Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa utawala wa sheria, upendo, ukarimu na mshikamano wa kidugu! Papa Francisko anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa utawala wa sheria, upendo, ukarimu na mshikamano wa kidugu!  (ANSA)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Sheria Kitaifa, Italia 2019

Papa Francisko anawataka vijana kujenga mazingira, ili miji ya Italia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine ni hatari sana! Vijana wajenge upendo na mshikamano wa kidugu, wa kuonesha ukarimu kwa maskini, wajiepushe na vitendo vya kudharau na kuwanyanyasa wenzao! Wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi yapanie kungo'a mizizi yake kwa kujikita katika utawala wa sheria kanuni na taratibu za nchi husika. Watu waelimishwe umuhimu wa kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kukoleza majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenda na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu! Vitendo vya kigaidi ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii, licha ya kuendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia!

Familia ya Mungu nchini Italia, tarehe 23 Mei 2019 imeadhimisha Siku ya 27 ya Sheria Kitaifa kwa kuwakumbuka viongozi wasiosimama kidete kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria na haki msingi za binadamu vinalindwa na kuheshimiwa nchini Italia! Hawa ni akina Jaji Giovanni Falcone, mkewe pamoja na msafara wake wote ulioteketea kwa shambulizi la bomu, katika mauaji yanayojulikana kama “Capaci, huko Palermo, Kusini mwa Italia. Imekuwa ni siku pia ya kumkumbuka Jaji Paolo Borsellino, aliyeuwawa kikatiliki kunako tarehe 9 Julai 1992. Siku ya Sheria Kitaifa nchini Italia inapania kukoleza mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na MAFIA ndani na nje ya Italia, ili kulinda na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe, Jaji Filippo Patroni Griffi, Rais wa Baraza la Ushauri wa Sheria Kitaifa, kwa ajili ya vijana walioshiriki katika maandamano makubwa dhidi ya vitendo vya kigaidi nchini Italia. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu amewatia moyo vijana kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira bora zaidi, ili miji ya Italia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine ni hatari sana! Vijana wajenge ari na moyo wa upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kuonesha ukarimu kwa maskini na jirani zao. Vijana wajiepushe na vitendo vya kudharau na kuwanyanyasa wenzao! Wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo.

Vijana wawe ni kielelezo cha ukweli na uwazi, tayari kuwapokea na kuwasaidia jirani zao. Baba Mtakatifu anasema, huu ni wito kutoka kwa Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, “Christus vivit” yaani “Kristo Yesu” anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Huu ndio ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisikia kwamba, wanaitwa na kutumwa kushiriki katika mchakato wa ukarimu, upendo na utii wa sheria, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki kama ambavyo inafafanuliwa kwenye Katiba ya Italia.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 27 ya Sheria Kitaifa nchini Italia kwa kuwataka vijana kuendelea kuwa na ndoto, ili kuhakikisha kwamba, yote wanayoyafanya yanasaidia kujenga na kudumisha ubora na uzuri wa nyumba ya wote!

Papa: Siku ya Sheria
25 May 2019, 15:00