Tafuta

Vatican News
Monsinyo Alberto Ricardo Lorenzelli, Askofu mteule wa Jimbo Katoliki la Santiago, Chile, anatarajiwa kuwekwa wakfu na Papa Francisko, tarehe 22 Juni 2019. Monsinyo Alberto Ricardo Lorenzelli, Askofu mteule wa Jimbo Katoliki la Santiago, Chile, anatarajiwa kuwekwa wakfu na Papa Francisko, tarehe 22 Juni 2019.  (� Vatican Media)

Papa Francisko kumweka wakfu Mons. Alberto R. L. Rossi kuwa Askofu

Askofu mteule Alberto Ricardo Lorenzelli Rossi alizaliwa mwaka 1953 huko, Buenos Aires, Argentina. Tarehe 24 Januari 1981 akaweka nadhiri kwenye Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco. Tarehe 1 Machi 2012 hadi Januari 2018 alikuwa ni mkuu wa Shirika Kanda ya Chile! Kunako mwaka 2018 akateuliwa kuwa mlezi wa maisha ya kiroho, kurugenzi ya ulinzi na usalama wa raia mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Jumamosi, tarehe 22 Juni 2019, majira ya saa 12:00 za jioni kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Ibada hii, atamweka wakfu, Monsinyo Alberto Ricardo Lorenzelli Rossi, S.D.B., aliyeteuliwa tarehe 22 Mei 2019 kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Santiago, nchini Chile. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Alberto Ricardo Lorenzelli Rossi alizaliwa tarehe 2 Septemba 1953 huko Isidro Casanova, Buenos Aires, Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, tarehe 24 Januari 1981 akaweka nadhiri kwenye Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco. Katika maisha na utume wake kama Padre na mtawa amewahi kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi ndani na nje ya Italia.

Kuaniza tarehe 1 Machi 2012 hadi Januari 2018 alikuwa ni mkuu wa Shirika Kanda ya Chile! Kunako mwaka 2018 akateuliwa kuwa mlezi wa maisha ya kiroho, kurugenzi ya ulinzi na usalama wa raia mjini Vatican. Tarehe 22 Mei 2019 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Santiago nchini Chile! Kanisa la Kitume ni chemchemi ya Sakramenti ya daraja takatifu ambalo kimsingi limegawanyika katika madaraja makuu matatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi, kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Askofu anapaswa kuwa ni shahidi wa Kristo Mfufuka; Ukuu wa Mungu katika uchaguzi wa Maaskofu wapya; Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachamungu, watu wa sala na wachungaji wema. Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa sala, kiongozi anayejipambanua kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake adili na matakatifu.

Ni kiongozi anayepaswa kuwa kweli ni mchungaji mwema, anayetambulikana pia kutokana na harufu ya kondoo wake, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Kimsingi haya ndiyo mambo muhimu ambayo yanapaswa kuoneshwa na kushuhudiwa na Askofu au wale wanaotamani kufikia utimilifu wa Daraja Takatifu la Upadre Askofu anapaswa kuwa ni shahidi aminifu wa Kristo na Kanisa lake; mtu wa sala na tafakari ya Neno la Mungu; kiongozi ambaye ataonesha kwa maneno na maisha yake kwamba, uongozi kwake ni huduma na wala si cheo! Kwa wanajimbo wake anapaswa kuwa kweli ni mfano wa Baba na Kaka; mpole na mnyenyekevu wa moyo, mwingi wa huruma na mapendo; mvumilivu na mwenye hekima na busara! Awe ni kiongozi anachota utajiri wa maisha na utume kwa ajili ya Familia ya Mungu katika chemchemi ya:Maandiko Matakatifu, Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Sakramenti za Kanisa, Jumuiya ya waamini na marafiki wa Yesu waliojipambanua kwa maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Kwa maneno mengine hawa ni kama vile Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, Mitume, Watakatifu na wafiadini; watu waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Askofu awe ni kiongozi mwenye ari na mwamko wa kimissionari anayetaka kuhakikisha kwamba, watu wanaendelea kutangaziwa Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha. Waamini wajisikie kuwa ni sehemu kubwa ya Familia ya Mungu inayowajibika. Askofu awe ni Baba mwema anayejitaabisha kuwachanga kondoo wake, kwa kuwaonesha dira na mwelekeo wa maisha; daima akikazia umoja, upendo na mshikamano, ili kati ya Kondoo wake, asiwepo anayepotea njia, Askofu awe kweli ni kiongozi anayekesha kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Kanisa la Kristo, pasi na kumezwa na malimwengu.

Papa: Uaskofu
21 June 2019, 14:41