Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Baba Yetu Uliye Mbinguni: Awe ni chanzo cha hija ya pamoja katika maisha, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati! Papa Francisko: Baba Yetu Uliye Mbinguni: Awe ni chanzo cha hija ya pamoja katika maisha, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati!  (AFP or licensors)

Hija ya Kitume Romania: Baba Yetu: Chanzo cha umoja & Upendo

Sala ya Baba Yetu ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sala ya waamini wanaotembea kwa pamoja katika safari ya udugu. Romania iwe ni maskani ya wote, mahali panapowakutanisha watu na bustani ambamo upatanisho na umoja vinaimarishwa na kustawishwa. Waamini wote wanaunganishwa chini ya Baba yao aliye mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Romania, Ijumaa, tarehe 31 Mei 2019 amepata nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Kanisa la Kiorthodox, Wokovu wa watu, lililozinduliwa kunako mwaka 2018 na Patriaki Daniel wa Kanisa la Kiorthodox la Romania, akishirikiana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Ujenzi wa Kanisa hili inatarajiwa kukamilika mwaka 2024 na asimilia 70% ya gharama zote ni mchango wa Serikali ya Romania.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutafakari kuhusu Sala ya Baba Yetu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sala ya waamini wanaotembea kwa pamoja katika safari ya udugu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Romania inakuwa ni maskani ya wote, mahali panapowakutanisha watu na bustani ambamo upatanisho na umoja vinaimarishwa na kustawishwa. Waamini wote wanaunganishwa chini ya Baba mmoja, ndiyo maana wanathubutu kumwita Mwenyezi Mungu, Baba Yetu; changamoto na mwaliko wa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini; kuwakaribisha na kuwapokea kama ndugu ili kuendelea kusaidiana.

Baba Yetu Uliye mbinguni! Mbingu zinafumbata yote kwani ni mahali ambapo jua linawangazia wema na wabaya na kuwanyeeshea mvua wenye haki na wasio na haki. Ni mahali pa kuombea amani na utulivu, kwa njia ya ndugu zao katika imani, wanaoishi huko mbinguni, baada ya kuamini, kupenda na kuteseka sana kwa sababu tu ni Wakristo; hali inayoendelea hata leo hii sehemu mbali mbali za dunia. Pamoja na watakatifu hawa, waamini wanamwomba Mungu ili jina lake litukuzwe na kuwa ni chemchemi ya upendo, kwa kumsifu, kumwabudu na kumtukuza kwa njia ya ndugu zao, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu mambo yanayodumu, yaani uwepo wake endelevu pamoja na ule wa ndugu zao. Waamini wanamwomba Mwenyezi Mungu ili ufalme wake ufike ili kuondokana na uchu wa fedha, mali na madaraka; kwa kutafuta mafao binafsi; kuzamishwa katika malimwengu na ulaji wa kupindukia. Ni sala inayomwomba Mungu kuwasaidia ili waweze kuondokana na tabia ya kujiaminisha sana katika nguvu na usalama wao binafsi; pamoja na kutafuta mambo ya nje; ambayo kimsingi inawapofusha kiasi cha kushindwa kuona ufalme wa Mungu. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni na kwamba, ni utashi wa Mungu watu wote waweze kuokoka.

Waamini watambue udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, ili kuwa tayari kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, chemchemi ya ujasiri na furaha, awawezeshe kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, nje ya mipaka ya jumuiya zao, lugha wanazotumia, tamaduni na mataifa yao. Utupe leo mkate wetu wa kila siku, ili kusikia uwepo endelevu wa Mungu. Huu ni mkate unaomegwa kwa ajili ya huduma kwa jirani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mkate wa kumbu kumbu unaorutubisha mizizi na utambulisho wa Kikristo, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuthamini asili na utambulisho wao. Ni mkate unaoboresha uvumilivu ili kujenga na kudumisha umoja, wema na mshikamano unaowawezesha wakristo wote kufanya kazi kwa pamoja kwa kuthamini na tofauti zao msingi, kama amana na utajiri unaowawezesha kupata furaha ya kidugu na upatanisho katika tofauti zao. Hata leo hii, kuna mamilioni ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa na utupu duniani. Kuna watu wenye njaa na kiu ya upendo dhidi ya ubinafsi na hali ya kutowajali wengine, inayotoa kashfa mbele ya Mungu!

Waamini wawe wepesi kujisadaka kwa ajili ya jirani zao; kwa kujimega na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Usituache kishawishini na utuopoe maovuni, ni mwaliko na changamoto ya kujifunza kusamehe wengine kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, kama wao wanavyosamehewa na Mwenyezi Mungu. Wawe na ujasiri wa kuwa wazi pasi na woga; wawe na nguvu ya kusamehe na kusonga mbele; ujasiri wa kuendelea kutafuta ili kukutana na jirani zao katika ukweli na haki na kwamba, Shetani, Ibilisi anataka kuwafungia katika ubinafsi wao; kwa kuwatumbukiza katika kishawishi, ili kuwageuzia ndugu zao mgongo! Mwenyezi Mungu awe ni chanzo cha hija ya pamoja katika maisha, ili kwa pamoja waweze kuwa na ujasiri wa kusema, Baba Yetu!

Papa: Baba Yetu

 

31 May 2019, 18:23