Papa Francisko: Barua Binafsi: Vos estis lux mundi" yaani "Ninyi ni Nuru ya Ulimwengu": Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Papa Francisko: Barua Binafsi: Vos estis lux mundi" yaani "Ninyi ni Nuru ya Ulimwengu": Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia. 

Ninyi ni Nuru ya Ulimwengu: Sheria Mpya Dhidi ya Nyanyaso!

Papa anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa wanapaswa kuwajibika barabara. Wakleri na watawa wanapaswa kutoa taarifa na kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia.  Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wakleri na watawa kwamba, wao ni nuru ya ulimwengu na kwamba, Kristo Yesu anawaita na kuwataka kuwa waaminifu na mfano mahiri wa tunu msingi za maisha, uadilifu na utakatifu. Hii ni sehemu ya mafundisho mazito yaliyomo kwenye barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazoweza kutendwa na wakleri pamoja na watawa. Nyanyaso za kijinsia ni uhalifu unaosababisha madhara makubwa ya kimwili, kisaokolojia na kiroho si tu kwa waathirika bali haya kwa Jumuiya ya waamini. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Huu ni wajibu wao wa kimaadili. Hati hii ni matunda ya mkutano wa ulinzi wa watoto wadogo uliofanyika mjini Vatican, mwezi Februari 2019. Hizi ni sheria kwa ajili ya Kanisa Katoliki katika ujumla wake. Hadi kufikia Juni 2020, Majimbo yote ya Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, yatapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Sheria hii inahusu pia matumizi ya picha za ngono pamoja na viongozi wa Kanisa kuficha kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Kumbe, Sheria inatoa mwanya kwa kila jimbo kuhakikisha kwamba linatenda kadiri ya tamaduni na mazingira ya Kanisa mahalia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waathirika wa nyanyaso za kijinsia wanapokelewa na kusikilizwa, hata kama kunaweza kutokea pia shutuma za uongo, lakini shutuma hizi zitapaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Wakleri na watawa wote wanawajibika sasa kisheria kutoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia wanazozifahamu, haraka iwezekanvyo kwa uongozi wa Jimbo! Watapaswa pia kutoa taarifa pale ambapo kiongozi wa Kanisa hakutimiza wajibu wake au amefumbia macho uwepo wa nyanyaso za kijinsia katika eneo lake. Hadi wakati huu, wajibu wa kutoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa lilibaki ni jambo la dhamiri ya mtu binafsi, lakini kuanzia sasa na kuendelea huu ni wajibu wa kisheria kwa wakleri, watawa pamoja na waamini walei! Familia ya Mungu katika ujumla wake inapaswa kusimama kidete kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa kutoa taarifa. Hati hii inaendelea kuwabana hata wakleri wanapowakosea haki watawa au nyanyaso dhidi ya waseminari na wanavisi.

Kuficha kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni kesi ambayo imepewa uzito wa pekee kabisa. Haya ni matukio yanayoweza kufanyika moja kwa moja au kwa kutotimiza wajibu; kwa kuingilia au kuvuruga uchunguzi unaofanywa na vyombo vya kiraia au kadiri ya Sheria za Kanisa na uongozi dhidi ya mkleri au mtawa aliyemdhalilisha mtu kijinsia. Wahusika wakuu ni wale waliopewa dhamana na wajibu ndani ya Kanisa, badala ya kufuatilia kashfa ya nyanyaso za kijinsia zilizotendwa na watu wengine, wao wamezificha na kujenga ngome ya kuwalinda watuhumiwa badala ya kuwalinda waathirika.

Baba Mtakatiifu katika barua yake binafsi: “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ulinzi wa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 18 pamoja na watu wanyonge ndani ya jamii. Hili ni kundi ambalo linawaunganisha watu wote ambao licha ya kufikiri na kutenda kwa ufasaha, wanaweza kujikuta wametumbukia katika nyanyaso za kijinsia. Sehemu hii ya barua binafsi ya Baba Mtakatifu inafanya rejea kwenye Sheria za Vatican: Namba CCXCVII. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wajibu wa kutoa taarifa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, kwa namna yoyote ile haiwezi kuingiliana na sheria za nchi husika.

Kumbe, hapa kinachotakiwa ni kuhakikisha kwamba, sheria na wajibu wa wale wote wanaohusika zinatekelezwa kikamilifu. Wale wote wanaofikisha tuhuma za nyanyaso za kijinsia dhidi ya wakleri na watawa wanapaswa kulindwa na kamwe wasibezwe, kutengwa wala kudhalilishwa. Baba Mtakatifu anapenda kuona kwamba, waathirika wanasikilizwa kwa umakini mkubwa kuliko ilivyokuwa huko nyuma kwa kunyamazishwa. Lakini, ikumbukwe kwamba, siri ya maungamo inabaki kuwa ni siri ya maungamo na kamwe haiwezi kubatilishwa na Barua hii binafasi anasema Baba Mtakatifu Francisko. Waathirika pamoja na familia zao wanapaswa kusaidiwa: kiroho, kisaikolojia pamoja na kupewa huduma ya afya wanayohitaji.

Baba Mtakatifu anafafanua sheria, taratibu na kanuni zinazopaswa kuzingatiwa pale ambapo watuhumiwa ni kati ya: maaskofu, makardinali au wakuu wa mashirika ya kitawa, au wale wenye dhamana ya kuongoza jimbo hata ikiwa ni kwa kipindi kifupi. Viongozi hawa watawajibishwa kwa kesi za nyanyaso za kijinsia zilizofanywa moja kwa moja au zile ambazo, walizinyamazia, bila kuzishughulikia, ingawa walikuwa na habari kuhusu nyanyaso hizi! Itakuwa ni jukumu lao kuweza kujitetea. Askofu mkuu wa kanda husika atapewa dhamana na Vatican ya kufanya uchunguzi ikiwa kama mtuhumiwa ni Askofu.

Dhamana na wajibu wake kadiri ya Mapokeo ya Kanisa yanaendelea kuimarishwa sanjari na kuendelea kutumia rasilimali na utajiri wa Kanisa mahalia mintarafu uchunguzi dhidi ya askofu anayetuhumiwa. Askofu mkuu anayepewa dhamana ya kufanya uchunguzi, atapaswa katika muda wa siku 30 kutoa taarifa Vatican kuhusu uchunguzi uliofanywa na uchunguzi huu utapaswa kuwa umekamilika katika kipindi cha siku 90. Muda huu unaweza kuongezwa, ikiwa kama kutakuwepo na sababu msingi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Mabaraza ya Kipapa yanayohusika, yaweze kufanya maamuzi kwa haraka zaidi. Baba Mtakatifu Francisko katika Barua hii binafsi, anagusia pia nafasi ya waamini walei wenye uwezo na sifa, wanaweza kushirikiana na Askofu mkuu kufanya uchunguzi.

Waamini walei ni amana na utajiri mkubwa kwa Kanisa. Sheria hizi mpya zinayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Majimbo yote kuwaandaa watalaam watakaoweza kusimamia uchunguzi, lakini wajibu msingi unabaki kuwa chini ya Askofu mkuu. Baba Mtakatifu tangu mwanzo anasema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kanuni ya kutokuwa na hatia inaheshimiwa hadi pale Baraza lenye dhamana litakapokuwa limetoa taarifa. Mtuhumiwa hana budi kufahamishwa, ikiwa kama uchunguzi utaanza kufanyika kama sehemu ya utekelezaji wa taratibu za kawaida na kama itaonekana inafaa, ili kulinda uadilifu katika mchakato wa uchunguzi, vidhibiti au hatua hii inaweza kurukwa katika hatua za mwanzo!

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia anahitimisha kwa kukazia mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kufanya upelelezi wa kesi husika. Baada ya upelelezi kukamilika, Askofu mkuu, au Askofu mahalia mwenye umri mkubwa zaidi, anawasilisha uchunguzi wa tuhuma hizi kwenye Baraza linalohusika na huu ndio unakuwa ni mwisho wa dhamana yake.

Baraza linalohusika litaendelea kushughulikia kesi kadiri ya Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo. Baada ya uchunguzi na upelelezi kufanyika na matokeo yake kutumwa panapohusika, Vatican inaweza kuchukua hatua ili kujihami dhidi ya mtuhumiwa! Sheria hizi ni nyenzo muhimu sana kwa Kanisa Katoliki kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, kwa kukazia mambo msingi yanayopaswa kutekelezwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kuhakikisha kwamba, kashfa kama hizi, hazijirudii tena. Hapa kuna haja ya kuwa na wongofu endelevu kutoka katika undani wa waamini. Familia yote ya Mungu inahusishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Motu Prorio

 

14 May 2019, 09:45