Papa Francisko wakati wa hija yake ya kitume Romania amepata nafasi ya kuzungumza na Patriaki Daniel pamoja na wajumbe wa kudumu wa Sinodi ya Kanisa la Kiorthodox Romania. Papa Francisko wakati wa hija yake ya kitume Romania amepata nafasi ya kuzungumza na Patriaki Daniel pamoja na wajumbe wa kudumu wa Sinodi ya Kanisa la Kiorthodox Romania. 

Hija ya Kitume Romania: Ushuhuda: Damu, Neno, Huduma & Sala

Baba Mtakatifu Francisko asema: Yuko kati yao kwa ajili ya kutafakari, Sura ya Kristo Mteseka, ili kupyaisha matumaini ya watu wa Mungu. Ushuhuda na kifungo cha imani uliwasukuma Mitume Petro na Andrea, ndugu wa damu kutangaza na kushuhudia Injili nchini Romania, kwa kusadaka maisha yao, kiasi cha kuanzisha uekumene wa damu unaorutubisha majadiliano ya kiekumene.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake nchini Romania, Ijumaa, tarehe 31 Mei 2019 amekutana na kuzungumza na Patriaki Daniel pamoja na wajumbe wa kudumu wa Sinodi ya Kanisa la Kiorthodox la Romania. Katika hotuba yake, amegusia kuhusu: Uekumene wa damu; amana na utajiri wa maisha ya kiroho; umoja na mshikamano wa Kanisa. Wakristo wanapaswa kutembea pamoja kwa nguvu ya kumbu kumbu, kwa kusikiliza Neno la Mungu; kwa kuumega mkate. Wakristo watembee pamoja, kuelekea Pentekoste mpya.

Baba Mtakatifu amewaambia wajumbe wa kudumu wa Sinodi ya Kanisa la Kiothodox kwamba, yuko kati yao kwa ajili ya kutafakari, Sura ya Kristo Mteseka, ili kupyaisha matumaini ya watu wa Mungu. Ushuhuda na kifungo cha imani uliwasukuma Mitume Petro na Andrea, ndugu wa damu kutangaza na kushuhudia Injili nchini Romania kadiri ya Mapokeo. Hawa ni Mitume ambao walisadaka maisha yao, kiasi cha kuanzisha uekumene wa damu unaoendelea kurutubisha majadiliano ya kiekumene. Hata leo hii bado kuna Wakristo wanaoendelea kuteseka katika Ijumaa ya Madhulumu, wakionesha kimya kikuu cha Jumamosi kuu na hatimaye, kuzaliwa upya Jumapili ya Ufufuko wa Bwana!

Hawa ndio wafia dini na waungama imani, mfano bora wa kuigwa kwa vijana wa kizazi kipya. Mashuhuda na wafiadini hawa ni amana na utajiri wa pamoja. Mashuhuda hawa wa imani wamezamishwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu na hatimaye, kuungana naye tena baada ya ufufuko, ili na wao waenende katika upya wa uzima. Papa Francisko anakaza kusema, miaka ishirini iliyopita, Mtakatifu Yohane Paulo II aliweza kukutana na kuzungumza na Patriaki Teoctist wa Kanisa la Kiorthodox la Romania, akatoa wito wa Makanisa kuungana, huu ni wito wa matumaini uliozindua nyakati mpya na sasa ni wakati wa kutembea kwa pamoja ili kugundua na kupya udugu na mambo msingi yanayo waunganisha!

Baba Mtakatifu anayataka Makanisa kutembea kwa pamoja kwa nguvu ya kumbu kumbu inayojikita katika mizizi katika historia ya uinjilishaji kwenye karne ya kwanza. Ni katika mazingira haya, wakristo wakawa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia roho ya kinabii, wakajibidisha katika mchakato wa utamadunisho. Hiki ni kipindi ambacho Kanisa lilibahatika kuwa na mashuhuda wa imani na waungama dini; utakatifu wa maisha, ukawa ni chachu inayomwilishwa katika medani mbali mbali, kiasi cha kuutolea ushuhuda na kuvumilia nyanyaso na madhulumu! Hata leo hii, Wakristo wanahamasishwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, ili kwa njia ya neema, waweze tena kugundua ndani mwao kumbu kumbu ya umoja, ili kuyaangazia mapito yao.

Wakristo wanaitwa na kuhamasishwa kutembea kwa pamoja huku wakisikiliza Neno la Mungu kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau. Hii ni changamoto kwa Wakristo kwa pamoja kumsikiliza Kristo Yesu, hasa nyakati hizi ambazo zinashuhudia mabadiliko makubwa ya kijamii na kitamaduni; maendeleo ya sayansi, teknolojia, ustawi, maendeleo na ukuaji wa kiuchumi. Utandawazi umedhohofisha kanuni maadili na utu wema; imeng’oa tunu msingi za maisha ya watu; umesababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira na zaidi yao, umewafunga watu katika choyo, chuki na ubinafsi. Umefika wakati wa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwanusuru watu kutoka katika utamaduni wa chuki na uhasama, ubaguzi, kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Huu ni utandawazi unaowakatisha vijana tamaa ya maisha bora zaidi. Wote hawa wanahitaji kukutana na Kristo Mfufuka, chemchemi ya matumaini mapya kwa kusikiliza, kulitangaza na kulishuhudia Neno lake. Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha wakristo kutembea pamoja katika uekumene wa sala na kuumega mkate kwa pamoja, changamoto inayohitaji waamini kuheshimiana, kuthaminiana na kushirikiana katika Injili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuwapokea na kuwaonjesha mshikamano.

Wakristo wanapaswa kutembea kwa pamoja, kuelekea kwenye Pentekoste mpya, kama ilivyokuwa kwenye ile Pentekoste ya kwanza, wakiwa wameungana na Bikira Maria, Mama wa Kanisa, wakashukiwa na Roho Mtakatifu na kutambua utajiri wa lugha, kiasi cha kumshuhudia Kristo Mfufuka. Roho Mtakatifu ndiye anayeliwezesha Kanisa kujenga umoja katika utofauti, kwa kukazia mambo msingi yanayowaunganisha. Roho Mtakatifu ni chombo cha ujenzi wa udugu na anayewapatia neema ya kuweza kutembea kwa pamoja katika upya wa maisha! Anawawezesha kuwa na ujasiri wa kushirikishana na kushikamana katika maisha na utume wa Kanisa. Roho Mtakatifu ni nguvu ya mashuhuda na waungama imani.

Papa: Sinodi Romania
31 May 2019, 18:04