Vatican News
FAO imezindua mpango mkakati wa miaka kumi wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani: 2019-2018 kwa kuwekeza zaidi katika familia. FAO imezindua mpango mkakati wa miaka kumi wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani: 2019-2018 kwa kuwekeza zaidi katika familia.  (Vatican Media)

Papa Francisko apongeza mkakati wa kupambana na njaa duniani

FAO imezindua mpango mkakati wa miaka kumi wa kupambana na baa la njaa duniani kwa kuwekeza katika familia kuanzia mwaka 2019-2028. Lengo ni kufuta baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030 kama iliyokubaliwa na Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2030. Umoja wa Mataifa unasema, Lengo la Pili ni kumaliza njaa, kufikia usalama wa chakula na lishe bora na kueneza kilimo endelevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa umezindua mpango mkakati wa miaka kumi wa kupambana na baa la njaa duniani kwa kuwekeza katika familia, kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka 2028. Lengo ni kufuta baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030 kama iliyokubaliwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu Ifikapo mwaka 2030. Umoja wa Mataifa unasema, Lengo la Pili ni kumaliza njaa, kufikia usalama wa chakula na lishe bora na kueneza kilimo endelevu. Katika mchakato huu, familia zinapewa kipaumbele cha kwanza kama mahali ambapo kilimo kinaweza kuendelezwa na hivyo kuwa na matokeo chanya si tu kwa ajili ya sekta ya kilimo, bali kwa ajili yabinadamu wote pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

Katika mkutadha huu, familia inaweza kuwa ni nyenzo inayounganisha binadamu, kazi ya uumbaji na kilimo! Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliomwandikia Profesa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, akimpongeza kwa kuzindua mbinu mkakati huu. Baba Mtakatifu anasema, familia ni mfano hai wa utekelezaji wa kanuni auni inayoratibu mahusiano na mafungamano ya binadamu, ili kupata mwelekeo mpya katika maisha ya kijamii. Kwa njia hii, viongozi kutoka katika ngazi mbali mbali wanaweza kushirikiana na familia kuendeleza maeneo ya vijijini, kwa kuzingatia mafao ya wote sanjari na kutoa kipaumbele cha pekee kwa mambo msingi.

Hii ni Kanuni ya Auni inayosimamia uwakilishi kutoka katika ngazi ya chini kabisa, kwa kujali, heshima na wito wa wanawake, kipimo cha ubora wa jamii na utetezi thabiti wa haki ya wanawake kufanya kazi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wanawake katika Nchi Zinazoendelea Duniani ni wadau wakuu katika sekta ya kilimo. Wanachangia nguvu kazi katika katika mchakato mzima wa uzalishaji katika kilimo na ufugaji. Nchi Changa Duniani zinakabiliwa na hali mbaya ya maendeleo kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na athari za mfumo wa fedha kitaifa na kimataifa. Katika muktadha huu, kilimo kinakuwa ni chanzo cha ajira na maendeleo kwa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake.

Vijana wakiboreshewa mazingira, sekta ya kilimo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa fursa za ajira, kumbe, Malengo ya Maendeleo Endelevu Ifikapo mwaka 2030 hayana budi kutoa nafasi kwa vijana, ili kuchangia na hatimaye, kuleta mageuzi. Ili kuweza kufikia Malengo haya kuna haja kwa mfumo wa elimu kuboreshwa, ili kukidhi mahitaji ya maendeleo katika sekta ya kilimo na hivyo kuwasaidia vijana kuingia katika soko la ajira, ili kushirikisha karama na vipaji vyao. Elimu makini pamoja na sera bora za kilimo ni muhimu sana katika mchakato wa mabadiliko katika sekta ya kilimo, kwa kuzingatia ekolojia fungamani.

Umefika wakati kwa sekta ya elimu kuboresha mfumo mzima wa ufundishaji kwa kuwajengea vijana uwezo wa kuwa ni chachu ya mageuzi, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa ekolojia fungamani inayofumbatwa katika “namna ya kufikiri, sera, mpango wa elimu, mtindo wa maisha na maisha ya kiroho ambavyo kwa pamoja vinapinga uvamizi wa mfumo wa teknokrasia” (Laudato si,111). Urithishaji wa tunu hizi msingi zinazofumbatwa katika familia unaweza kubadilisha maisha ya Jumuiya mahalia na maisha ya jumuiya ya kimataifa katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni wakati muafaka wa kutafakari na kuhamasisha mchango wa familia katika kilimo, ili kundokana na baa la njaa duniani, sanjari na kukidhi mahitaji msingi ya binadamu. Hapa kuna haja ya kuwa na rasilimali watu watakaoweza kuibua mbinu mkakati wa kufyekelea mbali baa la njaa! Utekelezaji wa changamoto hii unahitaji ujasiri na utashi; kwa kuheshimu haki msingi za binadamu na mshikamano kama msingi wa maendeleo fungamani. Mambo haya yataisaidia Jumuiya ya Kimataifa kufikia Lengo la Pili la kumaliza njaa, kufikia usalama wa chakula na lishe bora pamoja na kueneza kilimo endelevu.

Papa: FAO
30 May 2019, 17:42