Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika hotuba yake amekazia: Utamaduni wa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu; Majadiliano ya Kiekumene; Wahamiaji & Utamaduni wa watu kukutana! Papa Francisko katika hotuba yake amekazia: Utamaduni wa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu; Majadiliano ya Kiekumene; Wahamiaji & Utamaduni wa watu kukutana!  (AFP or licensors)

Hija ya kitume: Bulgaria & Macedonia ya Kaskazini: Hotuba: wanadiplomasia

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu; ushirikiano wa kiekumene, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nchini Bulgaria pamoja na kujenga utamaduni wa watu kutoka katika tamaduni, makabila, staarabu na dini mbali mbali kukutana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 29 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bulgaria kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Pacem in terris” yaani “Amani duniani” na kwa Kibulgaria “Mir na zemyata”. Baba Mtakatifu baada ya kuwasili na kupokelewa kwa heshima zote za kitaifa. Amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza kwa faragha na Bwana Boyko Borisov kwenye Uwanja wa Ndege, baadaye akamtembelea Rais Rumen Radev na hatimaye, kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, viongozi wa kijamii pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchini zao kwenye Uwanja wa Atanas Burov, mjini Sofia, Bulgaria.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu; ushirikiano wa kiekumene, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nchini Bulgaria pamoja na kujenga utamaduni wa watu kutoka katika tamaduni, makabila, staarabu na dini mbali mbali kukutana. Baba Mtakatifu anasema, Bulgaria ni makutano ya tamaduni na staarabu mbali mbali;  ni daraja kati ya Mashariki na Kusini mwa Bara la Ulaya ni mahali pa watu wa Mataifa kukutana, iili kutajirishana na wala si sababu ya kinzani na mipasuko!

Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Serikali, wakuu mbali mbali wa kidini pamoja na wanadiplomasia na kuwahimiza kwamba, wote wanayo dhamana na jukumu la kukuza na kudumisha misingi: amani, maridhiano na utulivu. Mazingira ya Bulgaria yachangie ukuaji wa utamaduni na mazingira ya kuheshimu binadamu na utu wake; kwa kujenga na kuimarisha tamaduni na mapokeo mbali mbali, kwa kukataa kishawishi kinachoweza kuwatumbukiza kwenye kinzani na mipasuko mbali mbali. Anakaza kusema, wale wanaonuia kuvuruga na hatimaye kunyonya eneo hili watashindwa.

Hija ya Baba Mtakatifu nchini Bulgaria ni kumbukizi la hija iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II nchini humo kunako mwaka 2002 pamoja na uwepo wa Mtakatifu Yohane XXIII nchini humo kwa muda wa miaka 10 kama Balozi wa Vatican. Ni kiongozi alijejisadaka kujenga na kudumisha ushirikiano wa kidugu miongoni mwa Wakristo na huo ukawa ni mwanzo cha majadiliano ya kiekumene, yaliyopewa msukumo wa pekee wakati wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Tangu mwaka 1968 viongozi wa ngazi za juu kutoka Bulgaria wamekuwa wakitembelea mjini Vatican wakati wa kumbu kumbu ya Watakatifu Cyril na Methodi, waliojisadaka kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji, ukuzaji wa lugha ya Kislav, utamaduni, lakini kubwa zaidi, wamekuwa ni mashuhuda na chemchemi ya utakatifu wa Kikristo. Watakatifu hawa ni wasimamizi wa Bara la Ulaya, alama ya majadiliano, amani na udugu unaoyakutanisha waamini, nchi pamoja na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, tayari kuanza mchakato wa amani na maridhiano kati ya watu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, imegota miaka 30 tangu utawala wa mabavu ulipong’olewa nchini Bulgaria, lakini kwa sasa changamoto kubwa mbele yao ni watu zaidi ya milioni mbili wanaotafuta fursa za ajira. Bulgaria nayo inakabiliana na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa kila mwaka, kama ilivyo hata kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya, hali inayokatisha tamaa kwa kesho iliyo bora zaidi. Kuna baadhi ya vijiji na miji ambayo kwa sasa imebaki mahame baada ya kukimbiwa na watu.

Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Bulgaria kufungua macho na nyoyo zao, tayari kuwakaribisha wale wote wanaobisha hodi katika malango ya mipaka ya nchi yao. Hawa ni watu wanaokimbia: vita, kinzani na umaskini; wanatafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza viongozi wa Serikali ya Bulgaria kuhakikisha kwamba, wanawekeza kwa vijana ili waweze kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kuwa na maisha yenye hadhi na utu wa binadamu. Rasilimali mbali mbali zilizoko nchini Bulgaria ziwe ni ufunguo wa kitamaduni na ukuaji wa biashara kwa nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Urussi pamoja na Uturuki, ili kuwakirimia vijana matumaini zaidi!

Papa: Hotuba Viongozi
05 May 2019, 13:32