Tafuta

Papa Francisko: Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni: Kauli mbiu "Kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo" (Efe. 4:25) Papa Francisko: Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni: Kauli mbiu "Kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo" (Efe. 4:25) 

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO KWA SIKU YA 53 YA UPASHANAJI HABARI DUNIANI 2019

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 2 Juni 2019 unaoongozwa na kauli mbiu "Kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo" (Efe. 4:25): Kutoka Jumuiya ya mtandaoni kwenda kwenye Jumuiya halisi ya watu! Hii ni changamoto ya ujenzi wa Jumuiya halisi ya binadamu!

Na Shemasi Karoli Joseph AMANI – Vatican.

Katika Kipindi ambapo mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii yamechukua hatamu, Baba Mtakatifu Francisko amehimiza na kusisitiza umumimu na kiini cha kiu ya mwanadamu kuishi katika mahusiano na wengine licha ya changamoto mbalimbali zinazokabili mawasiliano hivi leo. Internet imeleta mageuzi makubwa akatika mtindo wa kuishi wa mwanadamu katika zama hizi mintarafu mawasiliano na upatikanaji wa taarifa na maarifa. Aidha, internet kwa upande mwingine imezidisha hatari na kasi ya upatikanaji na usambazi wa habari potofu ikiwa ni pamoja na kudhuru undani wa watu binafsi. Pamoja na kuwa nyenzo ya kuwakutanisha watu bila kujali umbali walipo, internet inatumiwa pia kama nyenzo ya kupata taarifa za siri juu ya watu na kuzitumia kwa malengo ya kibinafsi husasan kisiasa na kiuchumi bila kujali hadhi na haki za wahusika. Takwimu zinaonesha kwamba kijana mmoja kati ya wanne ni mhanga wa ukatili wa kimtandao (cyber bullism).

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, si vigumu leo hii kuonja ile ari ya kutamani kutengeneza jumuiya ndani ya mitandao ya kijamii ambamo watu hukutana mkondoni. Ari hii inadhihirisha tamanio la binadamu kuishi ndani ya jumuiya na kwamba dhana ya mtandao katika umaana wake inaweza pia kubeba ndani yake dhana jumuiya. Pamoja na hayo, ni ukweli kwamba hata kama watu hutengeneza jumuiya kupitia makundi sogozi mitandaoni, sababu za kuunda makundi hayo ya kuwakutanisha hazikabiliani vya kutosha na changamoto zinazohitaji uwepo halisi wa mtu ndani katika jumuiya. Mitandao ya kijamii haijafanikiwa kuchukua nafasi ya jumuiya halisi ya watu. Vilevile katika mitandao watu huvutwa kutambuana Zaidi kutokana na yale mambo yanayowatofautisha kuliko yanayowaunganisha; mfano jinsia, rangi, utaifa, dini na muonekano na hivi kile kilichopaswa kuwa dirisha la kuwaunganisha watu kinakuwa kioo cha kuang’azia ubinafsi wa watu.

Mitandao imegeuka kindumbwendumbwe kinachowaburuza vijana kutamani zaidi maisha mkondoni kuliko katika uhalisia. Inashambulia kwa jamii na kuharibu mahusiano asilia baina ya watu. Janga hili linahitaji hatua za haraka kwani linakuza kasi ya watu kujigenisha katika jamii. Idadi ni kubwa ya vijana ambao wanahangaika kutafuta mbinu mbadala ya kuwasaidia kutumia mitandao ya kijamii katika namna komavu na ya kiuwajibikaji. Katika hili, Kanisa halina budi kuwa mwenza wa safari. Ili kuielewa zaidi mitandao ya kijamii haitoshi tu kujiunga nayo, mingi kadiri inavyowezekana. Yafaa kubuni mbinu za kuweza kukuza uwajibikaji na uelewa zaidi wa nafasi ya jumuiya katika mitandao ya kijamii.

Baba Mtakatifu anabainishwa kwamba utajiri wa Maandiko Matakatifu ni kimbilio katika kubuni suluhisho la changamoto zilizoko mbele yetu kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii. Akidadavua mfano wa Mtume Paolo husika na mahusiano katika jumuiya anakaza kusema, Ukweli ni kiungo msingi katika kulinda mahusiano ya watu katika jumuiya. ‘‘kwa hiyo acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo’’ (Efe 4, 25). Kumbe, kila mmoja anapaswa kujibidiisha kufyekelea mbali majungu, usengenyaji na kujikwezakweza, mambo ambayo hufifisha ukweli wa uhalisia wa maisha ya watu hasa kupitia machapisho katika mitandao ya kijamii. Uongo hutia ukakasi umoja wa watu katika jumuiya na zaidi humfanya mwongo mwenyewe ashindwe kujitambua mwenyewe na nafasi yake katika kuijenga jumuiya.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia kusema, kama wakristo utambulisho wetu ni udugu kama vile wana familia moja yaani Kanisa, Mwili mmoja ambao kichwa chake ni Kristo Yesu Mwenyewe. Umoja wetu unaofumbatwa katika Imani moja Takatifu Katoliki ya Mitume ambayo kwayo tunatambuana na kuwatazama wengine kama watoto wa Mungu na sio mtaji wa kujitajirishia. Kwetu wakristo hata adui haitaji kujitambulisha kwani Kristo ametufundisha kuwatambua walio tofauti na sisi katika mtazamo mpya. Tunajifunza kutoka kwa Mungu mwenyewe aliye katika uhusiano wa mapendo katika Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja ambaye haishi katika ubinafsi bali katika mawasiliano ya kimapendo. Ni upendo ambao hauishii kwa wenyewe bali umetolowa katika Nafsi ya pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kristo Yesu ambaye kwaye Mungu anahusiana na wanadamu na kujitambulisha mwenyewe kwao na hivi kuweka nafasi ya majadiliano baina ya Mungu na wanadamu (Dei Verbum 2).

Kwa kutuumba kwa mfano wake, Mwenyezi Mungu ameweka mioyoni mwetu kiu ya kuwa katika mahusiano naye. Kiu hii haiwezi kuzimika kamwe. Kwa sababu hiyo tunayo pia kiu ya kuwa katika mahusiano na wengine na hivyo kuishi katika jumuiya. Baba Mtakatifu anazidi kusema, Mt.Basili anatufundisha kwamba, ‘hakuna kilicho cha pekee katika asili ya mwanadamu kama kuwa katika mahusiano na kuwahitaji wengine’. Kumbe ni wajibu kwa wakristo kutambua kwamba Imani yetu ni tunda la mahusiano ya kijumuiya iliyo katika mahusiano yaliyojikita katika Upendo.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake wa Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2019 kwa kueleza kwamba mitandao ya kijamii ikitumika kuwakutanisha watu kiuhalisia uso kwa uso, itakuwa imetimiza shabaha yake katika kuboresha mahusiano na maisha ya mwanadamu kiujumla. Ikiwa katika familia watu wataunganishwa kwa mitandao kukutana pamoja na kushiriki mlo wakitazamana machoni na si kutazama luninga au simu zao za viganjani basi hapo mitandao itakuwa mtaji wa umoja. Ikiwa wanaparokia wanaunganishwa kwa mtandao kuandaa na badaye kushiriki kwa pamoja adhimimisho la Ekaristi Takatifu, basi mitandao ni hazina.

Hii ndiyo aina ya mitandao tunayotaka. Mitandao yenye uwezo wa kulinda jumuiya zetu na kukuza mawasiliano halisi siyo bandia. Kanisa pia ni mtandao, mtandao ambao asili na kilele chake  ni Ekaristi Takatifu si kwa wingi wa washiriki ‘like’ bali katika Ukweli wa ile ‘amina’ ambayo kwayo kila mmoja ana amini kuwa anapokea mwili wa Kristo katika utayari wa kuwakaribisha wengine.

Papa: Ujumbe Upashanaji

 

30 May 2019, 18:03