Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ametangaza nia ya kutembelea Iraq kunako mwaka 2020, Mwenyezi Mungu akipenda! Baba Mtakatifu Francisko ametangaza nia ya kutembelea Iraq kunako mwaka 2020, Mwenyezi Mungu akipenda! 

Papa Francisko atangaza nia ya kutembelea Iraq 2020!

Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo yake na wajumbe wa ROACO ametangaza nia ya kutaka kufanya hija ya kitume nchini Iraq katika kipindi cha Mwaka 2020 kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo kwa wahanga wa vita huko Mashariki ya Kati. Papa Francisko amesikitishwa na unafiki wa baadhi ya viongozi wa Serikali wanaozungumzia amani, lakini wanauza silaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Misaada kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO, Jumatatu, tarehe 10 Juni 2019 limeanza mkutano wake wa tisini na mbili kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Tangu mwaka 1968, ROACO kimekuwa ni chombo cha upendo na mshikamano kinachoratibiwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Ni huduma inayotekelezwa kwa namna ya pekee kupitia pia Mabalozi wa Vatican katika nchi hizi bila kusahau mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Wafranciskani waliopewa dhamana ya kulinda maeneo matakatifu.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amegusia yale yaliyojiri tangu walipokutana mara ya mwisho: umuhimu wa kuendeleza Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na waathirika wa vita na mipasuko ya kijamii; changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita pamoja na mchakato wa Kanisa kuendelea kuwekeza katika Injili ya matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwapongeza wajumbe wa ROACO kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini ya leo na kesho iliyo bora kwa Makanisa ya Mashariki ya Kati!

Tangu walipoachana mara ya mwisho, Mwaka Jana, 2018, kumekuwepo na matukio kadhaa katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, amepata fursa ya kujionea mwenyewe Injili ya huduma wakati wa hija zake za kitume huko Bulgaria, Macedonia ya Kaskazini pamoja na Romania. Kwa namna ya pekee kabisa, anakumbuka mkutano wa Sala ya Kiekumene kwa ajili ya Kuombea Amani huko Mashariki ya Kati, ulioadhimishwa mjini Bari, tarehe 7 Julai 2018. Ilikuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukutana, kusali na kutafakari pamoja na ndugu zake wakuu wa Makanisa kutoka Mashariki. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, mkutano mkuu wa ROACO ni fursa ya kusikiliza na hatimaye kujibu kilio cha watu waliopokonywa Injili ya matumaini katika maisha yao, kama ilivyo huko nchini Siria, ambako hali bado ni tete sana.

Kuna watu wanaoteseka kutokana na uhaba wa chakula na lishe bora; ukosefu wa huduma za afya na elimu pamoja na umati mkubwa wa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Hawa ni watu ambao wamejeruhiwa sana nyoyoni mwao, lakini wanayo nafasi ya pekee moyoni mwa Mwenyezi Mungu! Wale ambao wamejeruhiwa wanaweza kukimbilia na kupata hifadhi; huruma, upendo na nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye kwa hakika ni Baba anayewapenda na kuwalinda watoto wake! Baba Mtakatifu anaonya kwamba, iko siku, hasira ya Mungu itawawakia viongozi wanaozungumzia amani, lakini kwa upande mwingine ni wa kwanza kuuza silaha ambazo zinaendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu. Huu ni unafiki na dhambi kubwa machoni pa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapenda kuyaelekeza mawazo yake kwa familia ya Mungu nchini Iraq,  ambako anatarajia kwenda kufanya hija ya kitume mwaka 2020, Mwenyezi Mungu akipenda. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ustawi na mafao ya wengi, utasaidia kuvunjilia mbali chuki na uhasama unaokita mizizi yake katika migogoro ya kidini katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini kimsingi ni mgogoro unaojikita katika uchu wa madaraka. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, awamu ya pili ya ukarabati wa Kaburi Takatifu utaweza pia kuwashirikisha kwa namna ya pekee Wakristo pamoja na viongozi mahalia, ili hatimaye, haki, amani na maridhiano yaweze kutawala kati ya watu, kama alama ya baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Baba Mtakatifu anasema, kuna kilio cha wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta matumaini, lakini hakuna nchi ambayo iko tayari kuwapokea. Bandari zimefungwa kwa wakimbizi na wahamiaji, lakini malango yake yamefunguliwa kwa meli zinazobeba silaha ya maangamizi na zenye gharama kubwa zinazoendelea kusababisha maafa makubwa! Huu ni unafiki mkubwa. Hiki ni kilio cha Abeli kinalomfikia Mwenyezi Mungu. Hawa ni watu wanaotafuta neema, baraka na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watu hawa ni Uso wa Kanisa, unaopaswa kupyaishwa, kwa kutangaziwa na kushuhudiwa Injili ya matumaini, kama walivyokazia Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyoadhimishwa kunako mwaka 2018.

Vijana wanapokutana na mashuhuda aminifu na wa kweli, hawana sababu ya kuogopa na kwamba, wako tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! ROACO iendelee kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa malezi na makuzi ya vijana kiutu na kimaadili na kamwe wasikubali kutekwa na ukoloni wa kiitikadi; wazamishe mizizi ya maisha yao katika mila, tamaduni na mapokeo ya nchi zao, daima wakiwa mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, amani, ustawi na maendeleo yanapatikana kwa ajili ya wote na wala hakuna mtu awaye yote anayeachwa nyuma!

Baba Mtakatifu anasema, kwa mara ya kwanza katika historia, vijana kutoka Ethiopia na Eritrea watashuhudia kuzimika kwa mlio wa silaha, tayari kuanza mchakato unaofumbatwa katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kuheshimiana na kuthamianiana kama ndugu wamoja kama inavyosisitizwa kwenye Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa ROACO kumsaidia kusambaza ujumbe wa Agano hili, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wote wajisikie kwamba wanahusika kikamilifu katika kutekeleza yale yaliyotajwa kwenye hati hii. Dhamana hii ipewe kipaumbele cha pekee anasema Baba Mtakatifu na wadau katika: taasisi za malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya, hasa huko Lebanon na Mashariki ya Kati. Lengo liwe ni kuwawezesha vijana kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa haki, amani na maridhiano kwa watu wote.

Papa: ROACO

 

11 June 2019, 09:54