Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Kristo Yesu amewaahidia wafuasi wake zawadi ya Roho Mtakatifu atakayewafundisha na kuwakumbusha yote aliyosema na kutenda! Papa Francisko: Kristo Yesu amewaahidia wafuasi wake zawadi ya Roho Mtakatifu atakayewafundisha na kuwakumbusha yote aliyosema na kutenda!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Roho Mtakatifu

Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni aliwaambia wafuasi wake kwamba, atawapelekea Roho Mtakatifu na kamwe hatawaacha yatima; atakuja kwao! Haya ni maneno ya faraja ambayo hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuwaambia wafuasi wake. Watakuwa ni marafiki zake, ikiwa kama watafikiri na kutenda kama anavyotaka! Daima ataonesha na kudhihirisha uwepo wake endelevu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Katika Kanuni ya Imani Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, “Akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 29 Mei 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa, tarehe 30 Mei 2019 linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ingawa kutokana na sababu za kichungaji, Sherehe hii itaadhimishwa rasmi, Jumapili tarehe 2 Juni 2019 sanjari na Siku ya 53 ya Upashanaji habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2019.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni aliwaambia wafuasi wake kwamba, atawapelekea Roho Mtakatifu na kamwe hatawaacha yatima; atakuja kwao! Haya ni maneno ya faraja ambayo hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuwaambia wafuasi wake. Watakuwa ni marafiki zake, ikiwa kama watafikiri na kutenda katika maisha yao kama anavyotaka! Daima ataonesha na kudhihirisha uwepo wake endelevu na kamwe hawatajisikia kuwa yatima! Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wajumbe wa Mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa unaoendelea mjini Roma! Baba Mtakatifu amewataka waamini kufuata mfano wa Bikira Maria na Mitume wa Yesu waliokuwa wakidumu katika moyo mmoja katika kusali, ili waweze kuwa imara katika kufuata nyayo za Kristo.

Kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, awawezeshe wafuasi wa Kristo kuwa wanyenyekevu, huku wakiendelea kusali na kungoja ujio wa Roho Mtakatifu. Wakristo wakuze na kudumisha ndani mwao sanaa ya ujenzi wa umoja wa kanisa; wawe ni mashuhuda wa imani na vyombo vya Injili ya upendo. Wakristo wajitahidi katika maisha na utume wao, kuwa kweli ni washiriki na mashuhuda wa kazi ya ukombozi, kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza. Wajitahidi kumfungulia Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia mapaji na karama zake; ili hatua kwa hatua, aendelee kuwafunda katika mantiki ya Injili, upendo na ukarimu; kwa kuwafundisha na kuwakumbusha yale yote ambayo Kristo Yesu aliyasema katika maisha na utume wake hapa duniani!

Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee, vijana kutoka Poland ambao Jumamosi ijayo, tarehe Mosi, Juni 2019, watakusanyika kwenye Madhabahu ya Lednica, kuadhimisha Siku ya Vijana Poland. Amewakumbusha kwamba, Kristo Yesu kabla ya kupaa mbinguni alimuuliza Petro mara tatu, ikiwa kama kweli alikuwa anampenda na Petro akamjibu kwa uhakika, hakika anatambua kwamba, anampenda! Maneno haya yawaongoze kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Mahakama ya Huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho pamoja na kushibishwa kwa chakula kilichoshuka kutoka mbinguni yaani, Ekaristi Takatifu.

Siku ya Vijana Poland iwe ni kielelezo cha imani, sala, furaha na sherehe ya umoja wa Kanisa. Vijana wajitahidi kumpokea na kumkaribisha Roho Mtakatifu katika maisha yao kwa kukumbuka kwamba, wametiwa muhuri wa Roho Mtakatifu. Wachunguze vyema dhamiri zao kwa kutambua kwamba, Mathayo mtoza ushuru aliweza kutubu na kumwongokea Mungu, leo hii ni Mtakatifu! Hali hii inawezekana hata kwa vijana wa kizazi kipya, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani!

Papa: Kupaa Bwana

 

29 May 2019, 15:18