Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume! Papa Francisko ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume!  (Vatican Media)

Papa: Mzunguko Mpya wa Katekesi: Safari ya Injili Ulimwenguni: Ushuhuda!

Papa Francisko ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume. Hii ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji: Wahusika wakuu katika mchakato huu ni Neno la Mungu na Roho Mtakatifu. Ushuhuda wa Mitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 29 Mei 2019 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume. Hii ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana mchango wa Neno la Mungu na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji: Wahusika wakuu katika mchakato huu ni Neno la Mungu na Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu lina mwendo mkali, linapyaisha na kunyeeshea kila mahali linapopita. Mwenyezi Mungu ametumia maneno ya kibinadamu kwa njia ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu anayeyatia nguvu na kuyatakasa na hatimaye, kuyawezesha kuwa ni chemchemi ya maisha!

Biblia imesheheni maneno ya binadamu yaliyopata nguvu kwa njia ya Roho Mtakatifu kiasi kwamba, maneno haya yanakuwa ni mbegu ya utakatifu, maisha na ufanisi. Roho Mtakatifu anapotumia maneno ya binadamu, maneno haya yanageuka kuwa ni mwanga angavu unaovunjilia mbali: ukakasi wa moyo, kuta za utengano pamoja na kufungulia njia mpya zinazopanua wigo wa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, haya ndiyo mambo msingi atakayoyatafakari wakati wa Katekesi zake kuanzia sasa kutoka kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume. Roho Mtakatifu ndiye anayetia nguvu kwenye maneno ya binadamu na kuwawajibisha kikamilifu.

Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Ni Roho Mtakatifu ambaye anategemeza maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya Mitume, Roho Mtakatifu ameliwezesha Neno la Mungu kutangazwa, kushuhudiwa na kuendelea kudumu hadi leo hii. Injili inahitimishwa kwa Fumbo la Ufufuko na Kupaa Bwana Mbinguni kama linavyosimuliwa kwenye Matendo ya Mitume, yanayoonesha nguvu, kazi na utume wa Roho Mtakatifu anayeendeleza maisha ya Kristo Mfufuka yanayomwilishwa ndani ya Kanisa. Mwinjili Luka anasema, Yesu aliwatokea Mitume wake kwa muda wa siku arobaini na kuyanena mambo yaliyohusu Ufalme. Aliweza kushiriki nao chakula, akawataka kuwa na imani na matumaini naye na kwamba, wao watabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku chache.

Huu ni mchakato unaowaingiza waamini kuweza kuwa na ushirika na Mwenyezi Mungu, hatimaye, kushiriki pia katika kazi ya ukombozi wa ulimwengu kwa kujipatia kutangaza kwa uhuru na ujasiri wa watoto wa Mungu. Neno la Mungu ni kweli na haki linawapatia watu uhuru, lina nguvu. Limesheheni upendo kwa Kristo na jirani! Zawadi ya Mungu inatolewa bure kabisa na wala hakuna sababu ya kupambana au kudhani kwamba, ni haki ya mtu, bali inatolewa bure kabisa kwa wakati muafaka. Hakuna anayeweza kununua wokovu, kwa sababu ni zawadi ya Mungu! Hakuna sababu ya kujitaabisha kujua nyakati wala majira ambayo Mwenyezi Mungu ameyaweka katika mamlaka yake. Lakini watapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yao Roho Mtakatifu, nao watakuwa ni mashahidi wake katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mnwisho wa nchi.

Mitume wa Yesu walipaswa kujenga mahusiano na mafungamano mazuri na nyakati pamoja na majira; watambue jinsi ya kusubiria kushiriki katika historia takatifu inayosonga mbele, kwa kusikilizia hatua zinazopigwa na Mwenyezi Mungu katika majira na nyakati. Utume huu ni kazi ya Mwenyezi Mungu inayowashirikisha Mitume wa Yesu, baada ya kumpokea Roho Mtakatifu ndani mwao. Kwa njia hii wataweza kutoa ushuhuda wa kimisionari kwa kung’ara mjini Yerusalemu, Samaria hadi miisho ya dunia.Mitume wa Yesu waliweza kuingojea ahadi ya Baba wa milele kama familia wakiwa kwenye chumba cha juu, mahali ambapo Kristo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, uwepo wake endelevu kati ya wafuasi wake.

Wataweza kusubiri nguvu ya Roho Mtakatifu kwa kudumu katika sala; kwa kudumisha umoja na udugu, ili kuweza kuvunjilia mbali upweke, vishawishi na hali ya kudhaniana vibaya, ili kutoa nafasi kwa umoja na mshikamano. Baba Mtakatifu anakaza kusema, uwepo wa wanawake na Bikira Maria, Mama yake Yesu unaimarisha sana mang’amuzi haya. Wanawake wameweza kujifunza tangu mwanzo kutoka kwa Mwalimu wao, umuhimu wa kushuhudia uaminifu wa upendo na nguvu ya umoja na mshikamano wa dhati, ili kushinda hofu na wasi wasi inayoweza kujitokeza. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuomba neema ya kumngoja Roho Mtakatifu kwa uvumilivu, kwa kuwa wanyenyekevu, kwa kusali na kumwomba Roho Mtakatifu, lakini zaidi, kwa kujifunza na kudumisha sanaa ya ujenzi wa umoja wa Kanisa.

Papa: Matendo ya Mitume

 

 

29 May 2019, 15:39