Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Papa Francisko kwa wadau wa tasnia ya habari: Unyenyekevu na uhuru kwa ajili ya kujenga mshikamano katika huduma ya ukweli, amani na maendeleo fungamani. Ujumbe wa Papa Francisko kwa wadau wa tasnia ya habari: Unyenyekevu na uhuru kwa ajili ya kujenga mshikamano katika huduma ya ukweli, amani na maendeleo fungamani.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa kwa Wanahabari: Unyenyekevu, Uhuru na Ukweli!

Papa Francisko asema, ni wajibu wa wadau wa tasnia ya habari kuhakikisha kwamba, wanatenda kadiri ya ukweli na haki, ili mawasiliano yaweze kuwa ni nyenzo ya ujenzi na wala siyo ya uharibifu; chombo cha kuwakutanisha watu na wala si cha kuwasambaratisha; jukwaa la majadiliano ili kutoa dira na mwelekeo sahihi wa maisha na wala si mazungumzo yanayotawaliwa na mtu mmoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linaheshimu na kuthamini kazi inayotekelezwa na wadau wa tasnia ya habari, hata pale, wanapotia kidole kwenye madonda ya maisha na utume wa Kanisa. Hii ni huduma muhimu inayosaidia mchakato wa kutafuta ukweli, unaowaweka watu huru na kwamba, daima Kanisa litaendelea kuwa upande wa wadau wa tasnia ya mawasiliano, kwani linatambua uhuru wa vyombo vya habari! Hii ni dhamana inayowajibisha katika huduma inayotolewa kwa maneno au kwa picha pamoja na yale yote wanayoshirikisha katika mitandao ya kijamii.

Changamoto endelevu ni kutambua kuwa, kila mtu anawajibika mbele ya mambo mabaya na mazuri yanayotendeka ulimwenguni na kwamba, tabia na mwenendo wa maisha una athari zake hata kwa watu wengine ndani ya jamii. Hii ni changamoto kwa wadau wa tasnia ya habari kuhakikisha kwamba, wanatenda kadiri ya ukweli na haki, ili mawasiliano yaweze kuwa ni nyenzo ya ujenzi na wala siyo ya uharibifu; chombo cha kuwakutanisha watu na wala si cha kuwasambaratisha; jukwaa la majadiliano ili kutoa dira na mwelekeo sahihi wa maisha na wala si mazungumzo yanayotawaliwa na mtu mmoja.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mawasiliano yawe ni dira, inayowasaidia watu kuelewana, ili waweze kutembea kwa pamoja katika misingi ya amani badala ya kupandikiza chuki; vyombo vya mawasiliano viwe ni sauti ya wanyonge na kamwe si kipaza sauti kwa wale wanaopiga kelele zaidi! Wadau wa tasnia ya habari wanapaswa kujivika unyenyekevu katika maisha yao ya kiroho na kitaaluma, ili kuboresha weledi, kumbu kumbu za kihistoria, udadisi, uwezo wa kupembua mambo kiyakinifu; kwa kuuliza maswali sahihi na hatimaye, kuweza kutoa muhtasari kwa haraka!

Wadau wa tasnia ya habari wanapaswa kueleweka kwa hadhira wanayoikusudia. Unyenyekevu inaweza kuwa ni fadhila ya mageuzi katika maisha na utume wao kama waandishi wa habari! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 18 Mei 2019 kwa waandishi wa Habari za Nje ya Nchi ya Italia, walipomtembelea mjini Vatican. Unyenyekevu unahitajika sana ili kuweza kufikia ukweli unaokusudiwa kutoka katika uhalisia wa maisha! Tabia ya kudhania kwamba, wanayo majibu tayari inakwamisha mchakato wa kutafuta na hatimaye, kupata ukweli!

Wana habari wanyenyekevu ni wale wanaotoa ujumbe kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi wala hawapanii kudhuru jirani zao au wakati mwingine, Jumuiya nzima. Baadhi ya vichwa vya habari vinaweza kuwasilisha habari potofu, inayodhalilisha utu na heshima ya wengine; habari inayowachafua watu katika jamii. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vina nguvu sana, changamoto ni kuhakikisha kwamba, waandishi wa habari wanashinda kishawishi cha kuchapisha habari isiyohakikiwa barabara! Unyenyekevu uwasaidie waandishi wa habari kutafuta na hatimaye kuwa na muda muafaka, ili kufahamu tukio lililoko mbele yao pamoja na mazingira yake. Wanahabari wanyenyekevu wanajitahidi kuwa na uhakika wa ukweli wanaotaka kuutangaza, wakitambua kwamba, hata wao wanawajibika sana!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, leo hii mitandao ya kijamii imekuwa ni jukwaa linatotumia lugha kali sana, kiasi cha kuacha madonda na machungu katika maisha ya watu. Ni wakati wa kujifunza kutumia maneno yanayoweza kutibu na kuganga kama ilivyo kwa madaktari wanaofanya upasuaji kwa wagonjwa! Utu na heshima ya kila mtu inapaswa kulindwa na kudumishwa, kwa kuondokana na habari za kughushi na badala yake, wadau wa tasnia ya habari wawashirikishe wengine ukweli! Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waandishi wa habari waliopoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu wakiwa kazini na kwamba, uhuru wa vyombo vya habari ni kielelezo makini cha ustawi na maendeleo ya nchi. Jumuiya ya Kimataifa ina kiu ya uandishi wa habari unaofumbatwa katika uhuru, huduma ya ukweli; ustawi na haki.

Haya ni mawasiliano ambayo yatasaidia kujenga utamaduni wa watu kukutana. Waandishi wa habari wawe ni watetezi wa wale wanaoteseka na kunyanyasika; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na wale wanaobaguliwa kutokana na sababu mbali mbali! Waandishi wa habari wawe ni dira na mwanga kwa watu wanaoteseka kwa kutothaminiwa na jirani zao. Wawe ni watetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; watu wanaokufa kwa baa la njaa, ujinga na magonjwa; watoto wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita au wale wanaonyanyaswa na kudhulumiwa. Waandishi wa habari wawakumbushe walimwengu watu wanaoteseka kutokana na ubaguzi na nyanyaso za kidini; watu wanaoteseka kutokana na ukabila, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Wawakumbuke wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali! Hawa ni watu wenye sura, historia na kwamba, wana kiu ya kuonja furaha ya maisha! Wanahabari wanyenyekevu na huru watajibidiisha kutangaza wema unaojidhihirisha kati ya watu; utakatifu wa maisha na watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutafuta na kudumisha haki jamii; chemchemi ya matumaini ya wale waliokata tamaa. Wanahabari watambue na kuthamini mchango unaotolewa na wanawake katika jamii. Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, anathamini sana kazi ya wadau wa tasnia ya habari inayogeuka na kuwa ni utume. Anatambua fika changamoto na magumu wanayokabiliana nayo hasa pale wanapokuwa ugenini. Anawataka waandishi hawa kuchukua mazuri na mema kutoka kwa nchi wanamoishi na kufanyia kazi; wawe ni kioo cha matumaini ya jamii katika unyenyekevu, uhuru, ili hatimaye, waweze kuacha chapa nzuri katika historia ya binadamu!

Papa: Vyombo vya Habari
18 May 2019, 15:40