Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake nchini Bulgaria anapenda kupandikiza mbegu ya imani, umoja na amani! Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake nchini Bulgaria anapenda kupandikiza mbegu ya imani, umoja na amani!  (AFP or licensors)

Hija ya kitume: Bulgaria & Macedonia ya Kaskazini: Amani Duniani

Papa anasema, Mungu akipenda, huku akiwa anafuatana na waandamizi wake, wanafanya hija ya kitume nchini Bulgaria kama alama ya: imani, umoja na amani! Bulgaria ni nchi ambayo imekuwa ni shuhuda wa imani, tangu wakati wa akina Mtakatifu Cyril na Metodi, waliopandikiza mbegu ya Injili, ikazaa matunda hata nyakati ngumu za historia na maisha ya Kanisa katika Karne iliyopita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa familia ya Mungu nchini Bulgaria, kama sehemu ya maandalizi ya hija yake kitume nchini humo kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 anasema, Mwenyezi Mungu akipenda, huku akiwa anafuatana na waandamizi wake, wanafanya hija ya kitume nchini humo kama alama ya: imani, umoja na amani! Bulgaria ni nchi ambayo imekuwa ni shuhuda wa imani, tangu wakati wa akina Mtakatifu Cyril na Metodi, waliopandikiza mbegu ya Injili, ikazaa matunda hata nyakati ngumu za historia na maisha ya Kanisa katika Karne iliyopita!

Mtakatifu Yohane Paulo II alipenda kurudia akiwataka waamini Barani Ulaya, kugundua ndani mwao, ile nguvu ya Kristo Yesu inayookoa, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya Kiekumene. Baba Mtakatifu anasema, akiwa nchini Bulgaria, atakutana na Patriaki pamoja na Wajumbe wa Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiorthodox nchini Bulgaria. Kwa pamoja wanapenda kushuhudia ile nia ya kuendelea kumfuasa Kristo Yesu katika njia ya umoja wa kidugu na Wakristo wote.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, hija hii ni sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya Mtakatifu Yohane XXIII, aliyebahatika kufanya kazi na kuishi mjini Sofia kwa takribani miaka 10. Katika kipindi chote hiki, akajenga mafungamano na heshima ya pekee sana kwa familia ya Mungu nchini Bulgaria. Mtakatifu Yohane XXIII alikuwa ni mtu wa imani, umoja na amani. Ndiyo maana hija hii ya kitume nchini Bulgaria inaongozwa na kauli mbiu “Pacem in terris” yaani “Amani duniani” na kwa Kibulgeria “Mir na zemyata”.

Mwishoni mwa ujumbe wake kwa njia ya video, Baba Mtakatifu Francisko tangu sasa anapenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa njia ya sala. Mwishoni, anaombea amani na ustawi kwa familia ya Mungu nchini Bulgaria!

Papa Bulgaria

 

 

03 May 2019, 18:00