Tafuta

Vatican News
Economy of Francesco: Uchumi wa Francisko ni tukio litakalowakusanya wachumi na wajasiriamali vijana zaidi ya 500 kuanzia tarehe 26-28 Machi 2020 mjini Assisi. Economy of Francesco: Uchumi wa Francisko ni tukio litakalowakusanya wachumi na wajasiriamali vijana zaidi ya 500 kuanzia tarehe 26-28 Machi 2020 mjini Assisi. 

Mkutano wa Uchumi wa Francisko: Assisi: 26-28 Machi 2020

Baba Mtakatifu Francisko katika tukio la "Economy of Francesco" yaani "Uchumi wa Francisko" anataka kuzama zaidi katika uchumi unaouhisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaokita mizizi yake katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Yote haya ni Assisi 26-28 Mei 2020.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni tukio ambalo litawakusanya wachumi na wajasiriamali wachumi vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 26- 28 Machi 2020 huko Assisi, nchini Italia. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, unaotekelezwa kwa namna ya pekee, na Baba Mtakatifu Francisko. Hii itakuwa ni nafasi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kukutana na kuzungumza na vijana wanaojifunza uchumi unaotekelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu!  Baba Mtakatifu anataka kuzama zaidi katika uchumi unaouhisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo.

Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaokita mizizi yake katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Jumanne, tarehe 14 Mei 2019, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, amewasilisha tukio hili kwa waandishi wa habari mjini Vatican. Viongozi wengine waliokuwa wameandamana naye ni pamoja na Askofu mkuu Domenico Sorrentino, wa Jimbo kuu la la Asisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino, Prof. Luigino Bruni, kutoka Chuo Kikuu cha LUMSA, Roma, Prof. Stefania Proietti, Meya wa Mji wa Assisi pamoja na Padre Mauro Gambetti, Mlinzi mkuu wa Konventi ya Assisi, wameshiriki katika tukio la kuwasilisha “Uchumi wa Francisko” kwa waandishi wa habari mjini Vatican.

Tukio hili la aina yake, linatarajiwa kuwakutanisha vijana zaidi ya mia tano huko Assisi. Nusu ya vijana hawa ni wale wanaotoka kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyojihusisha na uchumi. Kardinali Peter Turkson anasema, lengo la Baba Mtakatifu ni kuchochea mchakato wa mageuzi ya kiuchumi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ili dunia iweze kuwa na uchumi unaojikita katika misingi ya haki; uchumi fungamani au shirikishi bila kumwacha mtu awaye yote, kuchechemea nyuma ya maendeleo fungamani ya binadamu.

Askofu mkuu Domenico Sorrentino, wa Jimbo kuu la Asisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino anasema, huu ni mkutano utakaowajumuisha vijana watafiti katika shahada ya uzamivu kwenye masuala ya uchumi. Mkutano huu utafanyikia mjini Assisi, mji ambao kama alivyosema Mtakatifu Yohane Paulo II, unalenga kuwasaidia vijana kuchota “ari na moyo wa Assisi” mambo msingi yanayozingatiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake mintarafu uchumi jamii. Kwa bahati mbaya uchumi mamboleo unaoendelea kukumbatia utamaduni wa kifo, uharibifu wa mazingira pamoja na kuwakatisha watu tamaa ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa na kuanza kuelekezwa ili kujenga uchumi unaofumbatwa katika misingi ya: haki, udugu, fungamani pamoja na kuhakikisha kwamba, maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wanawezeshwa kikamilifu, ili kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Askofu mkuu Domenico Sorrentino anakiri kwamba, amepokea changamoto na mwaliko huu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ari na moyo wa unyenyekevu. Katika utekelezaji wa mradi huu, anatarajia kuwashirikisha watu wa Mungu wanaoishi mjini Assisi, ili kuonja upendo usiokuwa na mipaka kama ilivyokuwa kwa Taasisi hii ya Mtakatifu Francisko iliyoanzishwa kunako mwaka 1871.

Taasisi hii ikawa ni chombo cha huduma kwa walemavu na leo hii ni kielelezo cha mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ndiyo dhana ya uchumi unaojikita katika huduma ya upendo wa dhati, ili kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto kubwa kwa vijana kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi wakati wa ujana wake, aliposigana na maamuzi ya Baba yake mzazi na kuamua kuambata tunu msingi za Kiinjili na hivyo kuyapatia kisogo malimwengu, leo hii ni mfano bora wa kuigwa katika kutafuta na kudumisha amani, utunzaji bora wa mazingira pamoja na huduma kwa maskini, matendo makuu ya Mungu.

Kanuni maadili ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ujirani mwema, ni kati ya mambo msingi yaliyovaliwa njuga na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, anataka kuunganisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unaojikita katika ekolojia na uchumi fungamani. Kwa upande wake, Prof. Luigino Bruni, kutoka Chuo Kikuu cha LUMSA, Roma anasema, mkutano wa “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni sehemu ya utekelezaji wa mbinu mkakati wa utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto endelevu iliyotolewa na vijana wakati wa maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linawajengea vijana uwezo wa kupambana na changamoto za maisha pamoja na kuendelea kuwamotisha wale vijana wanaojipambanua katika ujenzi wa misingi ya uchumi fungamani, yaani uchumi unaofumbatwa katika udugu wa binadamu na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Malezi na majiundo makini ya vijana ni kati ya mambo yanayopewa kipaumbele na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu! Prof. Luigino Bruni kuhusu “Uchumi wa Francisko” anakaza kusema, hili ni tukio ambalo litawakusanya wachumi na wajasiriamali vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 26-28 Machi 2020 huko Assisi. Huu ni mwanzo mpya wa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya.

Kardinali Turkson anasema, huu ni uchumi jamii unaojikita katika huduma kwa binadamu, ili kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki zake msingi. Ni uchumi unaofafanuliwa na Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” pamoja na Wosia wake wa Kitume: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” dira na mwelekeo wa maisha na shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Ni uchumi unaoratibu matumizi ya rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Prof. Luigino Bruni ambaye amepewa dhamana ya kuratibu tukio la“Uchumi wa Francisko” Machi 2020 anasema, ni nafasi ya kuweza kutafakari tema msingi zinazopewa kipaumbele na Baba Mtakatifu Francisko katika utume wa Kanisa kwa vijana, uchumi fungamani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mji wa Assisi ni mahali muafaka pa kuweza kutafakari kwa kina kuhusu: Vijana, Mazingira na Maskini. Mtakatifu Francisko alikuwa chachu ya uchumi mpya na Wafranciskani katika maisha na utume wao, wamekuwa ni waasisi wa uchumi mpya Barani Ulaya.

Ni katika sera, mipango na mikakati yao, huo ukawa ni mwanzo wa Benki nyingi duniani. Katika umaskini wao, wakasukumwa kuwashirikisha maskini utajiri unaobubujika kutoka katika sadaka na majitoleo yao ya kila siku. Wafranciskani ni waasisi wa dhana ya uchumi fungamani na utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya matumaini, kwa kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, usawa, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa dhati. Tukio hili linataka kuwashirikisha hata vijana wanaotoka katika Nchi maskini, ili hata wao katika umaskini wao, waweze kuwa ni chachu ya mageuzi ya kiuchumi!

Uchumi wa Francisko 2020

 

16 May 2019, 16:34