Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika hotuba kwa viongozi wa serikali, vyama vya kiraia na viongozi amekazia umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Francisko katika hotuba kwa viongozi wa serikali, vyama vya kiraia na viongozi amekazia umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  (AFP or licensors)

Hija ya Kitume Romania: Hotuba: Viongozi wa Serikali & Mabalozi!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia zaidi umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru, umoja na mshikamano; changamoto ya wakimbizi, wahamiaji; dhamana na wajibu wa wanasiasa; ujenzi wa jamii shirikishi pamoja na utume wa Makanisa nchini Romania. Miaka thelathini ya utawala dhalimu wa kikomunisti ulisigina:: uhuru wa kuabudu, haki msingi za binadamu, utu na heshima yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, vyama vya kisiasa na kiraia, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao pamoja na viongozi mbali mbali wa kidini, wakati wa hija yake ya kitume, Bucarest nchini Romania, Ijumaa tarehe 31 Mei 2019 amesema, yuko kati yao kwa ajili ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani na ushuhuda wa Kikristo! Hija hii ni kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Romania na mara ya kwanza tangu Romania inashika hatamu za uongozi wa Baraza la Ulaya!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia zaidi umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru, umoja na mshikamano; changamoto ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum; dhamana na wajibu wa wanasiasa; ujenzi wa jamii shirikishi pamoja na dhamana na wajibu wa Makanisa nchini Romania. Miaka thelathini imegota tangu Romania ilipojikwamua kutoka katika makucha ya utawala dhalimu, uliosigina: uhuru wa kuabudu na haki msingi za binadamu. Leo hii, Romania iko mstari wa mbele katika ujenzi wa demokrasia inayounganisha nguvu ya kisiasa na kijamii; kwa kukuza na kudumisha majadiliano, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini.

Romania katika kipindi cha miaka ya hivi karibu anasema Baba Mtakatifu imepata mafanikio makubwa yanayopaswa kuendelezwa, ili kuzima kiu na matamanio halali ya wananchi wa Romania pamoja na kuendeleza mapaji ya watu wake. Jitihada hizi zisaidie kukuza na kudumisha amani na utulivu; kwa kuonesha mshikamano na wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum; hali inayohatarisha ubora wa maisha ya wananchi pamoja na kudhohofisha mizizi ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, ambazo zimesimamiwa kidete na wananchi wa Romania.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ili kukabiliana na changamoto mamboleo kuna haja ya kushirikiana na kushikamana kwa kuunganisha nguvu ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidini, ili kuweza kutembea kwa pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ndiyo njia muafaka ya ujenzi wa historia mpya inayojikita katika sadaka ili kujenga amani na utulivu, ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa. Romania inapaswa kujielekeza katika ujenzi wa jamii shirikishi kwa kutoa fursa kwa kila mwananchi kutumia vyema karama na mapaji yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani ni kwa njia ya kazi inayofanywa kwa uhuru, kwa ubunifu, kwa kushirikiana na kwa kusaidiana na wengine, ndivyo mwanadamu hudhihirisha na kuendeleza heshima na utu wao.

Hii ni Jamii ambamo maskini wanaheshimiwa na kuthaminiwa kama ndugu, kwa kushirikishwa katika ujenzi wa nchi yao, kielelezo makini cha jamii inayoendelea, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maendeleo ya kweli yanafumbatwa katika mshikamano na upendo unaounganisha nguvu, sera na mikakati kwa ajili ya mafao ya wengi kwa kutumia vyema rasilimali iliyopo! Baba Mtakatifu anasema, ni katika muktadha huu, Makanisa nchini Romania yana jukumu la kusaidia kuibua sera na mikakati itakayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi, kama ushuhuda wa imani tendaji.

Kanisa Katoliki linapenda kuchangia katika mchakato wa kukuza na kudumisha amani, umoja na matumaini, kwa ajili ya huduma kwa binadamu na maendeleo ya wengi. Kanisa linataka kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa la Romania hususana katika malezi, makuzi na majiundo makini katika elimu pamoja na huduma mbali mbali zinazogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Papa: Viongozi
31 May 2019, 17:31