Vatican News
Nia za Papa Francisko kwa Mwezi Mei 2019: Kanisa Barani Afrika: Liwe ni chachu ya umoja na matumaini ya familia ya Mungu Barani Afrika. Nia za Papa Francisko kwa Mwezi Mei 2019: Kanisa Barani Afrika: Liwe ni chachu ya umoja na matumaini ya familia ya Mungu Barani Afrika.  (AFP or licensors)

Nia za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Mei 2019: Kanisa Barani Afrika!

Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Mei 2019: Kanisa Barani Afrika liweze kuwa ni chachu ya umoja. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye kwa ajili ya kuombea shughuli za kitume na kichungaji zinazotekelezwa na Kanisa Barani Afrika, ili liweze kuwa ni chachu ya umoja na matumaini ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, kwa ajili ya Nia za Mwezi Mei 2019, analiombea Kanisa Barani Afrika liweze kuwa ni chachu ya umoja. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye kwa ajili ya kuombea shughuli mbali mbali za kitume na kichungaji zinazotekelezwa na Kanisa Barani Afrika. Kuna umati mkubwa wa wakleri, watawa, waamini walei pamoja na Jumuiya mbali mbali za Kikristo zinazotekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya familia ya Mungu Barani Afrika.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, utume huu, unapaswa kuwa ni chachu ya umoja na matumaini kwa familia ya Mungu Barani Afrika. Wananchi Barani Afrika wanaweza kuvuka vikwazo vya “mipasuko” ya kidini, kikabila na mahali anapotoka mtu kwa kujikita zaidi na zaidi katika umoja unaofumbata utofauti. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwashukuru: wakleri, watawa, waamini walei pamoja na wamisionari wanaoendelea kujisadaka kila kukicha ili kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano na upatanisho kati ya makundi ya watu mbali mbali katika Jamii ya watu wa Mungu Barani Afrika.

Ujumbe huu unaweza pia kupatikana kwa njia ya video kwa kubofya kwenye anuani ifuatayo: www.thepopevideo.org. Ujumbe huu, umetafsiriwa katika lugha tisa na Kampuni ya “La Machi” inayojihusisha kutengeneza na kusambaza ujumbe huu, kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Vatican Media ambayo imerekodi sauti ya Baba Mtakatifu Francisko.

Papa: Nia Mei 2019

 

11 May 2019, 14:26