Tafuta

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa wamisionari wa mitandaoni, imision anawataka kuwa mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu! Papa Francisko katika ujumbe wake kwa wamisionari wa mitandaoni, imision anawataka kuwa mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu! 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Wamisionari wa mitandaoni!

Kunako mwaka 2012 kulianzishwa kundi la watumiaji wa mitandao nchini Hispania, linalopania kusaidia mchakato wa uinjilishaji katika ulimwengu wa kidigitali, kundi hili likapewa jina “iMission”. Huu ni mtandao wa kimisionari unaowasaidia wamisionari kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweka kujifunza namna ya kutumia vyema internet kwa ajili ya uinjilishaji sehemu mbali mbali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema mitandao ya kijamii kama vyombo vya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kunako mwaka 2012 kulianzishwa kundi la watumiaji wa mitandao nchini Hispania, linalopania kusaidia mchakato wa uinjilishaji katika ulimwengu wa kidigitali, kundi hili likapewa jina “iMission”. Huu ni mtandao wa kimisionari unaowasaidia wamisionari kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kujifunza namna ya kutumia vyema internet kwa ajili ya uinjilishaji. Mtandao huu pia unao mafunzo na majiundo yenye ubora kwa wale wote wenye nia ya kutaka kuwa wamisionari katika ulimwengu wa kidigitali na hatimaye, mtandao huu, hujihusisha kupanga siku ambazo wamisionari wa mitandaoni wanaweza kukutana mubashara kwa ajili ya kusaidia maboresho katika malezi, makuzi na majiundo yao katika mitandao ya kijamii.

Siku ya Alhamisi, tarehe 13 Juni 2019, Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua mchango mkubwa unaotekelezwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya, amewatumia salam na matashi mema wajumbe wa “iMission” kwa njia ya video, akiwataka kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano, huku wakisaidiana katika utekelezaji wa majukumu yao katika uhalisia wa maisha ya kawaida. Wasaidiane na kutiana shime; wafarijiane na kuthaminiana katika safari yao ya maisha na kamwe wasiogope kumegeana upendo, kwani hii ni lugha na utambulisho wa Mungu.

Mwenyezi Mungu amejifunua kwa taifa lake teule la Israeli kwa kujionesha kuwa ni Baba mwema anayewajali na kuwalinda watoto wake; kwa kuwabeba mikononi mwake! Ni kwa njia hii, wamisionari wa mitandaoni wataweza kuguswa na upendo wa Mungu na hivyo kutangaza na kushuhudia mambo msingi, chachu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa sasa na kwa ajili ya vizazi vijavyo. Wamisionari wa mitandaoni watambue kwamba, hii ni dhamana pevu ambayo wamejitwalia, kwa ajili ya shughuli za uinjilishaji! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka katika maisha na utume wao. Anawaomba hata wao kumkumbuka na kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Papa: Mawasiliano
14 June 2019, 16:30