Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Papa Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Simameni kidete kulinda na kudumisha uhai!

Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Kama waamini wanahamasishwa: kuilinda na kuidumisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu, hata pale watu wanapokumbana na magonjwa na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Hakuna mwenye haki ya “kufyekelea mbali zawadi ya maisha ya binadamu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 12 Juni 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, baada ya Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume, amewaambia waamini na mahujaji waliofurika kwa wingi mjini Vatican kwamba, Kanisa limezaliwa kutoka katika nguvu ya Fumbo la Ufufuko. Mwanga wa Kristo Mfufuka katika Jumuiya ya kwanza ya Wafuasi wa Kristo umevunjilia mbali ubinafsi na woga dhidi ya wafuasi wengine. Mwanga huu ukawahamasisha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa Kanisa hadi miisho ya dunia! Huko, wakatangaza na kushuhudia upendo wa Mungu uliomwilishwa katika umoja na ushirikiano; ushuhuda na udugu! Hii ni changamoto kwa Wakristo kuendelea kuishi katika umoja unaofumbatwa katika utofauti wao kama ulivyoshuhudiwa na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwakumbusha waamini kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama waamini wanaitwa na kuhamasishwa kulinda, kuitunza na kuidumisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu, hata pale watu wanapokumbana na magonjwa pamoja na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Hakuna mwenye haki ya “kufyekelea mbali zawadi ya maisha ya binadamu”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, uhai wa binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa na kwa njia hii, kuwekza kutangaza na kushuhudi tunu msingi za maisha ya Kikristo katika mazingira ya kifamilia. Baba Mtakatifu amehitimisha Katekesi yake kwa kusema kwamba, Sherehe ya Pentekoste inafunga rasmi shamara shamra za Sherehe ya Pentekoste.

Papa: Uhai
12 June 2019, 14:47