Papa Francisko: Sekta ya Madini: Izingatie: Ustawi na maendeleo ya binadamu wote; Uchimbaji uwe ni kwa ajili ya huduma ya binadamu; sekta ya madini iwe ni sehemu ya uchumi endelevu Papa Francisko: Sekta ya Madini: Izingatie: Ustawi na maendeleo ya binadamu wote; Uchimbaji uwe ni kwa ajili ya huduma ya binadamu; sekta ya madini iwe ni sehemu ya uchumi endelevu 

Papa Francisko: Sekta ya Madini: Ustawi, huduma, uchumi endelevu

Baba Mtakatifu Francisko anasema: Sekta ya madini haina budi kujielekeza zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo binadamu wote. Pili uchimbaji wa madini uwe ni kwa ajili ya huduma ya binadamu na wala si vinginevyo. Tatu, sekta ya madini iwe ni sehemu ya uchumi endelevu! Sekta ya madini haina budi kujielekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anakazia umuhimu wa majadiliano kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, kwa kuzingatia: uaminifu, ujasiri na udugu! Ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa usiegemee sana katika mchakato wa kupata faida kubwa, hali ambayo inahatarisha utu, heshima ya binadamu pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Kumbe, kuna haja ya kuwa na sera na mikakati ya maendeleo inayokita mizizi yake katika maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya wa shughuli za kiuchumi hata katika sekta ya madini! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 3 Mei 2019 kwa washiriki wa mkutano kuhusu sekta ya madini na mafao ya wengi!

Katika hotuba yake, amekazia mambo makuu matatu: Sekta ya madini haina budi kujielekeza zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo binadamu wote. Pili uchimbaji wa madini uwe ni kwa ajili ya huduma ya binadamu na wala si vinginevyo. Tatu, sekta ya madini iwe ni sehemu ya uchumi endelevu! Sekta ya madini haina budi kujielekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote. Hii ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Huu ni uchumi shirikishi unaozingatia mafao ya jumuiya mahalia, ili kuweza kuangalia mustakabali wake na watoto wao kwa siku za usoni, badala ya kuangalia malengo ya uchumi mpito! Watu mahalia wanapaswa kuwa ni wadau wakuu pale kunapokuwepo na utekelezaji wa miradi mkubwa ya uchimbaji madini, kwa kutambua kwamba, ardhi si bidhaa bali ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe ni kito cha thamani, kinachopaswa kudumishwa.

Watu mahalia wasinyanyaswe na kufukuzwa kutoka katika maeneo yao, ili kupisha kazi ya uchimbaji madini ambayo wakati mwingine inakuwa ni chanzo cha uharibifu wa mazingira na tamaduni za watu! Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kuheshimiwa na kuzingatiwa na wote! Pili, uchimbaji wa madini kama shughuli ya kiuchumi inapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu; kwa kuheshimu utu na haki zake msingi. Usalama wa wachimba madini na haki zao msingi vilindwe. Maendeleo fungamani ya binadamu, yawafikie watu wote. Tatu, Sekta ya madini inapaswa kujikita katika mchakato wa uchumi endelevu, kwa kuchakata rasilimali madini ili iwe mtaji, utakaosaidia kuzalisha bidhaa sokoni na huduma kwa jamii sanjari na kuendelea kutunza mazingira. Kuna haja kwa viwanda kuhakikisha kwamba, vinakuwa na utunzaji bora wa taka zinazoweza kutumiwa tena katika uzalishaji pamoja na kusaidia kuratibu ulaji.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni sehemu ya kanuni maadili pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu amepongeza juhudi za majadiliano ya kiekumene zinazofanywa kwa kuwaunganisha waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kushirikiana na viongozi wa sekta ya madini ili kulinda mazingira. Binadamu anapaswa kutambua kwamba, ni chombo cha Mungu katika kutunza mazingira, kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli na vipaji vyake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mkutano huu, utakuwa ni fursa ya kufanya mang’amuzi na hatimaye, kuwa na sera na mikakati inayotekelezeka katika maeneo husika.

Mapendekezo haya yasaidie pia kuleta mabadiliko katika maisha, sera na mikakati ya sekta ya madini itakayozingatiwa na wadau mbali mbali. Lengo ni kufikia ustawi na mafao ya wengi sanjari na maendeleo ya kweli na fungamani ya binadamu. Sekta ya madini inapaswa kuangaliwa kwa karibu sana kwani inagusa mustakabali wa binadamu kwa siku za usoni. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanarithi mazingira bora zaidi. Hili ni suala linalowaathiri watu wote kwa kuwa lina uhusiano na maana halisi ya safari ya maisha yao hapa duniani.

Papa: Sekta ya Madini
03 May 2019, 17:16