Papa Francisko amekutana na kuzungumza na Patriaki Neofit wa Kanisa la Kiorthodox nchini Bulgaria pamoja na Wajumbe wa Sinodi Takatifu: Uekumene wa damu na maskini! Papa Francisko amekutana na kuzungumza na Patriaki Neofit wa Kanisa la Kiorthodox nchini Bulgaria pamoja na Wajumbe wa Sinodi Takatifu: Uekumene wa damu na maskini! 

Hija ya kitume: Bulgaria & Macedonia ya Kaskazini: Uekumene wa damu

Katika majadiliano ya kiekumene, kuna mashuhuda wengi wa Fumbo la Pasaka, ambao wamejisadaka na kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ndio uekumene wa damu, uliowawezesha kutangaza harufu nzuri ya Injili inayobubujika kutoka katika imani na utu wema. Mapokeo ya Kimonaki yamesaidia sana kurutubisha imani ya familia ya Mungu nchini Bulgaria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jumapili ya Mtakatifu Tomaso kwa Makanisa ya Mashariki, yaani tarehe 5 Mei 2019, amekutana na Patriaki Neofit wa Kanisa la Kiorthodox nchini Bulgaria pamoja na Wajumbe wa Sinodi Takatifu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu. Lengo ni kukiri kwa pamoja kwamba, Kristo Yesu ni Bwana na Mungu wao. Kwa pamoja watambue mapungufu yao kama binadamu, tayari kujitumbukiza katika upendo wa Kristo unaobubujika kutoka katika Madonda yake Matakatifu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa njia hii, kwa pamoja wataweza kugundua furaha ya msamaha, tayari kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu wakiwa wameungana. Katika hija ya majadiliano ya kiekumene, kuna mashuhuda wengi wa Fumbo la Pasaka, ambao wamejisadaka na kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake katika karne iliyopita. Huu ndio uekumene wa damu, uliowawezesha kutangaza harufu nzuri ya Injili inayobubujika kutoka katika imani na utu wema. Mapokeo na maisha ya Kimonaki yamesaidia sana kurutubisha imani ya familia ya Mungu nchini Bulgaria.

Mashuhuda wa uekumene wa damu kutoka katika Makanisa mbali mbali kwa sasa wanaunganishwa na kifungo cha upendo huko mbinguni. Mbegu waliyopandikiza duniani, itazaa matunda kwa wakati wake. Hata katika ulimwengu mamboleo, bado kuna Wakristo wanaoendelea kuteseka kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha huu, Mashuhuda wa uekumene wa damu, wanawataka Wakristo kubaki wakiwa wameungana, ili mbegu hii iweze kuzaa matunda ya umoja.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, mkutano huu ni mwendelezo wa mkutano uliofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II na Patriaki Maxim na kama mwendelezo wa maisha ya Mtakatifu Yohane XXIII wakati wa maisha yake. Papa Yohane XXIII aliwapongeza watu wa Mungu kwa: uaminifu, kwa kuchapa kazi pamoja na kudumisha utu wao hata wakati wa majaribu makubwa, kielelezo kikuu kinachothamini udugu, tayari kuanza mchakato wa umoja wa Wakristo!

Ujumbe kutoka Kanisa la Kiothodox ulihudhuria wakati wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kila mwaka, kumekuwepo na ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Bulgaria unaotembelea Vatican. Kumekuwepo na ushirikiano mzuri wa kitamaduni kati ya Jumuiya za Kikatoliki na Kanisa la Kiothodox. Matukio yoye haya yameendelea kuimarisha majadiliano ya kiekumene. Umefika wakati wa kufanya hija na kutenda kwa umoja, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kwa njia ya uekumene wa huduma kwa maskini.

Watakatifu Cyril na Methodi walisimama kidete katika mchakato wa utume wa Uinjilishaji, mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya utengano miongoni mwa Wakristo. Wao ni mashuhuda wa utume na umoja, changamoto na mwaliko wa kukua na kukomaa katika udugu ili kujenga uekumene wa utume! Watakatifu hawa ni mfano na vyombo vya uinjilishaji kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuhakikisha kwamba, tamaduni na mapokeo mbali mbali ya Makanisa haya yanawasaidia vijana wa kizazi kipya kupata mang’amuzi ya furaha ya uwepo wa Mungu katika maisha yao. Vinginevyo, vijana hawa watajikuta wakimezwa na jamii inayojikita katika ulaji wa kupindukia!

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kukazia: Umoja na utume; Ukaribu na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, kama walivyofanya watakatifu hawa, ili kujenga umoja wa Ulaya, kulinda amani, kuishi kwa umoja na upendo; kwa kushirikiana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti msingi. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa umoja na amani kwa jina la Kristo Yesu. Bulgaria ni makutano ya tunu msingi za maisha ya kiroho; mahali ambapo watu wengi wanaweza kukutana na hatimaye wakaelewana.

Bulgaria imebahatika kuwa na waamini wengi wa dini ya Kiislam, Kiyahudi, Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Kanisa Katoliki linaheshimiwa katika Mapokeo ya dini na Makanisa mbali mbali ya Kikristo. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa la Kiorthodox kwa mapokeo mazuri waliyomkirimia. Tofauti zao za Mapokeo na tamaduni zisaidie kuboresha amana hii kwa kukamilishana badala ya kuwa ni chanzo cha kinzani. Makanisa haya yanaweza kujifunza zaidi kutoka kwa jirani zao.

Watakatifu mbali mbali wa Kanisa wawe ni madaraja ya kuwakutanisha Wakristo nchini Bulgaria. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, hii ni hija ya uekumene wa damu, uekumene wa utume na maskini. Kwa njia ya sala, ukweli na uwazi, mambo mengi yanaweza kutendeka! Ataendelea kuhifadhi kwenye sakafu ya moyo wake, kumbu kumbu ya hija hii ya kitume nchini Bulgaria!

Papa: Patriaki Neofit

 

 

05 May 2019, 13:58