika hawa ni mashuhuda na vyombo vya Habari Njema ya Wokovu kwa maskini!

Utume miongoni mwa vijana na wito ndiyo tema ambayo imekuwa ni dira na mwongozo wa mkutano mkuu. Itakumbukwa kwamba, hii ni tema ambayo imepembuliwa kwa kina na mapana na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa kunako mwaka 2018. Tema hii pia ni muhimu kwa familia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hati ya kutendea kazi ya Mkutano mkuu wa Shirika imebainisha changamoto na ugumu wanaokabiliana nao katika kuwasiliana na ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya. Shirika limebainisha umuhimu wa kuwa na majiundo makini kwa ajili ya utume wa vijana, kwa kuwasindikiza na hatimaye, kuwawezesha kufanya mang’amuzi ya maisha yao!

Changamoto kubwa ni utupu unaojionesha katika tamaduni kutokana na mawazo hafifu pamoja na kutopea kwa imani, kunakowafanya watu kushindwa kuzamisha maisha yao katika mambo msingi, kiasi cha imani kuonekana kuwa si mali kitu kwa vijana wa kizazi kipya!Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hitimisho la namna hii ni kosa kubwa, kwani leo hii kuna vijana wanaochakarika kutafuta maana ya maisha; vijana wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mambo makuu ya maisha, vijana wanaompenda na wanataka kuambatana na Kristo Yesu; hawa ni vijana wenye upendo mkubwa kwa binadamu. Kuna vijana wanaotafuta furaha, upendo wa kweli, mafanikio na hata utimilifu wa maisha ya ujana wao! Yote haya ni matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya, ambayo yanapaswa kuratibiwa kama alivyofanya Mwenyezi Mungu katika kazi ya Uumbaji.

Kanisa halina budi kuwasaidia vijana kuratibu na kudhibiti matamanio yao pamoja na kuwawezesha kuwa kweli ni wadau,  kwa kuwapatia nafasi, ili kweli waweze kuchachua matamanio yao! Ulimwengu wa vijana umegawanyika katika sehemu mbali mbali! Kumbe, kunahitajika: ubunifu unaofumbatwa katika wongofu wa kichungaji, ili kuwaonesha mapendekezo ya Kiinjili yanayoweza kuwasaidia kufanya mang’amuzi ya miito yao ndani ya Kanisa. Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, 2018 pamoja na Wosia wa Kitume: ”Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” ni nyaraka muhimu sana zinazoweza kuwasaidia wanashirika hawa kuwafikia vijana wa kizazi kipya.

Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, 2018 imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo  zimejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka. Hii ndiyo changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanayataka Makanisa mahalia kuimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa, daima yakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume: ”Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Sinodi ya vijana na familia. Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake, ametaja changamoto mbili muhimu zinazojitokeza katika shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana: Ukaribu na Kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu na Wafuasi wa Emau.

Vijana wanahitaji kuwa na mwenza wa safari ili kutafuta visima vya maji hai, ili kuzima kiu ya utimilifu wa maisha yao. Ukaribu usaidie kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano makini yanayofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya sala, udugu wa kibinadamu pamoja na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Vijana waoneshwe upendo na ushuhuda wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika Heri za Mlimani.Baba Mtakatifu anawataka wanashirika hawa kutoka na kuwaendea vijana ambao wametokomea mbali zaidi na kuwapokea jinsi walivyo; kwa kutambua na kuheshimu karama na mapungufu yao, ili hatimaye, kuwasaidia kadiri inavyowezekana.

Utume huu, unahitaji kwa namna ya pekee, ujasiri, upendo na umakini wa kuweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya, ili kutambua ukweli na kuweza kuufuata! Kwa kutembea pamoja na vijana kunahitaji moyo uvumilivu kwa kupanda mbegu na kuipatia nafasi ya kuweza kumea, kukua na kuchanua. Ili kufikia lengo hili utume wa shughuli za kichungaji mintarafu miito unapaswa kuwa hai, endelevu, shirikishi, wenye furaha na wingi wa matumaini, ili kuamsha imani miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Vijana wanapaswa kuhisi uwepo wa Mungu katika maisha yao. Huu ni utume unaokita mizizi yake kwa Kristo Yesu, Njia na mlango unaowapeleka vijana kwa Baba wa mbinguni; Ukweli unaozima na kukata kiu ya vijana na maisha ambayo, kwa hakika yanalipa kweli kweli kuyakimbilia na kuyaambata!

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, utakatifu wa maisha ndiyo lengo na hatima ya maisha ya kitawa na utume miongoni mwa vijana, ili waweze kupelekwa kwa Mwenyezi Mungu, bila kutumbukia katika kishawishi cha kujikatia tamaa. Utume wa miito miongoni mwa vijana, utengeneze mtandao utakaoshusha nyavu zake kwa wakati muafaka! Wanapaswa kukesha na kuwa macho; wawe ni mashuhuda na manabii wa matumaini na upya wa maisha; manabii wa furaha kwa kuishi vyema wito wao! Kamwe vijana wasipokonywe unabii! Jambo la msingi ni kuvunjilia mbali minyororo inayowafunga katika hofu na woga! Watambue kwamba, vijana wanawasubiri hamu kubwa!

Papa: Miito: Vijana
15 June 2019, 14:39