Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anaitaka Caritas Internationalis kukita mizizi yake katika mambo makuu matatu: Upendo, Maendeleo fungamani ya binadamu na umoja! Papa Francisko anaitaka Caritas Internationalis kukita mizizi yake katika mambo makuu matatu: Upendo, Maendeleo fungamani ya binadamu na umoja!  (Vatican Media)

Papa: Caritas Internationalis: Upendo, Maendeleo na Umoja.

Papa Francisko katika mahubiri yake alikumbusha kwamba, kutangaza na kushuhudia Injili ni mpango mkakati wa maisha na utume wa Kikristo. Tarehe 27 Mei 2019, kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano wa ishirini na moja wa Caritas Internationalis kwa kukazia mambo makuu matatu: Upendo, maendeleo fungamani na umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, tarehe 23 Mei, limefungua mkutano wake wa ishirini na moja kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mkutano huu unahitimishwa rasmi tarehe 28 Mei 2019 na unawashiriklisha wajumbe 450 kutoka katika mataifa 164 na unaongozwa na kauli mbiu “Familia moja ya binadamu, nyumba moja kwa ajili ya wote”.  Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake alikumbusha kwamba, kutangaza na kushuhudia Injili ni mpango mkakati wa maisha na utume wa Kikristo.

Tarehe 27 Mei 2019, kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano wa ishirini na moja wa Caritas Internationalis kwa kukazia mambo makuu matatu: Upendo, maendeleo fungamani na umoja! Mkutano huu umekuwa ni fursa ya kukuza na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wajumbe wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kwa kutambua kwamba, Shirikisho hili linashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya huduma ya Injili ya upendo. Upendo unapata asili na chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mungu ni upendo. Kanisa linatekeleza dhamana hii kama chombo cha upendo kwa ajili ya binadamu na kazi nzima ya uumbaji, ambayo kimsingi ni nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu anasema, maendeleo fungamani ni mchakato wa utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo inayomgusa na kumwambata binadamu mzima, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee, ili kuwaonjesha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mama Kanisa. Katika muktadha huu, Kanisa linataka kujipambanua kuwa ni mdau mkuu wa maendeleo fungamani ya binadamu, dhana inayokwenda kinyume kabisa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ubaguzi mbaya kabisa dhidi ya maskini ni ukosefu wa huduma za maisha ya kiroho.

Hii inatokana na ukweli kwamba, maskini mara nyingi ni wepesi sana kukumbatia zawadi ya imani na wanayo kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Maskini waonjeshwe urafiki na Neno la Mungu; washirikishwe katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa sanjari na safari ya kukua na kukomaa katika imani. Upendeleo kwa maskini unapaswa kutafsiriwa hasa kama huduma ya kiroho iliyo bora zaidi na inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee! Baba Mtakatifu anasema, umoja ni kiini na tafsiri ya Kanisa linalopata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Neno lake, linaweza kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kujenga umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Umoja kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake ni kiini na chachu inayosindikiza na kuenzi huduma ya Injili ya upendo ndani na nje ya Kanisa. Huduma ya upendo inayotolewa na Kanisa inakuwa ni Sakramenti ya umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu anaipongeza Caritas Internationalis kwa kazi nzuri, utume unaomwilishwa katika maisha ya Kanisa. Mambo haya makuu yanapaswa kushuhudiwa katika ari na moyo wa ufukara, sadaka na unyenyekevu! Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na maskini, ili kushirikishana na wengine, hata kile kidogo walicho nacho! Injili ya upendo inapaswa kumwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Hii ni changanoto ya kuondokana na huduma ya upendo wa “kinafiki” inayopania kutuliza dhamiri zinazohangaika.

Ikumbukwe kwamba, upendo ni fadhila ya Kimungu unaowataka wahudumu wa Injili ya upendo kuwa watu wa kiasi, kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha ya Kanisa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa yaani uinjilishaji wa kina! Huduma ya upendo ni mchakato wa kukutana na Kristo katika huruma, upendo na mshikamano wa dhati, katika ari na mwamko wa ufukara! Mama Kanisa anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Waendelee kujenga na kudumisha umoja na kujisadaka kwa furaha kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Waendelee kuboresha maisha yao kwa Neno la Mungu, Mafundisho ya Kanisa na tunza ya kichungaji inayotolewa na Mama Kanisa!

Papa: Caritas
27 May 2019, 17:33