Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amehitimisha Katekesi kuhusu Sala ya Baba Yetu, Sala ya Wafuasi wa Kristo wanayopaswa kuisali kwa unyenyekevu chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Papa Francisko amehitimisha Katekesi kuhusu Sala ya Baba Yetu, Sala ya Wafuasi wa Kristo wanayopaswa kuisali kwa unyenyekevu chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu.  (ANSA)

Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu: Unyenyekevu & Roho Mtakatifu

Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini hawana hofu na hivyo wanaweza kuthubutu kumwita Mungu “Aba!” yaani “Baba”, kiini cha Sala ya Kikristo, maarufu kama Sala ya Bwana, Sala ya Baba Yetu! Hii ni sala inayohitaji ujasiri kwani kwa neema ya Mungu wameunganishwa kuwa waana kama ilivyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu anayewawezesha kumwita Mwenyezi Mungu, “Baba”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Roho Mtakatifu anawafanya waamini kuwa waana kwani hawana hofu na hivyo wanaweza kuthubutu wakati wowote ule kumwita Mwenyezi Mungu “Aba!” yaani “Baba”. Hiki ndicho kiini cha Sala ya Kikristo, maarufu kama Sala ya Bwana, Sala ya Baba Yetu Uliye mbinguni! Hii ni sala inayohitaji ujasiri kwani kwa neema ya Mungu wameunganishwa kuwa waana kama ilivyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu anayewawezesha kumwita Mwenyezi Mungu, “Baba”. Mwamini anaweza kuyaelewa maneno haya kwa kusoma kwa makini Maandiko Matakatifu na hivyo atagundua kwamba, haya ni maneno yaliyotumiwa na Kristo Yesu na sasa ndiyo “Sala ya Baba Yetu”.

Hii ni Sala aliyoitumia Kristo Yesu alipokuwa Bustanini Gethsemane, hatua ya mwisho kabisa katika Fumbo la Umwilisho, linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Katika kipindi hiki kigumu cha mateso na majaribu makubwa, Kristo Yesu anapata ujasiri wa kumwita Mungu “Aba” na kusema, kama inawezekana mapenzi yake yatimizwe! Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 22 Mei 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya hitimisho la katekesi yake kuhusu Sala ya Wakristo, Sala ya Bwana, yaani Baba Yetu Uliye Mbinguni.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwahimiza wafuasi wake kukuza na kudumisha ari na moyo wa sala dumifu, kwa kuwakumbuka na kuwaombea ndugu zao hasa wale wanaoishi katika mahusiano magumu na Mwenyezi Mungu! Wafuasi wa Kristo wajifunze kusamehe na kusahau kama wanavyosamehewa dhambi zao na Baba yao wa mbinguni. Sala ya Baba Yetu ni mfano bora wa Sala ya Kikristo! Mtakatifu Paulo hazungumzii sana kuhusu Sala ya Baba Yetu, lakini, muhtasari wa Sala hii unafumbatwa katika neno moja tu “Aba” yaani “Baba”. (Rej. Rm. 8: 15 na Gal.4:6). Katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka, Kristo Yesu, anazima kiu ya Mitume wake kwa kuwafundisha Sala ya “Baba Yetu” inayojulikana pia kama “Sala ya Wakristo” (Lk. 11:1).

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa Sala ya Kikristo. Waamini hawawezi kamwe kusali vyema pasi na nguvu ya Roho Mtakatifu anayesali pamoja nao. Roho Mtakatifu anawawezesha kusali kama wafuasi wa Kristo na waana wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini “kuchota” utajiri wa chemchemi ya maisha ya sala ambao umeandaliwa na Kristo Yesu, kiasi cha kuanzisha majadiliano ya upendo na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu alikuwa na mitindo mbali mbali ya kusali, kwa mfano aliweza kusali kwa kusema: “Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha”.

Hii ni Zaburi ya 22 ambayo Mwinjili Mathayo anaitumia. (Rej. Mt. 27:46). Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kumwacha Mwanaye wa pekee, anaendelea kuwafunulia upendo wake usiokuwa na mipaka hata watoto wake wadhambi. Yesu hata katika dakika ya mwisho ya maisha yake, bado alithubutu kumwita Baba yake wa mbinguni, kiini cha uhusiano na mafungamano ya dhati katika imani na sala. Hii ni chemchemi ya Sala ya Wakristo na kwamba, kwa njia ya Maandiko Matakatifu, mwamini anaweza kusali kama anavyopenda, kwani sala ina historia ndefu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanaposali, wajitahidi kuwakumbuka na kuwaombea ndugu zao, na hasa zaidi maskini, ili waweze kupata faraja na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Mwishoni mwa Katekesi kuhusu Sala ya Wakristo, Baba Mtakatifu amemshukuru: Baba, Bwana wa mbingu na nchi kwa kuwa mambo haya amewaficha wenye hekima na akili; akawafunulia watoto wachanga, kwa kuwa ndivyo ilivyo mpendeza! (Rej. Lk. 10:21). Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujinyenyekesha wanaposali, ili Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza katika sala! Yaani imependeza sana kuona umati wa mahujaji kutoka Tanzania, wengi wao wakiwa ni Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, wakiwa wameungana na mahujaji wengine kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kusikiliza katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko! Hili ni kundi la WAWATA 58 chini ya uongozi wa Padre Raphael Madinda, Mratibu wa Kurugenzi ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Papa: Sala ya Baba Yetu
22 May 2019, 14:51