Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika Wosia wake wa kitume "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" anazungumzia kuhusu miito mbali mbali ndani ya Kanisa na changamoto zake! Ushuhuda! Papa Francisko katika Wosia wake wa kitume "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" anazungumzia kuhusu miito mbali mbali ndani ya Kanisa na changamoto zake! Ushuhuda!  (ANSA)

Siku ya 56 ya Kuombea Miito: Mashemasi 19 Kupewa Daraja!

Kuhusu Miito, Baba Mtakatifu Francisko katika wosia wake anawaalika vijana kung’amua kwamba, Kristo Yesu anataka kujenga nao urafiki wa dhati. Wito ni mwaliko wa huduma ya kimisionari kwa Mungu na jirani, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kuna aina mbali mbali za miito ndani ya Kanisa.

Na Suzanna Kipapy, Songea & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani, anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 19 kutoka Jimbo kuu la Roma. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili 12 Mei 2019 majira ya saa 3:15 kwa Saa za Ulaya. Baba Mtakatifu katika Wosia wake wa Kitume, “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” uliotolewa hivi karibuni, anawakumbusha vijana kwamba, wao ni leo ya Mungu; na ujumbe makini kwa vijana ni kwamba, Mungu ni upendo na anawapenda vijana.

Kuhusu Miito, Baba Mtakatifu anawaalika vijana kung’amua kwamba, Kristo Yesu anataka kujenga nao urafiki wa dhati. Wito ni mwaliko wa huduma ya kimisionari kwa Mungu na jirani, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kuna aina mbali mbali za miito ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wito wa kwanza kabisa ni upendo unaomwilishwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; wito unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kinachosikitisha katika wito wa ndoa ni kuendelea kushuhudia wimbi kubwa la talaka na ndoa kuvunjika, hali inayosababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wasikubali kupwoka furaha na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana wanapaswa kujitaabisha kutafuta kazi, ili waweze kujiimarisha kiuchumi na hivyo kutelekeza dhamana na majukumu yao ya maisha ya ndoa na familia bila shida kubwa.Baba Mtakatifu anatambua changamoto na matatizo wanayokabiliana nayo vijana katika hija ya maisha yao katika ulimwengu mamboleo. Baadhi yao wanatengwa na kubaguliwa, wengine hawana hata chembe ya uzoefu kazini, kiasi kwamba, inawawia vigumu kuweza kupata fursa za ajira. Changamoto hii inapaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali. Vijana wasipende sana kuchagua aina ya kazi.

Baba Mtakatifu katika Wosia huu wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” anapenda kukazia kwa namna ya pekee, wito wa kipadre na maisha ya kuwekwa wakfu. Wito huu una changamoto na matatizo yake, lakini, inalipa kwa wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Bwana wa mavuno anaendelea kuita watenda kazi katika shamba lake. Hii ni changamoto kwa wakleri na watawa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mifano bora ya kuigwa katika maisha na utume wao. Licha ya mapungufu na udhaifu wao wa kibinadamu, kamwe Kristo Yesu hataacha kuwaita vijana watakaojisadaka kwa ajili maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo anaendelea kutembea katika viunga vya maisha ya waja wake, bila ya haraka! Anasimama kidogo, anaangalia na kuchagua bila ya haraka. Inasikitisha kuona kwamba, ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia una makelele kibao kutokana na uchafuzi wa mazingira, kiasi kwamba, wakati mwingine, inakuwa vigumu kuweza kusikiliza sauti ya Mungu inayomwita mtu kutoka katika undani wa maisha yake. Katika ulimwengu mamboleo kuna mengi yanayovutia kwa akili na macho! Kijana akithubutu kuyakumbatia na kuyaambata, anajikuta akiwa mtupu kutoka katika undani wake.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutafuta nafasi zenye ukimya, utakaowawezesha kupata nafasi ya ukimya, ili kutafakari, kusali na hatimaye, kufanya upembuzi yakinifu kwa kushirikiana na Kristo Yesu. Kwa njia hii, vijana wataweza kupata mang’amuzi ya wito wao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea, Tanzania alitoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Frederick Fidelis Patrick Mwabena, OSB wa Abasia ya Mtakatifu Benedikto, Peramiho, Jimbo kuu la Songea. Amemtaka Padre mpya kuhakikisha kwamba,  anatekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, kwa kujisadaka zaidi kwa njia ya nadhiri ya: Ufukara, Utii na Useja, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Mapadre watambue kwamba, katika maisha na utume wao, kamwe si wakamilifu.

Kumbe, wanapaswa kujibidisha kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha na utume wa Kipadre kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Waamini wanahimizwa pia kuwasindikiza mapadre wao kwa sala na sadaka zao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, malezi na majiundo ya kipadre kwanza kabisa ni kazi ya Mwenyezi Mungu ambayo inamtaka jandokasisi au Padre kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumfunda kadiri anavyotaka! Pili, Kasisi mwenyewe anapaswa kutambua kwamba, ni mhusika mkuu wa majiundo katika wito, maisha na utume wake wa kipadre. Tatu, wadau wakuu wa malezi ni walezi waliopewa dhamana hii kwa kusaidiana na Maaskofu huku wakitambua kwamba, wito unazaliwa, unakua na kukomaa ndani ya Kanisa ambaye ni Mama na mlezi wa miito yote mitakatifu!

Kanisa linawahitaji mapadre: wema, watakatifu na wachamungu; wanaoweza kutambua changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zilizoko katika maisha, tayari kuzifanyia kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu wanaowahudumia kwa moyo, akili na nguvu zao zote! Kwa upande wake, Askofu mkuu Damian Denis Dallu anasema, Seminarini ni mahali pa malezi na makuzi ya kipadre. Seminari ni mahali ambapo jandokasisi anapewa fursa ya kutathmini na kufanya mang’amuzi kuhusu wito wake wa kuwa padre au mtawa! Mkazo umewekwa katika majiundo ya maisha ya kiroho kwa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha; umuhimu wa maisha ya Kisakramenti; Mafundisho Tanzu ya Kanisa bila kusahau malezi  na majiundo ya kiakili, kiutu na kichungaji kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Wazazi washirikiane vyema na Kanisa, ili kuhakikisha kwamba, majandokasisi wanapata malezi makini, tayari: kutangaza, kuadhimisha na kuwahudumia watu wa Mungu bila ya kujibakiza. Walezi seminarini wanapaswa kujiridhisha kuhusu wito wa majandokasisi wanaowafunda, ili kweli Kanisa liweze kuwapata mapadre watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Waamini waendelee kujibidisha kuwakumbuka na kuwambea mapadre wao pamoja na kuhakikisha kwamba, wanalitegemeza Kanisa mahalia kwa hali na mali!

Jimbo kuu la Songea
10 May 2019, 15:17