Papa Francisko anakazia uekumene wa umoja katika utofauti kwa kukikita katika ushuhuda wa Injili ya huduma kwa maskini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Papa Francisko anakazia uekumene wa umoja katika utofauti kwa kukikita katika ushuhuda wa Injili ya huduma kwa maskini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! 

Papa Francisko: Majadiliano ya kiekumene: Umoja katika huduma!

Msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu Uekumene ni kujenga umoja katika utofauti. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza viongozi na waamini wa Makanisa haya kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana, ili kushirikishana na kuhudumiana ili kuvunjilia mbali hofu na mashaka yasiyokuwa na mashiko, tayari kujenga umoja wa Kanisa. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 28 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol unaoshiriki katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amesema kwamba, huu ni ushuhuda wa hija ya pamoja inayopania kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa, kadiri ya mapenzi ya Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja, dunia ipate kuamini! Kadiri ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa, watakatifu Petro na Paulo, wanaadhimishwa siku moja kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi, mwaliko wa kupyaisha upendo unaozalisha umoja!

Waamini wanakumbushwa kuwa na ujasiri wa kitume ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Injili ya Kristo Yesu! Waamini waendelee kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote ili kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani mintarafu mwanga wa Injili. Baba Mtakatifu anampongeza na kumshukuru sana Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa kuendelea kujipambanua katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, kwa hakika mchango wake ni amana na utajiri wa Kanisa zima.

Huyu ni kiongozi ambaye hata viongozi wa Makanisa mengine ya Kiorthodox kama ilivyo kwa Kanisa Katoliki wanapenda kushirikiana naye katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; umuhimu wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji pamoja na kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko amekumbushia kuhusu hija yake ya kitume nchini Bulgaria na Romania ambako alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox katika nchi hizi, akashuhudia imani, busara, hekima na utajiri wa maisha ya kiroho kutoka kwa viongozi hawa wa Kanisa.

Kwa kuunganisha Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki, sanjari na kuendelea kuheshimu utambulisho wa Makanisa haya kunaweza kukuza umoja katika utofauti wake. Ni kazi ya Roho Mtakatifu kuratibu karama mbali mbali kwa ajili umoja na upendo wa Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, msimamo wa Kanisa Katoliki ni kujenga umoja katika utofauti na wala hakuna sababu msingi ya kumeza Makanisa mengine. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza viongozi na waamini wa Makanisa haya kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana, ili kushirikishana na kuhudumiana ili kuvunjilia mbali hofu na mashaka yasiyokuwa na mashiko, tayari kujenga umoja wa Kanisa.

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana na kamwe wasikubali kumezwa tena na historia iliyopita ya kuwa na maamuzi mbele. Ukweli na uwazi, utawasaidie waamini kupendana na kuheshimiana kama wanavyopendwa na Kristo Yesu; wataweza kushikamana kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao na kwamba, kuna mambo mengi yanayowaunganisha ikilinganishwa na yale yanayowatenganisha. Kumbe, huu ni wakati wa kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe hawa na kuwaombea kumfikishia Patriaki Bartolomeo wa kwanza salam na matashi mema yeye binafsi pamoja na Sinodi nzima ya Kanisa la Kiothodox.

Papa: Umoja wa Kanisa

 

28 June 2019, 18:04