Wajumbe wa Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, Jumatano tarehe 22 Mei 2019 wamekutana na Papa Francisko. Wajumbe wa Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, Jumatano tarehe 22 Mei 2019 wamekutana na Papa Francisko. 

Mkutano wa Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani!

Mama Evaline Malisa Ntenga kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, ni kati ya wajumbe 30 wa Bodi ya Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki waliokupo kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kushiriki Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kama hitimisho la mkutano wa Bodi: Sala ya Baba Yetu! Roho Mtakatifu, Msamaha! Big Up WAWATA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wajumbe wa Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, ni kati ya mahujaji walioshiriki kikamilifu katika katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tarehe 22 Mei 2019. Shirikisho hili linawaunganisha wanawake wakatoliki zaidi ya milioni 8 kadiri ya taarifa iliyotolewa na Mama Maria Lìa Zervino, Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani. Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki vimekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Kanisa kuanzia kwenye vigango.Ni wadau wakuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Shirikisho hili katika kipindi cha mwaka 2020 linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 110 tangu kuanzishwa kwake! Mama Evaline Malisa Ntenga kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, ni kati ya wajumbe 30 wa Bodi ya Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki waliokupo kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kushiriki Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kama hitimisho la mkutano wa Bodi. Bara la Afrika limewakilishwa na wajumbe kutoka: Kenya, Mali, Malawi, Pwani ya Pembe, Senegal, Gabon, Eswatin ambayo kwa wengi inafahamika kama Swaziland pamoja na Tanzania.

Mama Evaline Malisa Ntenga katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakiri kwamba, ameguswa sana na Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewakumbusha umuhimu wa Sala ya Wakristo katika maisha yao, kielelezo makini cha muungamano na mafungamano ya imani, matumaini na mapendo. Waamini watambue kwamba, mhusika mkuu ni Roho Mtakatifu anayewapatia mapaji na nguvu ya kuthubutu kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka. Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba kwa njia ya Mwana, ili awafundishe, awakumbushe, alitakatifuza Kanisa na kuwasaidia waamini kuwa vyombo na mashuhuda wa Kristo Mfufuka, huku akiwaongoza katika kweli na haki.

Karama na mapaji ya Roho Mtakatifu yawasaidia waamini kulijenga Kanisa! Mama Evaline Malisa Ntenga anasema, Baba Mtakatifu amekazia pia umuhimu wa msamaha katika maisha ya Wakristo kama utambulisho wa ufuasi wao kwa Kristo Yesu, ambaye amewafundisha kusamehe na kusahau na kuwataka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu duniani! Kwa njia ya uwepo endelevu wa Roho Mtakatifu, waamini si pweke! Mama Evaline Malisa Ntenga anakiri kwamba, amejifunza mambo mengi wakati wa mkutano wao hapa Roma. Kwa namna ya pekee kabisa, anawashukuru WAWATA Tanzania kwa kumwezesha kushiriki kwa karibu zaidi katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Wanawake Wakatoliki Duniani wanazo nyenzo kumbe wanapaswa kuwajibika na kutumika kwa kusoma alama za nyakati!

Papa: Wanawake
23 May 2019, 16:05