Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Kesha na hatimaye, Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2019 Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Kesha na hatimaye, Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2019  (AFP or licensors)

Papa Francisko kuongoza mkesha na Sherehe ya Pentekoste 2019

Pentekoste ni Siku kuu, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na kuwakirimia Mapaji yake saba. Ni sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa. Mitume waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, wakawa na nguvu na ujasiri wa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Injili. Ni Siku kuu ya Waamini walei ndani ya Kanisa wanaoitwa na kutumwa kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuadhimisha mkesha wa Sherehe ya Pentekoste, Jumamosi, tarehe 8 Juni 2019 majira ya saa 12:00 jioni kwa Saa za Ulaya. Na tarehe 9 Juni 2019 Sherehe ya Pentekoste, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Pentekoste ni Siku kuu, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na kuwakirimia Mapaji yake saba. Sherehe ya Pentekoste, Kanisa linaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake. Mitume waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, wakawa na nguvu na ujasiri wa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Sherehe ya Pentekoste, ni Siku kuu ya Waamini walei ndani ya Kanisa wanaoitwa na kutumwa kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kutumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu. Waamini walei wanakumbushwa kwamba, wanao wajibu wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma katika barua yake kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, anapenda kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki katika mkesha wa Sherehe ya Pentekoste, Jumamosi tarehe 8 Juni 2019. Baada ya maadhimisho haya, waamini wa Jimbo kuu la Roma, wataondoka na kuelekea kwenye Madhabahu ya Divin Amore, huku wakiwa wanaandamana na Sanamu ya Bikira Maria “Madonna del Divino Amore”.

Hija hii ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma pamoja na Maaskofu wao. Hii ni changamoto kwa mihimili ya uinjilishaji Jimbo kuu la Roma kusoma alama za nyakati ili kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha watu wa Mungu. Ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu huu, kila Parokia imepewa jukumu la kuunda kikosi kazi, kitakachokuwa na dhamana ya kusikiliza na kujibu kilio cha wanaparokia, kama alivyoshauri Baba Mtakatifu Francisko. Kikosi kazi, kiwe na watu wenye uwezo wa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji parokiani.

Kardinali Angelo De Donatis anaendelea kufafanua kwamba, tarehe 24 Juni 2019, majira ya saa 1:00 Usiku kwa saa za Ulaya, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Wakleri na waamini wote wa Jimbo kuu la Roma, watakutana kuadhimisha Masifu ya Jioni na baadaye, watakabidhiwa Malengo Maalum na Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji zinazopaswa kutekelezwa katika kipindi cha Mwaka 2019-2020. Utekelezaji wa malengo haya unahitaji kwanza kabisa kipaji cha ubunifu kinachomwilishwa katika uaminifu katika hija ya maisha na utume wa Jumuiya za Waamini Parokiani.

Papa: Kesha Pentekoste
06 June 2019, 12:17