Papa Francisko litaka Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa utamaduni wa ufufuko dhidi ya kifo! Papa Francisko litaka Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa utamaduni wa ufufuko dhidi ya kifo! 

Papa: Tangazeni na kushuhudia Utamaduni wa ufufuko!

Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle ana mchango mkubwa katika sekta ya elimu, kwani kwa mfano na ushuhuda wake, ameisaidia jamii kuzingatia mambo makuu matatu: Dhana ya shule; Uelewa wa mwalimu na Mbinu za ufundishaji. Mambo haya yamefafanuliwa na Papa Francisko alipokutana na kuzungumza na Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo; kumbu kumbu ya miaka 300 ya huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC., katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, muasisi wa Shirika hili, wameendelea kuwa waaminifu kutekeleza dhamana na wito wao ndani ya Kanisa kwa: ukarimu na uaminifu wa Kiinjili. Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle ana mchango mkubwa katika sekta ya elimu, kwani kwa mfano na ushuhuda wake, ameisaidia jamii kuzingatia mambo makuu matatu: Dhana ya shule; Uelewa wa mwalimu pamoja na Mbinu za ufundishaji.

Haya ni mambo makuu matatu ambayo yamefafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC, Alhamisi, tarehe 16 Mei 2019. Elimu ni haki ya kila mtu hata kwa maskini ndiyo maana Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, akatoa kipaumbele cha kwanza kwa elimu katika familia; akaanzisha Shirika la waamini walei, ili kuendeleza mawazo yake ya kutoa elimu kwa umma pasi na kulazimika kwanza kabisa kuwa Mapadre. Huu ukawa ni mwelekeo mpya wa Kanisa kupata “Wamonaki walei” waliojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii ya kiraia. Kwa kuzama katika shughuli za elimu, Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle akapata mang’amuzi mapya juu ya dhana ya mwalimu! Yaani mtu aliyefundwa na kufundika; aliyetambua fika changamoto zilizokuwa mbele yake na kwamba, Ualimu si tu taaluma bali ni wito.

Ni katika muktadha huu, akawatafuta watu waliokuwa na karama na vipaji vya kurithisha elimu asilia na elimu ya darasani. Akajisadaka bila ya kujibakiza kuhakikisha kwamba, anawapatia elimu, ujuzi na maarifa, akionesha mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa Kanisa na Jamii iliyokuwa inawazunguka, ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya mwalimu. Katika utume huu, akagundua mbinu mpya za ufundishaji. Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, akaleta mwelekeo mpya katika masomo: badala ya wanafunzi kujifunza lugha ya Kifaransa akaanza kuwafundisha lugha ya Kilatini iliyokuwa inatumika wakati huo kufundishia.  

Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle aliwapanga wanafunzi wake kwa makundi, ili iwe ni rahisi kuwafundisha na akaanzisha Seminari kwa waalimu wa vijijini, watu waliotaka kufundisha bila ya kulazimika kuwa kwanza watawa. Akaanzisha Shule za Domenika kwa ajili ya watu wazima; vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi pamoja na wafungwa. Wazo lake lilikuwa ni kuanzishwa shule ambayo ingeweza kuwakusanya watu wote, kwa kuwapatia elimu, ujuzi na maarifa ya kazi na hatimaye, watu wakapata pia kufahamu stadi za maisha. Kwa njia hii akaleta mwamko mpya katika mchakato wa elimu kwa kuunganisha: masomo, kazi na ufundi.

Hii ni amana na utajiri mkubwa ambao Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo limeachiwa na Muasisi wao, changamoto na mwaliko wa kukuza ari na mwamko wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni mashuhuda na watangazaji wa utamaduni wa Kristo Mfufuka dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anatawaka wawe na ujasiri wa kuwaendea wale wote ambao wamemezwa na kuzamishwa katika malimwengu kwa kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha; kwa kutumbukia katika ombwe na mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema; watu walioathirika kwa baa la umaskini pamoja na kujikatia tamaa ya maisha.

Ari na mwamko mpya ulioletwa na Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, mwalimu na shuhuda katika upyaisho wa sekta ya elimu, iwe ni chachu ya miradi na utume wao! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waendelee kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika huduma ya uinjilishaji mpya, utume unaovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu, daima wakiwa waaminifu kwa asili na utume wa familia yao ya kitawa, ili kujibu kwa uhakika matamanio halali ya watu wa Mungu; changamoto inayopaswa kutekelezwa kwa ujasiri na uthabiti wa moyo!

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka waendelee kupyaisha utume wao miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na upendo. Daima wawe chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili waweze kupata matunda mengi katika utume wao. Baba Mtakatifu amelishukuru Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC., kwa uwepo na huduma zake katika sekta ya elimu.

Papa: Shule za Kikristo

 

16 May 2019, 15:54