Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Taifa Mexico: Mauaji ya Wanawake; Wakimbizi na Wahamiaji; Siasa na Uchumi; Mageuzi Vatican & Kashfa ya Nyanyaso za Kijinsia Papa Francisko: Mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Taifa Mexico: Mauaji ya Wanawake; Wakimbizi na Wahamiaji; Siasa na Uchumi; Mageuzi Vatican & Kashfa ya Nyanyaso za Kijinsia 

Papa Francisko: Mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Mexico!

Papa Francisko amegusia kuhusu: mauaji ya wanawake; ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji; uhusiano kati ya siasa na uchumi; mageuzi Vatican. Madhara ya biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Hii ni tafakari ya kina kuhusu hali halisi ya kimataifa, maisha na utume wa Kanisa kadiri anavyoufahamu Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Valentina Alazraky wa Kituo cha Televisheni cha Taifa nchini Mexico amegusia kuhusu: mauaji ya wanawake ndani ya familia, ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji; uhusiano kati ya siasa na uchumi; mageuzi yanayoendelea kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu pia amepembua kuhusu madhara ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Hii ni tafakari ya kina kuhusu hali halisi ya kimataifa sanjari na maisha na utume wa Kanisa kadiri anavyoufahamu Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa sasa, Papa Francisko anasema, hana mpango wa kwenda Mexico kwani anapania kutembelea nchi ambazo bado hajapata fursa ya kuzitembelea. Sera na mikakati ya ujenzi wa kuta zinazowatenganisha watu, kama ulivyokuwa ukuta wa Berlin, kwa kisingizio cha usalama wa taifa ni kinyume kabisa cha ujenzi wa utamaduni wa madaraja ya kuwakutanisha watu kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ulinzi na usalama wa taifa unafumbatwa katika majadiliano yanayokita mizizi yake katika ukweli na uwazi; ukuaji wa uchumi fungamani; elimu bora na makini pamoja na watu kushirikishwa kwenye maamuzi mazito yanayohusu nchi yao. Watu wana haki ya kuhakikishiwa ulinzi na usalama wa maisha yao; kwa kuzingatia uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu. Watoto kutenganishwa na wazazi pamoja na walezi wao, ni jambo linalopingana na haki msingi za watoto pamoja na sheria asilia.

Sera za ulinzi na usalama zinazovunja haki msingi za binadamu ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia ni matokeo ya athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; athari za mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote; uchoyo na ubinafsi, unaofanywa na kikundi cha watu wachache duniani, kuhodhi sehemu kubwa ya utajiri na rasilimali za dunia ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna umaskini mkubwa wa hali na kipato, unaowalazimisha watu kuzikimbia nchi zao ili kutafuta maisha bora zaidi.

Kwa bahati mbaya, anasema Baba Mtakatifu Francisko, uchumi wa dunia unadhibitiwa na mifumo ya fedha kitaifa na kimataifa na matokeo yake, wananchi waliowekeza fedha na akiba zao, wanajikuta wakiogelea kwenye maji marefu baada ya Benki hizi kufilisika. Mfumo wa fedha kitaifa na kimataifa umekuwa ni chanzo mojawapo kinachosababisha ukosefu wa haki jamii. Hapa kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, uchumi wa dunia unakita mizizi yake katika maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kukidhi mahitaji msingi, utu na heshima ya binadamu. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano kati ya uchumi, utu wa binadamu na maisha ya kiroho. Umaskini ni janga la kimataifa linalopaswa kuvaliwa njuga na wadau wote kwani umaskini unadhalilisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Takwimu zinaonesha wamba, nchini Mexico katika kipindi cha mwaka 2018 zaidi ya watu 40, 000 waliuwawa kikatili na kwamba, kila kukicha idadi ya watu wanaopoteza maisha, pamoja na watu wanaopotea katika mazingira ya kutatanisha inazidi kuongezeka. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, haya ni matokeo ya siasa za chuki na tabia ya kulipizana kisasi. Wanasiasa wanasahau kwamba, siasa ni huduma ya upendo jamii inayopaswa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa wanasiasa wanaojitafuta wenyewe kwa masilahi binafsi ni hatari sana kwa jamii na matokeo yake ni ghasia, mipasuko na kinzani zisizokuwa na tija hata kidogo!

Wanasiasa wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Wanasiasa wawe ni vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu wao na kamwe wasiwe ni chanzo cha kinzani, mipasuko na vita. Kanisa litaendelea kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani, maridhiano, umoja na udugu wa kibinadamu! Baba Mtakatifu anasema, Shetani, Ibilisi si dhana ya kufikirika, yupo na anaendelea na kazi ya kuwasambaratisha walimwengu. Kuna madhulumu makubwa na nyanyaso dhidi ya Wakristo nchini Mexico, kazi inayofanywa na Ibilisi. Mexico ni daraja kati ya Amerika ya Kusini na Amerika ya Kaskazini. Kumbe, kuna haja ya kukesha na kuangalia ili kamwe watu wasimezwe na malimwengu. Vijana wa kizazi kipya wana matumaini, matatizo na changamoto mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuendeleza majadiliano na wazee ili waweze kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kijamii na kitamaduni, ili vijana hawa waweze kuzamisha mizizi yao katika uhalisia wa maisha. Mchakato huu unawezekana kwa njia ya majadiliano yanayomwilishwa katika utashi wa kutaka kukutana na wengine. Ikumbukwe kwamba, wazee wana ndoto na vijana wana utabiri; mambo msingi katika malezi, makuzi na ukomavu wa vijana wa kizazi kipya! Baba Mtakatifu anasikitika kuona kwamba, bado mfumo dume unaendelea kutawala na kuwanyanyasa wanawake kana kwamba, wao ni watu wa daraja la pili duniani! Kuna wanawake wengi ambao wanatumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Haya ni mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki zao msingi. Wanawake wanayo dhamana na utume katika jamii na Kanisa katika ujumla wake. Wana utajiri na karama nyingi zinazopaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Chuki, uhasama na mauaji ya wanawake ni mambo ambayo yamepitwa na wakati. Wanawake wana karama ya kuvumilia mateso kwa ajili ya ustawi wa watoto wao pamoja na kuendeleza Injili ya uhai. Baba Mtakatifu anasema kuna mifano ya wanawake wengi ambao wanaendelea kujisadaka kama vyombo na mashuhuda wa upendo kwa watoto na waume zao hata kama wako gerezani.

Katika maisha na utume wake anapenda sana kuheshimu kazi na dhamana inayotekelezwa na wadau katika tasnia ya mawasiliano. Jambo la msingi ni kwa wadau wa mawasiliano kuwa na uvumilivu kidogo kwake, kwani anawapenda na kuwathamini kutoka katika undani wa moyo wake. Waandishi wa habari kwa maswali yao dodoso wamemwezesha kufikiri na hatimaye, kutafuta ukweli wa mambo kama ilivyotokea kwenye kashfa ya nyanyaso za kijinsia zilizolikumba Kanisa nchini Chile! Alipata muda wa kusali, kutafakari na kuomba ushauri na kashfa hii ikashughulikiwa kikamilifu na kwa sasa Sekretarieti kuu ya Vatican iko makini zaidi. Baraza la Makardinali Washauri linaendelea kumsaidia vizuri katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kuhusu shutuma za kashfa mbali mbali zinazoendelea kujitokeza ndani ya Kanisa, Baba Mtakatifu anasema, wanazifanyia kazi na kwamba, si kila kitu lazima kitolewe hadharani! Jambo la msingi ni watu kuwa na uvumilivu, ili kutoa nafasi kwa viongozi wa Kanisa kufanya uchunguzi wa kina na matokeo kutolewa kwa wakati! Pale viongozi wa Kanisa wanapopatikana na hatia, hatua za kisheria na kinidhamu zinachuliwa mara moja! Wakati mwingine, Kanisa linalazimika kukaa kimya kama alivyofanya Yesu na hapo ni mwanzo wa watu kuchunguza dhamiri zao ili hatimaye, kuibuka na majibu muafaka! Mkutano wa Kanisa kuhusu ulinzi wa watoto wadogo umekuwa na mafanikio makubwa na wengi wameridhishwa na jinsi mambo yalivyoendeshwa.

Wajumbe walitoa mapendekezo ambayo tayari yamefanyiwa kazi. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika Barua binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia;  anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Kanisa litaendelea kuwa ni Mama na Mwalimu kwa kukazia toba na wongofu wa ndani, ili watoto wake waweze kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya maskini na Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kanisa litaendelea kuhamasisha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia kwa kutambua kwamba, leo hii Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi lisiliokuwa na alama. Mambo makuu manne yanayozingatiwa na Kanisa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Wakimbizi na wahamiaji wakiheshimiwa na kuthaminiwa wanaweza pia kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi wahisani anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa litaendelea kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, kifo laini au “Eutanasia”.

Uhusiano wake na viongozi mbali mbali wa Serikali ni  kutaka kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kukazia mema na mazuri kutoka kwa watu ili waweze kuyakuza na kuyaendeleza. Wambeya hawana bunge! Kanisa litaendelea kuonesha upendo kwa watoto wake wote, yaani watakatifu na wadhambi, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanahitaji toba na wongofu wa ndani, ili kuambata utakatifu wa maisha. Watu wenye mielekeo ya ndoa za jinsia moja wana haki zao msingi zinazopaswa kuheshimiwa na kuzingatiwa, bila kubaguliwa hata kidogo.

Kwa ufafanuzi huu, Baba Mtakatifu anakaza kusema si kwamba, Kanisa linahalalisha matendo yao ambayo ni kinyume cha mpango wa Mungu. Mafundisho msingi ya Mama Kanisa kuhusu ndoa na familia ni kama yanavyofafanuliwa kwenye Katekesimu ya Kanisa Katoliki ma Wosia wa Kitume: Furaha ya Upendo ndani ya familia ”Amoris Laetitia” ni habari njema kwa familia ya Mungu. Katika maisha na utume wake, ataendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Mafundisho ya Kanisa bila kupepesapepesa macho! Hakuna ndoa ya watu wa jinsia moja!

Watu wanaweza kutofautiana kwa mawazo na mitazamo ya maisha, huu ni utajiri na amana ya Kanisa na kamwe hauwezi kuwa ni sababu ya kujenga chuki na uhasama. Kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa utakatifu wa maisha. Kukosoana kwa heshima na upendo, kunasaidia kulijenga Kanisa. Furaha yake kubwa ni kukaa pamoja na kati ya watu wa Mungu. Anapowatembelea wafungwa na wagonjwa anapata amani na utulivu wa ndani. Pale anapogundua kwamba, anakwenda mrama, anajisahihisha na kujirekebisha, akiomba neema na huruma ya Mungu kama ilivyokuwa kwenye kesi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia nchini Chile.

Baba Mtakatifu Francisko anatambua kwamba, si mkamilifu, ndiyo maana kila baada ya siku kumi na tano, anakimbilia kwenye mahakama ya huruma ya Mungu ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zake kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio! Kwa wale wanaomtuhumu kwa mambo yasiyokuwa na ukweli, anawaombea. Papa Francisko anasema, ataendelea kutekeleza maagizo ya Baraza la Makardinali kuhusu mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican. Kanisa linakabiliana na changamoto nyingi, lakini linaendelea kukua na kukomaa katika maisha na utume wake. Kuna wakleri, watawa na waamini walei wanaoendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikulu Ndogo ya Castel Gandolf kwa sasa itaendelea kuwa ni Jumba la Makumbusho. Papa ataweza kuamua mahali pa kufanyia mapumziko yake!

Baba Mtakatifu anasema, majadiliano ya kidini na kiekumene ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, ili kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu! Huu ni utekelezaji wa maazimio ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kuna changamoto kubwa ya misiamo mikali ya kidini na kiimani pamoja na mashambulizi ya kigaidi, lakini zote hizi ni changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi kwa njia ya upendo na mshikamano wa kidugu! Baba Mtakatifu anasema, anaipenda sana familia ya Mungu nchini China ni hamu ya moyo wake, iko siku atakwenda kutembelea China. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na uhusiano mzuri kati ya Vatican na China.

Wakatoliki waliokuwa wanaishi ufichoni na wale waliokubaliwa na Serikali, sasa wanaishi kwa umoja na upendo kama ndugu wamoja. Baadhi ya Maaskofu kutoka China wamekwisha kutembelea Vatican. Kuna ushirikiano wa utamaduni unaoendelea kwa sasa kati ya China na Vatican. Vatican imekubali mwaliko wa Serikali ya China wa kushiriki katika “Expo Bejing 2019” yaani “Onesho la Kilimo cha Maua na Utunzaji Bora wa mazingira” na linaongozwa na kauli mbiu “Ishi kijani, Ishi vizuri zaidi”. Katika hali na mazingira kama haya, upinzani ni jambo la kawaida lakini hali hii ni kwa ajili ya watu wachache sana. Wakatoliki nchini China wameadhimisha kwa mara ya kwanza Fumbo la Pasaka kwa pamoja bila matatizo.

Mwishoni mwa mahojiano haya, Baba Mtakatifu amemshukuru kwa  namna ya pekee Valentina Alazraky wa Kituo cha Televisheni cha Taifa nchini Mexico. Amewakumbuka na kuwaombea wanawake wote wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo; wanawake wanaoteswa, kunyanyaswa na hatimaye, kuuwawa! Damu ya wanawake hawa iwe ni ushuhuda na changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wanawake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wamwombe Mwenyezi Mungu neema ya kuwalilia wanawake ambao: maisha, utu na heshima yao vinasiginwa kila kukicha!

Papa: TV Mexico

 

29 May 2019, 16:54