Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka watawa Barani Afrika kujibu kikamilifu changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kwa kusoma alama za nyakati na waaminifu kwa karama zao! Papa Francisko anawataka watawa Barani Afrika kujibu kikamilifu changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kwa kusoma alama za nyakati na waaminifu kwa karama zao!  (Vatican Media)

Papa: Watawa Barani Afrika: Jibuni changamoto za kichungaji!

baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa uinjilishaji daima unatekelezwa na Jumuiya inayoinjilisha, kwa kujihusisha kwa maneno na kwa matendo katika maisha ya kila siku; inafupisha umbali; inajishusha na kujinyenyekesha, ikiwa ni lazima, inakumbatia maisha ya mwanadamu, ikigusa mwili wa Kristo unaoteseka katika wengine! Ni wakati wa kusoma alama za nyakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Watawa wa Utume Barani Afrika “Société des Missions Africaines,” linaadhimisha mkutano wake mkuu, kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu anaye endelea kuwakirimia dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili Barani Afrika na hasa kati ya watu wanaoishi vijijini. Mwelekeo mpya kwa sasa ni huduma kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, kama njia muafaka ya kujibu changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanataka kuona mwanga angavu wa Injili, chimbuko la ari, mwamko na ujasiri wa kimisionari, unaowakirimia maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Hii ni dhamana nyeti, inayoweza hata kuhatarisha maisha ya wamisionari kama ilivyokuwa kwa Mtumishi wa Mungu Melchior de Marion Brèsilacc pamoja na Padre Augustin Planque. Hivi karibuni, Padre Pierluigi Maccalli wa Shirika hili alitekwa nyara na hadi wakati huu hajulikani mahali aliko! Haya ni matukio ambayo Vatican inayafuatilia kwa wasi wasi mkubwa!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 17 Mei 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Shirika la Watawa wa Utume Barani Afrika. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mchakato wa uinjilishaji daima unatekelezwa na Jumuiya inayoinjilisha, kwa kujihusisha kwa maneno na kwa matendo katika maisha ya kila siku; inafupisha umbali; inajishusha na kujinyenyekesha, ikiwa ni lazima, inakumbatia maisha ya mwanadamu, ikigusa mwili wa Kristo unaoteseka katika wengine!

Hii ni changamoto ya kuendelea kushirikiana na kushikamana na waamini wa dini na taasisi mbali mbali kwa ajili ya huduma kwa watoto maskini, waathirika wa vita, magonjwa na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Hii ni njia muafaka inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Kristo Yesu. Kwa kusukumwa na Roho Mtakatifu, watawa hawa wanaweza kuwa kweli ni wahudumu wa utamaduni wa majadiliano na watu kukutana, kwa ajili ya huduma kwa watoto wadogo na maskini, ili kusaidia ujenzi wa udugu wa kibinadamu!

Watawa hawa kama familia, wakiwa waaminifu kwa asili na utume wao, wanaitwa na kutumwa kumshuhudia Kristo kwa njia ya huduma ya upendo, wakiwashirikisha jirani zao miali ya maisha ya kidugu. Utume huu unaweza kupata mafanikio makubwa, ikiwa kama watazama zaidi katika tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na huduma kwa ndugu zao katika Kristo Yesu; mambo msingi yanayowawezesha kila mmoja wao kukutana mubashara na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, sababu ya kwanza ya kuinjilisha ni upendo wa Yesu walioupokea, uzoefu wa ukombozi unaowasukuma kumpenda zaidi. Wanahitaji kufufua tena roho ya kitaamuli inayoweza kuwasaidia kutambua upya kwamba, wameaminishwa hazina inayowafanya kuwa na utu zaidi na inayowasaidia kufuata maisha mapya.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa ushuhuda wanaoendelea kuutoa, anawataka wasonge mbele kwa ari na moyo mkuu, wakijitahidi kupyaisha njia ambayo Shirika lao limeipitia na hivyo kupata matunda mengi ya toba na wongofu kwa Kristo. Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, kwa wao kumsikiliza Roho Mtakatifu, kamwe wasiwe na wasi wasi ya kufuata njia mpya ya uinjilishaji. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya upya wa maisha anayewahamasisha kuanza upya na kubadili mahali, tayari kwenda hata sehemu zilizofahamika bado, yaani mwishoni mwa vipaumbele vya watu!

Papa: Uinjilishaji Afrika

 

17 May 2019, 16:28