Tafuta

Siku ya Wafanyakazi Duniani: Chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi! Mwanzo wa Mwezi wa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Siku ya Wafanyakazi Duniani: Chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi! Mwanzo wa Mwezi wa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. 

Siku ya Wafanyakazi Duniani 2019: Ulinzi na tunza ya Mt. Yosefu

Siku ya Wafanyakazi Duniani: Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Awalinde na kuwasaidia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, awaombee wale wote ambao wamepoteza fursa za ajira na kazi au ambao bado wanachakarika kutafuta fursa za kazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, Mei Mosi, 2019 amewakumbusha waamini kuhusu kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi. Kutokana na ugumu wa dhambi ya asili, Kristo Yesu alitoa mwelekeo mpya wa kazi, kuwa ni kielelezo cha ukombozi. Kielelezo cha kazi na utume huu, ni mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu! Mama Kanisa katika huruma na upendo wake, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, Papa Pio XII kunako mwaka 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi duniani.

Mkazo kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi kwa juhudi na maarifa, ili kuweza kujipatia: mali na mapato halali; watambue na kuheshimu kazi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Awalinde na kuwasaidia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, awaombee wale wote ambao wamepoteza fursa za ajira na kazi au ambao bado wanachakarika kutafuta fursa za kazi!

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Mwezi Mei, umetengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya kumheshimu Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Waamini katika ibada na matukio mbali mbali kama mtu binafsi au jumuiya, wasali kwa ajili ya kuliombea Kanisa, kuombea: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika nchi zao, bila kusahau kuombea amani duniani! Katika kipindi hiki cha Pasaka, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Mfufuka, ili kumshirikisha furaha, magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amewafungulia waja wake njia ya kwenda mbinguni! Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha uhusiano mwema na urafiki na Baba yao wa mbinguni kwa njia ya ushuhuda wa wema, upendo na huruma yake isiyokuwa na kifani!

Mei Mosi, Mwaka 2019, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 500 tangu Mtakatifu Francesco wa Paola alipotangazwa kuwa Mtakatifu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani; sanjari na upendo wa Mungu unaomwilishwa kwa jirani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Jumapili Ijayo, Kanisa nchini Italia, litaadhimisha Siku ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sacro Cuore, “Moyo Mtakatifu wa Yesu”. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Chuo hiki kitaendelea kuwa mahali muafaka pa malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya na jukwaa la majadiliano kati ya imani  na maswali yanayoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo!

Papa: Mwezi Mei 2019
01 May 2019, 15:19