Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma kuanzia tarehe 23-27 Juni 2021. Kauli mbiu: Upendo wa familia: Wito na njia ya Utakatifu wa maisha. Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma kuanzia tarehe 23-27 Juni 2021. Kauli mbiu: Upendo wa familia: Wito na njia ya Utakatifu wa maisha. 

Mkutano wa Familia Duniani, Juni 2021 Roma: Upendo & Utakatifu

Papa Francisko anasema Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma, nchini Italia, kuanzia tarehe 23-27 Juni 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Hii itakuwa ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka mitano ya: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma, nchini Italia, kuanzia tarehe 23-27 Juni 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Hii itakuwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mitano tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia.

Kanisa litakuwa pia linakumbuka miaka mitatu tangu Baba Mtakatifu achapishe Waraka wake wa kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani Yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Lengo la Wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la kuchagua tema hii ni kutaka kukazia mchakato wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika uhalisia wa kila siku wa mahusiano ndani ya familia.

Nyaraka hizi mbili za Kipapa ziwe ni rejea mahususi katika maandalizi ya Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani kwa mwaka 2021 utafanyika mjini Roma. Upendo wa wanandoa ndani ya familia ni kielelezo cha zawadi kubwa inayowaunganisha wanandoa ili kurutubisha umoja na hivyo kubadilisha mwelekeo wa tabia ya ubinafsi, ulaji wa kupindukia pamoja na tabia ya kutupa: “Uzuri wa upendo unadhihirishwa kwa ile namna ya “kutazama” kunakowatafakari wengine kuwa ni malengo kama walivyo” (AL 128). Wakati huo huo kutambua watu wengine ndani ya familia takatifu kama: mume, mke, baba, mama, mtoto, binti, babu au bibi.

Ndoa na familia inatoa sura kamili ya upendo na kushuhudia maana ya mahusiano ya kibinadamu ambamo furaha na mapambano ya maisha yanakuwa ni sehemu ya vinasaba vya kila siku, vinavyowaongoza watu ili kukutana na Mwenyezi Mungu. Wanandoa wanapoiishi safari hii kwa uaminifu na udumifu, wanaimarisha upendo na wito wa utakatifu wa maisha unaomilikiwa na kila mmoja wao na kumwilishwa katika mahusiano ya ndoa na familia. Kwa maana hii basi, maisha ya familia ya Kikristo ni wito na njia ya utakatifu, “kielelezo makini cha sura ya Kanisa inayovutia” (GE  9).

Familia 2021: Roma
20 May 2019, 09:42