Tafuta

Papa Francisko akiwa njiani kuelekea Bucarest nchini Romania amepata nafasi ya kusalimiana na waandishi wa habari pamoja na kutuma salam na matashi mema kwa viongozi mbali mbali. Papa Francisko akiwa njiani kuelekea Bucarest nchini Romania amepata nafasi ya kusalimiana na waandishi wa habari pamoja na kutuma salam na matashi mema kwa viongozi mbali mbali. 

Hija ya Kitume Romania: Salam na matashi mema kwa viongozi!

Baba Mtakatifu Francisko amepata nafasi ya kusalimiana na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake nchini Romania! Amewatakia heri na baraka katika utume wao. Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea Bucarest nchini Romania, amewatumia ujumbe wa matashi mema, heri na baraka wakuu wa nchi ya: Italia, Croatia, Bosnia Herzegovina, Montenegro, Serbia na Bulgaria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2019 anafanya hija ya 30 ya kitume kimataifa, nchini Romania inayoongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu anatembelea Romania kama hujaji na ndugu yao katika Kristo ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano unaokita mizizi yake katika amana na utajiri wa imani nchini Romania!

Baba Mtakatifu, Alhamisi, tarehe 30 Mei 2019 kama sehemu ya maandalizi ya hija hii ya kitume, alikwenda kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma. Hii ni sehemu ya mapokeo ya Baba Mtakatifu kabla na baada ya hija zake za kitume, kujikabidhi kwa Bikira Maria, tangu tarehe 14 Machi 2013, siku moja tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki! Ijumaa, tarehe 31 Mei 2019, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusalimiana na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake nchini Romania! Amewatakia heri na baraka katika utume wao, utakaomwezesha kukutana na wananchi wa Romania, kuona na kushuhudia utajiri wa tamaduni na mapokeo yao mbali mbali.

Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea Bucarest nchini Romania, amewatumia ujumbe wa matashi mema wakuu wa nchi ya: Italia, Croatia, Bosnia Herzegovina, Montenegro, Serbia na Bulgaria. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amewatakia viongozi hawa:furaha, amani, ustawi, maendeleo, utulivu, ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu na hatimaye, kuwapatia baraka zake za kitume! Hija hii ya kitume imepewa uzito wa pekee sana na Serikali ya Romania. Matukio muhimu yanarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa pamoja na vituo vya Radio.

Serikali imetenga waandishi wa habari maalum 1, 000 ili kuhakikisha kwamba, watu kutoka ndani na nje ya Romania wanapata kwa usahihi yale yanayoendelea kujiri. Baadhi ya shule zimefungwa ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao. Maaskofu nchini Romania wanawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutembea kwa pamoja chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini!

Papa Salam Viongozi
31 May 2019, 17:14