Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, kimsingi askofu ni mhudumu, mchungaji, baba, na ndugu na kamwe si mfanyabiashara! Papa Francisko asema, kimsingi askofu ni mhudumu, mchungaji, baba, na ndugu na kamwe si mfanyabiashara!  (Vatican Media)

Papa: Askofu ni: Mhudumu, Mchungaji, Baba & Ndugu!

Uaskofu ni huduma na wala si heshima; anaitwa kuongoza na wala si kutawala kwani uongozi ni huduma inayotekelezwa kwa unyenyekevu. Baba Mtakatifu anasema, kimsingi Askofu ni: mhudumu, mchungaji, Baba na Ndugu na kamwe si mfanyabiashara! Askofu anatumwa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kwa wakati unaofaa na wakati usiofaa. Kufundisha, Kuongoza na Kutakatifuza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Kristo Yesu,  maarufu kama “Corpus Domini” Jumamosi, tarehe 22 Juni 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kumweka wakfu Monsinyo Alberto Ricardo Lorenzelli Rossi, S.D.B., aliyeteuliwa tarehe 22 Mei 2019 kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Santiago, nchini Chile. Kanisa la Kitume ni chemchemi ya Sakramenti ya daraja takatifu ambalo kimsingi limegawanyika katika madaraja makuu matatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi, kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Daraja takatifu ni mwendelezo wa utume unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambalo Mitume, walikabidhiwa na unaendelezwa na waandamizi wao ambao ndio Maaskofu. Chini ya Kristo Yesu, wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, sehemu muhimu sana ya Mapokeo ya Kanisa, kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ya ukombozi hadi utimilifu wa dahali. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Askofu anapozungukwa na wakleri wake atambue kwamba, Kristo Yesu yuko kati yao kama Kuhani mkuu. Yesu kwa njia ya Askofu anaendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu; anaendelea kuwatakatifuza waamini kwa njia ya Sakramenti na imani ya Kanisa.

Yesu anaendelea kulikuza na kuliimarisha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa, kwa kulipatia watoto wapya wanaozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Kwa njia ya hekima na busara ya Askofu, Kristo Yesu, anaendelea pia kuwaongoza watu wa Mungu kuelekea katika furaha na maisha ya uzima wa milele! Baba Mtakatifu amewaalika Maaskofu kumpokea Askofu Alberto Ricardo Lorenzelli Rossi katika urika wao. Apewe heshima kama anavyostahili mtumishi wa Kristo Yesu na mgawaji wa mafumbo ya Mungu na kama kiongozi aliyekabidhiwa ushuhuda wa Injili na Roho Mtakatifu. Askofu ni kiongozi anayepaswa kusikilizwa kwa makini na kwa kufanya hivi, watakuwa wanamsikiliza pia Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu amemkumbusha Askofu Alberto Ricardo Lorenzelli Rossi kuwa ameteuliwa miongoni mwa watu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kukumbuka asili yake. Ameteuliwa kwa ajili ya mambo yanayomhusu Mungu. Uaskofu ni huduma na wala si heshima; anaitwa kuongoza na wala si kutawala kwani uongozi ni huduma inayotekelezwa kwa unyenyekevu. Baba Mtakatifu anasema, kimsingi Askofu ni: mhudumu, mchungaji, Baba na Ndugu na kamwe si mfanyabiashara! Askofu anatumwa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kwa wakati unaofaa na wakati usiofaa. Askofu akaripie kwa ujasiri na kuhimiza utekelezaji wa mafundisho ya Kanisa kwa ari na moyo mkuu.

Askofu awe ni mtu wa sala na anayetolea sadaka kwa ajili ya watu wake. Awe ni kiongozi anayechota utajiri wa maisha na utume kwa ajili ya Familia ya Mungu katika chemchemi ya: Maandiko Matakatifu, Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Sakramenti za Kanisa, Jumuiya ya waamini na marafiki wa Yesu waliojipambanua kwa maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Askofu ajitahidi kuchota utimilifu wa utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo na utajiri wa neema ya Mungu. Askofu awe mgawaji mwaminifu wa Mafumbo ya Kristo, mkuu wa familia yake, anayepaswa kuiga mfano wa Kristo mchungaji mwema anayewafahamu Kondoo wake na wao wanamtambua na kwamba, yuko tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili yao!

Askofu awe karibu sana na watu wake na ajitahidi kadiri anavyoweza kuwafahamu vyema; awepende na kuwathamini wote waliowekwa chini ya uongozi wake. Atoe upendeleo wa pekee kwa wakleri ambao ni wenza katika mchakato wa uinjilishaji. Awe tayari na mwepesi kupatikana kwa mapadre wake wanapomtafuta bila ukiritimba. Baba Mtakatifu amehitimisha wosia wake kwa Askofu mpya kwa kusema, Askofu anapaswa kuwa karibu na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na ukarimu. Mwishoni, lakini muhimu; Askofu ajitahidi kuwashirikisha waamini walei katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, pamoja na kuwasikiliza wote kwa umakini mkubwa!

Itakumbukwa kwamba, Askofu Alberto Ricardo Lorenzelli Rossi alizaliwa tarehe 2 Septemba 1953 huko Isidro Casanova, Buenos Aires, Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, tarehe 24 Januari 1981 akaweka nadhiri kwenye Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco. Katika maisha na utume wake kama Padre na mtawa amewahi kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi ndani na nje ya Italia. Kuaniza tarehe 1 Machi 2012 hadi Januari 2018 alikuwa ni mkuu wa Shirika Kanda ya Chile! Kunako mwaka 2018 akateuliwa kuwa mlezi wa maisha ya kiroho, kurugenzi ya ulinzi na usalama wa raia mjini Vatican. Tarehe 22 Mei 2019 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Santiago nchini Chile!

Papa: Daraja

 

23 June 2019, 16:24