Tafuta

Papa Francisko: Umisionari ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, ili kukoleza moyo wa toba na wongofu wa ndani! Papa Francisko: Umisionari ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, ili kukoleza moyo wa toba na wongofu wa ndani! 

Mpango Mkakati Mwezi Oktoba 2019: Mkutano Mkuu wa PMS

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 ni muda kwa ajili ya kuwahusisha Wakristo wote ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao. Jukumu la kwanza la Mama Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili, changamoto endelevu, inayohitaji kupewa kipaumbele cha pekee. Umisionari ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, ili kukoleza moyo wa toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwezi Oktoba 2019 Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa. Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu hadi miisho ya dunia!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapaswa kujiekeleza zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili, ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu, ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji!

Haya ni kati ya mambo ambayo yametiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko kwenye barua aliyomwandikia Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa Mashirika haya uliofunguliwa tarehe 27 Mei 2019 na hatimaye, kuhitimishwa hapa mjini Roma hadi tarehe 1 Juni 2019. Mkutano huu umewashirikisha Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anasema, hiki kiwe ni kipindi cha kupyaisha tena ari na moyo wa kimisionari, kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 ni muda uliokubalika, kwa ajili ya kuwahusisha Wakristo wote, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao. Jukumu la kwanza la Mama Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto endelevu, inayohitaji kupewa kipaumbele cha pekee. Umisionari ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, ili kukoleza moyo wa toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka wale wote walioshiriki katika mkutano huu. Watambue kwamba, wao ni mtandao wa sala na upendo wa kimisionari unaotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anawataka kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, huku wakiwa na chapa ya kimisionari na kichungaji.

Papa: Umisionari
04 June 2019, 09:42