Tafuta

Papa Francisko: Wahudumu wa Sekta ya Afya: Zingatieni dhamiri nyofu; lindeni: utu, heshima na haki msingi za wagonjwa! Papa Francisko: Wahudumu wa Sekta ya Afya: Zingatieni dhamiri nyofu; lindeni: utu, heshima na haki msingi za wagonjwa! 

Papa: Zingatieni: Uhuru wa dhamiri, utu & heshima kwa wagonjwa!

Maendeleo makubwa katika vifaa vya tiba ya afya kwa mwanadamu, yamewezesha kuwa na njia pamoja na teknolojia mpya ya kuchunguza na kutibu magonjwa, kiasi hata cha kuibua matatizo na changamoto za kanuni maadili na utu wema; mambo yanayotishia maisha, utu na heshima ya binadamu. Kutozingatia uhuru wa dhamiri kunahatarisha utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki wa Huduma ya Afya Nchini Italia, “ACOS”, kimekuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kusimama kidete kuwatetea maskini na wanyonge pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa, wazee na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika kipindi cha Miaka 40 “ACOS” imejipambanua kwa kuwa karibu sana na wagonjwa pamoja na maskini.

Wanachama wa “ACOS” wameendelea kusaidia mchakato wa maboresho ya mfumo wa huduma ya afya, mazingira ya kazi pamoja na maisha ya wagonjwa na ndugu zao, kama walengwa wa utume huu! Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana katika sekta ya afya kuhusu: maana ya dawa na uhusiano wake na mgonjwa. Maendeleo makubwa katika vifaa vya tiba ya afya kwa mwanadamu, yamewezesha kuwa na njia pamoja na teknolojia mpya ya kuchunguza na kutibu magonjwa, kiasi hata cha kuibua matatizo na changamoto za kanuni maadili na utu wema; mambo yanayotishia maisha, utu na heshima ya binadamu.

Kutozingatia uhuru wa dhamiri kunahatarisha utu na heshima ya binadamu, kiasi cha wafanyakazi katika sekta ya afya kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, kanuni maadili na utu wema. Hii ni changamoto kubwa hata kwa wagonjwa pamoja na familia zao. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 17 Mei 2019 alipokutana na kuzungumza na Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki wa Huduma ya Afya Nchini Italia, “ACOS”.

Uamuzi wa kufuata dhamiri nyofu unapaswa kutekelezwa kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, ili kutambua sababu msingi zinazowasukuma kutenda hivyo na wala usiwe ni sababu ya kudhalilisha au kuonesha kiburi na majivuno! Dhamiri nyofu iwe ni kikolezo cha majadiliano na wale wenye mawazo tofauti; iwe ni fursa ya kusikilizana, kwa ajili ya kulinda na kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi. Iwe ni kielelezo cha mwandani wa safari na wagonjwa, waliosahaulika na hatimaye, kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatufu anakaza kusema, hii ndiyo njia muafaka ya kuweza kutambua mambo msingi katika ukweli wa hali na mazingira mbali mbali, kwa ajili ya ustawi wa kimaadili wa wale waohusika! Na kwa hakika ni ushuhuda wa Injili unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha, utu na heshima ya binadamu. Fumbo la Umwilisho ni hazina, amana, utajiri na shule kubwa na endelevu kwa maisha ya binadamu. Kristo Yesu kwa maneno na matendo yake, amewasaidia walimwengu kutambua kwamba, mwanadamu umeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kila binadamu ana utu na heshima yake na wala si namba peke yake!

Wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kama binadamu na kwamba, kupunguza gharama za huduma kwa wagonjwa kisiwe ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya wagonjwa. Hawa ni watu wanaopaswa kusikilizwa kwa makini, kueleweka na kusindikizwa katika shida na mahangaiko yao, daima wakifanyiwa uchunguzi wa kina, ili waweze kupata tiba muafaka inayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili. Mgonjwa lazima ajenge imani kwa wale wanaomhudumia na kamwe asitendewe kama mashine!

Wagonjwa wanatofautiana kwa mahitaji, kumbe, wahudumiwe kwa heshima, kwani hii ni dhamana tete, ambayo wakati mwingine haifahamiki vyema, wala kuthaminiwa na jamii! Wahudumu wa sekta ya afya, wanapaswa pia kuangaliwa kwa jicho la upendo na huruma kwa kutambua kwamba, ugumu wa kazi na changamoto zake, vinaweza kusababisha majanga makubwa kwa wafanyakazi wenyewe. Mazingira mazuri ya kazi, stahiki za wafanyakazi pamoja kuthaminiwa ni mambo yanayopaswa kuangaliwa na kupyaisha daima.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema majiundo makini ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki wa Huduma ya Afya Nchini Italia, “ACOS” sanjari na kulinda uhai wa binadamu. Majiundo makini kitaaluma yaende sanjari pia na majiundo ya maisha ya kiroho, ili kutambua na kuthamini utu, heshima, ustawi na mafao ya wagonjwa: Mgonjwa anapaswa kuonekana kuwa ni jirani anayeteseka. Changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya afya zichambuliwe na kupewa ufumbuzi wa pamoja, ili kuwa na sauti moja.

Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu anawasihi wafanyakazi katika sekta ya afya kuboresha maisha yao kwa njia ya Neno la Mungu anayezungumza nao, Sala na Sakramenti za Kanisa. Waendelee kuiga mfano bora wa watakatifu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini. Amewaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria, ili waendelee kuwa mlinzi na kimbilio lao wakati wa shida na mfano bora wa huduma kwa jirani zao.

Papa: ACOS: Italia
17 May 2019, 16:42