Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 anafanya hija ya kitume nchini Bulgaria na Macedonia ya Kaskazini. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 anafanya hija ya kitume nchini Bulgaria na Macedonia ya Kaskazini. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko: Bulgaria & Macedonia ya Kaskazini

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bulgaria na Macedonia ya Kaskazini kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 inaongozwa na kauli mbiu "Pacem in terris" yaani "Amani duniani" pamoja na "Msiogope enyi kundi dogo". Hija hii inapania kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; pamoja na kuwawezesha waamini kukua na kukomaa katika ukweli, umoja na ustawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Bulgaria pamoja na Macedonia ya Kaskazini na hivyo anatarajiwa kufanya hija ya kitume katika nchi hizi mbili kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019. Hii ni hija ya 29 ya Baba Mtakatifu Kimataifa. Akiwa nchini Bulgaria, atatembelea mji wa Sofia na Rakovski. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bulgaria inaongozwa na kauli mbiu “Pacem in terris”, yaani “Amani duniani”, mwangwi wa Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane XXIII “Pacem in terris” anayekazia umuhimu wa haki, uhuru, ukweli, upendo na msamaha kama mambo msingi ya kujenga na kudumisha amani duniani sanjari na kukuza mahusiano mema kati ya wananchi na viongozi wao, Jumuiya za kisiasa na ulimwengu katika ujumla wake.

Familia ya Mungu nchini Bulgaria imekuwa ikisali kama sehemu ya maandalizi ya hija hii ya kitume, kwa kuombea amani pamoja na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaohitaji msaada wao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha, matumaini, msamaha na upatanisho. Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya amani, awakirimie waja wake amani ambayo wanapaswa kutangaza na kuishuhudia kwa njia ya maisha yao, kwani uwepo wa amani duniani ni jambo linalowezekana, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa!

Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili nchini Bulgaria, Jumapili asubuhi, kwenye Uwanja wa Ndege wa Bulgaria atalakiwa na Waziri mkuu, Bwana Boyko Borisov na baadaye, ataelekea Ikulu na hapo atapata mapokezi ya kitaifa na hatimaye, kukagua gwaride la heshima. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kumtembelea Rais Rumen Radev wa Bulgaria na hatimaye atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, viongozi wa kijamii pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao huko Bulgaria. Hija hii ya kitume, inapania pia kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Patriaki Neofit pamoja na wajumbe wa Sinodi Takatifu. Hapa Baba Mtakatifu anatoa hotuba yake ya pili. Majira ya mchana, Baba Mtakatifu atatembelea Kanisa kuu la Kipatriaki na hapo atasali mbele ya kiti cha Watakatifu Cyrili na Metodi wanaoheshimika sana kwa mchango wao katika uinjilishaji na utamadunisho wa Neno la Mungu pamoja na Liturujia. Akiwa mbele ya Kanisa, kwenye Uwanja wa Mtakatifu Alexander Nevsky, atawaongoza waamini kwa Sala ya Malkia wa Mbingu na majira ya alasiri, ataongoza Ibada ya Misa Takatifu Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka, kwenye Uwanja wa Knyaz Alexander 1 na baada ya maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa anahitimisha siku yake ya kwanza nchini Bulgaria.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Jumatatu, tarehe 6 Mei 2019, Baba Mtakatifu atatembelea Kambi ya Wakimbizi ya Vrazhdebna, iliyofunguliwa kunako mwaka 2013 na iko nje kidogo ya mji wa Sofia. Baadaye, Baba Mtakatifu ataelekea mjini Rakovski na huko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Komunyo ya kwanza kwa watoto waliojiandaa. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu huko Rakovsky. Atapata chakula cha mchana na Maaskofu watatu wa Kanisa Katoliki nchini Bulgaria. Hawa ni Maaskofu wa Majimbo Katoliki ya Nicopoli, Sofia na Filippopoli.

Majira ya Alasiri, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki kwenye Kanisa la Malaika mkuu Mikaeli huko Rakovsky. Hii itakuwa ni nafasi kwa Baba Mtakatifu kusikiliza shuhuda za familia ya Mungu nchini Bulgaria na hatimaye, atatoa hotuba yake. Mara baada ya tukio hili, Baba Mtakatifu ataelekea mjini Sofia ili kushiriki Ibada ya amani, itakayowashirikisha pia waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Bulgaria na atatoa tafakari yake. Jioni atakutana na kuzungumza kwa faragha na wafanyakazi pamoja na wafadhili wa hija hii ya kitume nchini Bulgaria. Huu utakuwa ni mwisho wa hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bulgaria.

Baraza la Maaskofu Katoliki la Macedonia ya Kaskazini, linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali na kuitikia mwaliko wa kuwatembelea, ili kuwabariki na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Maaskofu wanamwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kuwa kweli ni vyombo vya amani na utulivu nchini mwao. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu nchini humo inaongozwa na kauli mbiu “Msiogope enyi kundi dogo” Lk. 12:32. Familia ya Mungu nchini Macedonia ya Kaskazini, inamwomba Mwenyezi Mungu, aibariki nchi yao, na wao wakue na kukomaa katika ukweli na umoja, daima wakichuchumilia ustawi wa wengi na utukufu wa Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa Macedonia ya Kaskazini, Jumanne, tarehe 7 Mei 2019 atatembelea mji wa Skopje, mahali alikozaliwa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini! Atalakiwa kitaifa na baadaye atatembelea Ikulu ili kukutana na Rais Gjorge Ivanov wa Macedonia ya Kaskazini. Atakutana na kuzungumza kwa faragha na Waziri mkuu, baadaye atakutana na viongozi wa Serikali, jumuiya za kiraia pamoja na wanadiplomasia, wanaowakilisha nchi zao huko Macedonia ya Kaskazini.

Baba Mtakatifu atatembelea sehemu ya Makumbusho wa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, mbele ya viongozi wa kidini pamoja na kukutana na maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu atasali kwa ajili ya heshima ya Mtakatifu Theresa wa Calcutta. Majira ya mchana, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Macedonia. Atapata chakula cha mchana na Baraza la Maaskofu Katoliki Macedonia ya Kaskazini na majira ya jioni, ataongoza Sala ya Kiekumene na Kidini pamoja na vijana. Jioni, Baba Mtakatifu atakuna na wakleri na watawa pamoja na familia zao kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu. Atasikiliza shuhuda na baadaye, atakuwa anahitimisha hija yake 29 ya kitume kimataifa na hivyo kuanza safari ya kurejea tena Vatican.

Papa: Bulgaria

 

02 May 2019, 16:05