Katika maadhimisho ya Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani 2019: Papa Francisko ametoa daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 19. Katika maadhimisho ya Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani 2019: Papa Francisko ametoa daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 19. 

Ushauri kwa Mapadre Wapya: Biblia, Sala, Sakramenti & Umoja!

Papa Francisko anawataka Mapadre wapya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Mahubiri yao, yapate chimbuko lake katika Neno la Mungu na katika maisha ya Sala, ili kujenga na kuliimarisha Kanisa la Mungu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, maadhimisho ya Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2019, anawaalika waamini kuungana kwa pamoja, kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kugundua mpango wake wa upendo katika maisha yao. Wamwombe, awajalie ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, tarehe 12 Mei 2019 ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 19.

Baba Mtakatifu katika wosia wake kwa Mapadre wapya amewataka kutambua kwamba, wao ni Makuhani wa Agano Jipya, wanaoshirikishwa Ukuhani wa Kristo ili kuendeleza utume wake wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kristo Yesu katika maisha yake, alikuwa ni Bwana, Kuhani na Mchungaji mwema. Mapadre wapya wakiwa wameungana na Askofu mahalia, watakuwa ni watangazaji wa Neno la Mungu, Wachungaji wa waamini na kwa namna ya pekee, wataadhimisha Mafumbo ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre wapya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Mahubiri yao, yapate chimbuko lake katika Neno la Mungu na katika maisha ya Sala, ili kujenga na kuliimarisha Kanisa la Mungu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Mapadre wawe makini sana wanapoadhamisha Fumbo hili la Wokovu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka ya Kristo Altareni. Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu wanapoadhimisha Mafumbo ya Kanisa; kwa kuwatembelea wagonjwa na wazee.

Mapadre watekeleze maisha na utume wao, kwa furaha, upendo, uaminifu na ukweli, daima wakijitahidi kuwa karibu na watu wanaowahudumia. Mapadre wajenge na kudumisha uhusiano mwema na Askofu mahalia pamoja na wakleri wenzao! Daima Kristo Mchungaji mwema, awe mbele ya macho yao kama kiongozi, ambaye hakuja ulimwenguni kutumikiwa, bali kutumikia na kuyatoa maisha yake ili yawe ni fidia ya wengi! Amekuja ili kutafuta na kuokoa kile kilichopotea!

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Padre Alessandro Caserio, mwenye Umri wa Miaka 38 anamshukuru Mungu kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre. Katika maisha yake, alijitahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, akafikiri namna ya kuanzisha familia kwa kupata mchumba mwema, lakini daima ndani mwake, hakupata utulivu na kuhisi kana kwamba kulikuwa na ombwe zito katika maisha yake. Cheche za wito ulianza kupenyeza ndani mwake kwa njia ya huduma kwa maskini, kiasi cha kuthubutu kuacha kazi, marafiki waliokuwa wanamzunguka, furaha na anasa za dunia na kuamua kuingia seminarini, tayari kuanza safari ya malezi na majiundo ya Kipadre na hatima yake ni hapo tarehe 12 Mei 2019 alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Ukomavu wa wito wake wa Kipadre ni matunda ya malezi na makuzi ya Kikristo kutoka kwenye familia yake, lakini Mama yake Mzazi alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, watoto wake wanasali, wanatafakari Neno la Mungu na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Ka upande wake, Padre Johnny Joseph kutoka Haiti anasema, kipaumbele chake cha kwanza anapohitimisha masomo yake, ni kurejea mara moja nchini Haiti, ili kuwahudumia ndugu zake wanaopambana na hali ngumu ya maisha hasa kutokana na majanga asilia ambayo yamewatikisa sana kwa miaka ya hivi karibuni. Ni matumaini ya walezi wao kwamba, Mapadre wapya wataendelea kuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili; huduma ya upendo, mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kati ya waja wake!

Papa: Mapadre Wapya 2019
13 May 2019, 09:31