Papa Francisko nchini Macedonia ya Kaskazini anapenda kupandikiza mbegu ya utamaduni wa watu kukutana pamoja na udugu Papa Francisko nchini Macedonia ya Kaskazini anapenda kupandikiza mbegu ya utamaduni wa watu kukutana pamoja na udugu 

Hija ya kitume: Bulgaria & Macedonia ya Kaskazini: Udugu & Umoja

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Barani Ulaya na Ulimwenguni kote, utamaduni wa watu kukutana pamoja na utmaduni wa udugu vinakuzwa. Hizi ndizo mbegu ambazo angependa kuzipandikiza nchini Macedonia ya Kaskazini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mbegu hizi zitakuzwa katika tamaduni, makabila na dini mbali mbali nchini humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Macedonia ya Kaskazini tarehe 7 Mei 2019 inaongozwa na kauli mbiu: “Msiogope enyi kundi dogo”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa familia ya Mungu Macedonia ya Kaskazini anapenda kuonesha furaha yake kwa Kanisa na wananchi wa Macedonia ya Kaskazini katika ujumla wao. Baada ya Macedonia ya Kaskazini kujipatia uhuru wake kunako mwaka 1908, ikaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, uhusiano ambao umejengeka katika msingi wa urafiki.

Baba Mtakatifu anasema, leo hii, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Barani Ulaya na Ulimwenguni kote, utamaduni wa watu kukutana pamoja na utamaduni wa udugu vinakuzwa. Hizi ndizo mbegu ambazo angependa kuzipandikiza wakati wa hija yake ya kitume nchini Macedonia ya Kaskazini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, familia ya Mungu nchini humo itaweza kuzipokea mbegu hizi na kuzistawisha katika tamaduni, makabila na dini mbali mbali, miongoni mwa wananchi wake.

Maridhiano kati ya watu ni changamoto, lakini hii ni changamoto ambayo inapaswa kuvaliwa njuga kama sehemu ya utajiri wa Macedonia ya Kaskazini. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video, kwa kujiaminisha chini ya maombezi ya Mtakatifu Mama Theresa wa Calcuta, aliyezaliwa mjini Skopje (SKOPIE) na kwa neema ya Mungu akabahatika kuwa mmisionari hodari wa upendo wa Kristo sehemu mbali mbali za dunia. Ni mwanamke wa shoka aliyesimama kidete kuwapatia maskini kati ya maskini, utu na heshima yao. Baba Mtakatifu anaialika familia ya Mungu nchini Macedonia ya Kaskazini kwa sala, ili amani na ustawi viweze kuwafikia watu wa Mungu nchini humo!

Papa: Macedonia K.
03 May 2019, 18:17