Tafuta

Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, tarehe 24 Mei 2019 kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo nchini China! Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, tarehe 24 Mei 2019 kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo nchini China! 

Siku kuu ya B. Maria Msaada wa Wakristo: Siku ya Kuombea China!

Papa Francisko: Tarehe 24 Mei, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, anayeheshimiwa sana kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Sheshan, huko Shanghai, nchini China. Hii ni siku maalum ambayo, Wakristo wote wanaungana kiroho na waamini Wakatoliki wanaoishi nchini China ili kusali na kuwaombea ili waendelee kuamini, kutumaini na kupenda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 22 Mei 2019, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, anayeheshimiwa sana kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Sheshan, huko Shanghai, nchini China. Hii ni siku maalum ambayo, Wakristo wote wanaungana kiroho na waamini Wakatoliki wanaoishi nchini China ili kusali na kuwaombea katika shida, magumu na changamoto za maisha waendelee kuamini, kutumaini na kupenda.

Bikira Maria, Malkia wa mbingu, awasaidie ili wote waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo na udugu kwa kudumisha umoja na mshikamano na Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia sala zake za daima! Itakumbukwa kwamba, Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, ilianzishwa na Papa Pio wa VII kunako mwaka 1815. Huu ulikuwa ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Bikira Maria msaada wa Wakristo, ili awawezeshe kuwa na ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Kunako mwaka 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II, akamtangaza Bikira Maria kuwa ni Mama na msimamizi wa Familia ya Mungu nchini China. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akatangaza tarehe 24 Mei ya kila Mwaka kuwa ni Siku ya Kuombea China. Tangu wakati huo, Kanisa zima linakimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa ajili ya familia ya Mungu nchini China; siku ambayo China pia inaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Sheshan.

Papa: China 2019
22 May 2019, 14:25