Tafuta

Papa Francisko: "Lakini Utuopoe Maovuni" ni msingi wa Sala ya Kikristo! Papa Francisko: "Lakini Utuopoe Maovuni" ni msingi wa Sala ya Kikristo! 

Papa Francisko: Utuopoe Maovuni: Ni msingi wa Sala ya Kikristo!

Sala ya Bwana ina mwelekeza mwamini na kumwingiza katika mapana ya ya mpango wa wokovu. Mshikamano na Kristo Yesu pamoja na ushirika wa watakatifu, unawawezesha waamini kupambana na vishwishi pamoja na uwepo wa dhambi. Maovu yanayotajwa hapa ni nafsi, Shetani, Ibilisi anayetaka kuvuruga mpango wa Mungu na kazi ya wokovu inayotimizwa katika Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ombi la mwisho linalofumbatwa kwenye Sala ya Baba Yetu wa mbinguni ni lile linalosema, “Lakini Utuopoe Maovuni”. Sala ya Bwana ina mwelekeza mwamini na kumwingiza katika mapana ya mpango wa wokovu. Mshikamano na Kristo Yesu pamoja na ushirika wa watakatifu, unawawezesha waamini kupambana na vishwishi pamoja na uwepo wa dhambi. Maovu yanayotajwa hapa ni nafsi, Shetani, Ibilisi anayetaka kuvuruga mpango wa Mungu na kazi ya wokovu inayotimizwa katika Kristo Yesu.

Ni kwa njia ya Shetani, Ibilisi, dhambi na mauti vimeingia ulimwenguni. Mtakatifu Petro katika Waraka wake wa kwanza anawataka waamini kuwa na kiasi na kukesha, kwa kuwa mshitaki wao Ibilisi, kama Simba angurumaye, huzungukazunguka, akitafuta mtu ammeze na waamini wanamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwaopoa katika maovu (Rej. 1 Pt 5:8). Ni katika muktadha huu “Usituache katika kishawishi” na “Lakini Utuopoe Maovuni”, Yesu anatoa msingi wa Sala ya Kikristo na kuwataka rafiki zake, kumkimbilia Mwenyezi Mungu na hasa pale wanapohisi uwepo wa Shetani, Ibilisi unaotishia usalama wa maisha yao ya kiroho!

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 15 Mei 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya mwendelezo wa tafakari kuhusu Sala ya Bwana, maarufu kama Sala ya Baba Yetu. Waamini wanapokumbana na hatari za maisha, wajitahidi kukimbilia katika ulinzi na tunza ya Baba yao wa Mbinguni. Sehemu hii ya mwisho, inawapatia Wakristo fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea: wadhambi, wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; wale wanaokata tamaa katika maisha bila kuwasahau wale walioko kufani!

Sehemu hii ya mwisho ya Sala ya Baba Yetu ni kimbilio la waamini pale ambapo hawana tena tegemeo katika maisha! Daima katika maisha ya mwanadamu kuna uwepo wa dhambi na maovu kama unavyofafanuliwa na Maandiko mbali mbali. Kuna uwepo wa fumbo la dhambi ambao kwa hakika si kazi ya Mungu, lakini inapenyeza mizizi yake katika madonda ya historia. Wakati mwingine, dhambi na maovu yanayonekana kuwa na nguvu zaidi kushinda hata huruma na upendo wa Mungu. Hali hii inaweza kuonekana pale ambapo mwamini amejikatia tamaa ya maisha!

Kwa mwamini anayesali kwa imani na matumaini, anaiona dhambi na maovu haya mbele ya macho yake; mambo yanayokwenda kinyume cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mambo haya yanabubujika kutoka katika asili, historia na kuzama hadi katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Hakuna mtu awaye yote anayeweza kujigamba kwamba, ameipatia dhambi kisogo wala hana tena kishawishi, kwa sababu hii ni sehemu ya maisha ya mwanadamu yanayotibuliwa kwa uwepo wa Shetani, Ibilisi.

Baba Mtakatifu anasema, kilio cha waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaopoa kutoka katika maovu, ni kutaka kukimbilia chini ya ulinzi, tunza na mbawa zake. Haya ndiyo mambo ya misiba, mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia; majanga yanayowasibu wale wote wanaotumbukizwa katika utumwa; watu wanaowatumia wengine kwa mafao ya binafsi bila kusahau kilio cha watoto wadogo! Vilio vyote hivi vinapiga kelele katika sakafu ya moyo wa binadamu na hivyo kugeuka kuwa ni maombi ya mwisho katika Sala ya Bwana.

Katika simulizi la mateso ya Kristo Yesu anamwomba Mwenyezi Mungu akisema, “Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe” (Mk. 14:36). Hapa, Kristo Yesu anahisi ndani mwake, kuelemewa na uovu, kifo, lakini zaidi kifo cha Msalaba! Yesu anahisi upweke, dharau na nyanyaso! Anaonja ukatili na unyama wa binadamu ambaye anamgeuzia kisogo! Badala ya kuota upendo na ustawi katika maisha, mwanadamu anajikuta akiogelea katika maovu yanayomwaribia maisha, kiasi hata cha kujikatia tamaa!

Baba Mtakatifu anasema, Sala ya Bwana, maarufu kama Sala ya Baba Yetu ni kama muziki mwanana kila mtu anahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wake. Mkristo anatambua fika nguvu ya dhambi na ubaya wa moyo na wakati ule ule anatambua mang’amuzi ya Kristo Yesu, jinsi alivyopambana na dhambi, hadi dakika ya mwisho, sasa ni uamuzi wa waamini wenyewe, kumwalika Kristo Yesu, ili aje kuwasaidia katika mapambano na Shetani, Ibilisi. Hii ni amana na utajiri mkubwa ambao Kristo Yesu amewaachia wafuasi wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hiki ni kielelezo cha uwepo wa Mwana wa Mungu ambaye amewakomboa waja wake, kwa kuwakirimia toba na wongofu wa ndani. Kristo Yesu, hakushinda kwa upanga, bali kwa kutoa msamaha kwa watesi wake! Msamaha wa Kristo Yesu pale Msalabani ni chemchemi ya amani, kama alama ya Kristo Mfufuka. Amani hii inapaswa kukita mizizi yake katika nyoyo na maisha ya watu. Kristo Yesu ni chemchemi ya amani na furaha. Kristo Yesu Mfufuka ndiye anayeweza kuwaokomboa kutoka katika maovu; ni chemchemi ya matumaini na nguvu inayookoa!

Papa: Sala ya Baba Yetu

 

 

15 May 2019, 15:48