Papa Francisko: Mahubiri Misa Takatifu: Mwenyezi Mungu: Anaita; Anashangaza na Kupenda! Papa Francisko: Mahubiri Misa Takatifu: Mwenyezi Mungu: Anaita; Anashangaza na Kupenda! 

Hija ya kitume: Bulgaria: Mungu: Anaita, Anashangaza & Anapenda!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia mambo makuu matatu; muhimu kwa maisha ya mfuasi wa Kristo yaani: Mwenyezi Mungu anaita; Mwezi Mungu anashangaza na kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda! Christos vozkrese! Yaani Kristo Amefufuka kweli kweli! Huu ndiyo ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kutoka kwa Kristo Mfufuka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 5 Mei 2019 wakati wa hija yake ya kitume nchini Bulgaria, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa  Knyaz Alexandar I na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia mambo makuu matatu; muhimu kwa maisha ya mfuasi wa Kristo yaani: Mwenyezi Mungu anaita; Mwezi Mungu anashangaza na kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda! Christos vozkrese! Yaani Kristo Amefufuka kweli kweli!

Mwenyezi Mungu anaita! Kristo Yesu akiwa kando ya Ziwa la Genesareti alimwita Mtakatifu Petro na kumwambia kuacha yote na kuanza kumfuasa, kwani atakuwa ni mvuvi wa watu! Baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, Mtume Petro alirejea tena katika kazi yake ya awali na mitume wengine wakaamua kumfuata huko Ziwani, dalili za Mitume wa Yesu, kuanza kurejea tena nyuma na kuchukua nyavu zile walizokuwa wameziacha kwa muda wa miaka mitatu. Kashfa ya Msalaba iliwaelemea sana Mitume wa Yesu, ikawa kana kwamba, kuna jiwe kubwa lililokuwa limezamishwa katika sakafu ya nyoyo zao. Baba Mtakatifu anasema, Mitume walikuwa wamezama katika mateso na huku wakisutwa na dhamiri zao, kwani Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ilikuwa bado haijazamisha mizizi yake katika sakafu ya nyoyo zao!

Mwenyezi Mungu anatambua kishawishi kikubwa kinachowaandama waja wake, ni kile cha kutaka kurejea tena katika mambo ya kale, kutokana na mapungufu pamoja na madonda ya maisha, kwani mambo yanakwenda si kadiri ya matamanio ya binadamu. Hili li kaburi la Kisaokolojia anasema Baba Mtakatifu linalobeza kila kitu na kumfanya mwamini aanze kujihurumia mwenyewe na hatimaye, kuporomosha matumaini aliyokuwa nayo katika maisha! Hii ni hatari inayoweza kujitokeza katika Jumuiya yoyote ile pale inapodhani kwamba, mambo yanakwenda kama kawaida, lakini, ukweli wa mamboo unaonesha kwamba, imani inadhohofu na kuanza kudidimia kwenye hali ya ufinyu wa mawazo.

Katika hali ya Mtakatifu Petro kukata tamaa na kuanza kuelemewa na mapungufu yake ya kibinadamu, Kristo Yesu anamtokea na kumwita kwa upole, “Simoni”, Jina Petro, yaani “Mwamba” alipewa na Kristo Yesu alipomwita kwa mara ya kwanza. Yesu alimtambua fika Mtakatifu Petro na wala hakutegemea kukutana na watu wasiokuwa na matatizo, dhambi wala mapungufu katika maisha. Kristo Yesu, alipambana na dhambi na hali ya kutaka kukata tamaa, ili kuwatia shime waja wake, ili waweze kudumu. Anaendelea kuwaita, huku akiwapenda kwa dhati pamoja na kuwapatia nafasi nyingine tena ya kujaribu kupyaisha upendo unaojikita katika upya wake wa milele. Kila siku ya kwanza ya Juma, Kristo Mfufuka, anakutana na waja wake, ili kuwanyanyua juu ili watambue kwamba, wameumbwa kwa ajili ya mambo ya mbinguni, mambo ya maisha na wala si kwa ajili ya mambo ya duniani na hatimaye, kifo.

Wale wanaothubutu kumkaribisha, ataweza kuwainua tena na hivyo kukumbatia ya mbeleni kwa matumaini kwani inawezekana kabisa. Yesu anapomwita mtu, anaongoza maisha yake na nyoyo za waamini wake zinapyaishwa na kupata ujana zaidi.  Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyezi Mungu ni Bwana wa mshangao, anaendelea kuwashangaza waja wake! Anawataka kuwa wavuvi wa watu pasi na nyafu; anawataka kuvua mchana kweupe, kinyume cha taratibu zinazofahamika kwa wavuvi! Jambo la msingi analotaka kutoka kwao ni kuthubutu! Ili waweze kuvunjilia mbali, hali ya kutojiamini, hofu na woga! Mwenyezi Mungu anataka kuwazamisha waja wake si tu wakiwa na nyavu zao, bali wao wenyewe, ili kuweza kuyaangalia tena maisha yao ya dhambi, ili waweze kuzaliwa tena upya, wakitambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu, jinsi walivyo!

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu anaita, anaendelea kuwashangaza waja wake lakini zaidi anawapenda! Ndiyo maana Kristo Yesu alimuuliza Mtakatifu Petro mara tatu, ikiwa kama kweli alikuwa anampenda! Petro anatambua kwamba, kwa hakika Yesu anampenda na anapaswa kuwa ni kiini cha upendo wenyewe! Petro anatambua udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu na kwamba, bila kushikwa mkono na Kristo Yesu, “hawezi kufua dafu, maji ni mazito” atazama kama jiwe! Upendo wa Kristo ni nguvu inayookoa hadi mwisho! Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake ndiyo maana anawataka kupyaisha kila siku upendo huu, licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu.

Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka kutoka Bulgaria waliongozwa na imani pamoja na upendo kwa Mungu, kiasi hata cha kusadaka maisha yao na kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka. Ni watu walioshinda ubaya kwa ujasiri na kutoa majibu ya Kikristo baada ya kukutana na Kristo. Leo hii Wakristo wanaitwa kuinua macho yao, ili kutambua mambo makubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewatendea katika maisha, tayari kuandamana pamoja naye kuyaelekea ya mbeleni, kwa kutambua kwamba, daima atakuwa pamoja nao, akiwasihi kushusha nyavu zao! Baba Mtakatifu anasema, Kanisa ni kijana si kwa sababu ya umri, bali ni kutokana na neema ya Roho Mtakatifu, anayewaita kushuhudia upendo wa Kristo, ili hatimaye, kuweza kuchuchumilia ustawi na mafao ya wengi.

Upendo wa Kristo unawawajibisha kuwahudumia maskini na hivyo kuwa chachu ya mageuzi ya upendo na huduma; huku wakiwa na uwezo wa kushinda kishawishi cha kugeuzwa kuwa ni walaji wa kupindukia, wachoyo na wabinafsi. Waamini wanapaswa kung’ara kwa upendo wa Kristo kwa kuwa ni mashuhuda hai wa Injili ya Kristo kila pembe ya mji huu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kutoogopa kuwa watakatifu, kwa sababu wanahitajika sana, kwani ni chemchemi ya nguvu, maisha na furaha ya kweli. Watu wote watambue kwamba, wameumbwa na Mwenyezi Mungu ili wawe watakatifu na wakamilifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni! Kumbe, wanaitwa, wanashangazwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo!

Papa: Misa Bulgaria

 

 

05 May 2019, 16:18