Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Uchumi hauna budi kujikita katika kanuni maadili, ustawi na maendeleo ya wengi! Papa Francisko: Uchumi hauna budi kujikita katika kanuni maadili, ustawi na maendeleo ya wengi! 

Papa Francisko: Uchumi: Kanuni maadili, ustawi & mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, uchumi unapaswa kuhudumia ustawi na maendeleo ya wengi, ikiwa kama utakuwa unafumbatwa katika kanuni maadili, kipimo cha kweli kwa ajili ya ustawi wa binadamu. Mfuko wa Guido Carli, umejipambanua kwa kuwatambua na kuwatuza watu waliojitokeza kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ambao wamesimamia haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Guido Carli, ulioanzishwa miaka kumi iliyopita na Guido Carli, mchumi na kiongozi, huko Brescia, Kaskazini mwa Italia, umekuwa na uhusiano na urafiki wa pekee na familia ya Mtakatifu Paulo VI. Ni katika muktadha huu, Guido Carli akapiga hatua kubwa katika mchakato wa uwajibikaji wa jumla kama taasisi. Leo hii kuna nguvu mbili zinazokinzana: nguvu ya uchumi inayojielekeza katika ulaji na upande mwingine kunakosekana uwiano wa usambaji mzuri wa pato mintarafu mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Ikumbukwe kwamba, uchumi unapaswa kuhudumia ustawi na maendeleo ya wengi, ikiwa kama utakuwa unafumbatwa katika kanuni maadili, kipimo cha kweli kwa ajili ya ustawi wa binadamu. Mfuko wa Guido Carli, umejipambanua kwa kuwatambua na kuwatuza watu waliojitokeza kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ambao wamesimamia haki. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa Mfuko wa Guido Carli pamoja na Jopo la Majaji waliokuwa wamekusanyika ili kutoa tuzo kwa mshindi wa Tuzo ya Guido Carli kwa mwaka 2019.

Baba Mtakatifu anaupongeza Mfuko wa Guido Carli kwa kuendelea kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha mshikamano mintarafu mwanga wa Kikristo na kama sehemu ya utekelezaji wa upendo wa Kiinjili. Nchini Italia, kumekuwepo na idadi kubwa ya wananchi kutoka katika medani za kitamaduni, kisayansi, ulimwengu wa wafanyakazi, watu wa kujitolea na hata kutoka ndani ya Kanisa, ambao kutokana na shughuli zao mbali mbali, wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa na jamii. Baba Mtakatifu anawapongeza wajumbe, kwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wanyonge zaidi katika jamii, kama chachu ya ukuaji wa jamii katika ujumla wake!

Papa: Guido Carli

 

 

03 May 2019, 17:02