Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 15 Juni 2019 ameongoza Ibada ya Mazishi ya Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina! Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 15 Juni 2019 ameongoza Ibada ya Mazishi ya Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina! 

Papa Francisko aongoza mazishi ya Askofu mkuu Lèon Kalenga!

Baba Mtakatifu anasema, maisha yawafundishe waamini kusema buriani kama wachungaji, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo na kama ilivyokuwa kwa Yesu na wengine kama hata ilivyo kwa Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele. Viongozi wa Kanisa waanze kujiandaa kuagana na ndugu zao, wanapohamishwa kwenye maeneo ya kazi, lakini zaidi, wanapokwenda nyumbani kwa Baba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 15 Juni 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina. Askofu mkuu Kalenga amefariki dunia tarehe 12 Juni 2019! Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekumbushia kwamba, Ibada hii ya Misa Takatifu itahitimishwa na buriani kwa Askofu mkuu Kalenga, kwa kuiweka roho yake mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwani Maandiko Matakatifu yanasema bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu. Hii ni mikono safi, iliyokunjwa kwa upendo na huruma.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo mikono ambayo, Mama Kanisa anapenda kuikabidhi roho ya Marehemu Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele. Hii ni buriani kwa mchungaji kama alivyofanya Mtakatifu Paulo huko Mileto alipokuwa anawaaga wazee wa Kanisa la Efeso wakapiga magoti, wakaomba sana, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusubusu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mchungaji anawaaga watu wake kwa ushuhuda wa maisha yanayofumbatwa katika unyenyekevu, ari na moyo mkuu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni ushuhuda unaofumbatwa katika Utii kwa Mungu, Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu.

Mchungaji ambaye hakumezwa na malimwengu anashuhudia, kwa kusema kwamba, hawatauona tena uso wake! Anawataka kutunza nafsi zao, kupambana na kwamba, wao kwa sasa wamekuwa na kukomaa, wanaweza kujiongoza wenyewe. Mchungaji anawaaga watu wake kwa unabii, kwa kutambua kwamba, baada ya kuondoka kwake mbwa mwitu wakali wataingia kwao, wasilihurumie kundi. Mwishoni anasali na kuwaweka katika mikono ya Mwenyezi Mungu, na kwa neno la neema yake, ili kuwajenga na kuwapata urithi na wale wote waliotakaswa! Baba Mtakatifu anasema, huu ni ushuhuda wa Mtakatifu Paulo, Mtume, huko Mileto!

Pengine huu ndio ungeweza kuwa ushuhuda kutoka kwa Marehemu Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele kwa ndugu zake, familia ya Mungu nchini Argentina, El Salvador na sehemu mbali mbali ambako alikwenda kumwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro! Mwishoni, bila shaka anasema Baba Mtakatifu, angeweza kuwaaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu aliwaaga Mitume wake, kwa matumaini akisema kwamba, alikuwa anakwenda kuwaandalia mahali na wao wangeweza kumfuata baadaye, kama sehemu ya hatima ya maisha yao, yaani matumaini.

Maisha ya mwanadamu ni safari inayomwandaa kukabiliana na fumbo la kifo, ambalo kamwe haliwezi kuzoeleka! Baba Mtakatifu anasema, maisha yawafundishe waamini kusema buriani kama wachungaji, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo na kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu na wengine kama hata ilivyo kwa Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupiga hatua ya kuanza kujiandaa kuagana na kondoo wao, wanapohamishwa maeneo ya kazi, lakini zaidi, wajiandae kusema buriani, kwa herini ninakwenda kwa Baba wa milele. Waamini waombe neema na baraka ya kujifunza kuagana na Kondoo wao!

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Kalenga Badikebele alizaliwa kunako tarehe 17 Julai 1956 huko Kamina, nchini DRC. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 5 Septemba 1982 na kuingizwa Jimboni Luebo, DRC. Alianza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican tarehe 27 Februari 1990. Tangu wakati huo, akatumwa kutekeleza dhamana na utume huu huko nchini Haiti, Guatemala, Zambia, Misri, Zimbabwe na Japan kwa nyakati mbali mbali. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, tarehe 1 Machi 2008 akamteuwa kuwa Askofu mkuu na hatimaye, kuwekwa wakfu Mei Mosi, 2008 na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati ule na kutumwa kwenda nchini Ghana kama Balozi wa Vatican.

Tarehe 22 Februari 2013, akateuliwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini El Salvador, Belize na Antilles. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Machi 2018 akatemteua kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Argentina. Apumzike katika usingizi wa amani na astahilishwe kupokea tuzo ya maisha na uzima wa milele kwa mafumbo aliyokuwa anaadhimisha!

Papa: Misa: Leon
15 June 2019, 15:13