Tafuta

Papa Francisko anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani, wongofu na utakatifu wa maisha! Papa Francisko anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani, wongofu na utakatifu wa maisha! 

Waamini Salini Rozari: Kuombea wongofu na amani duniani

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 15 Mei 2019 amewakumbusha waamini umuhimu wa kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea: toba na wongofu wa ndani; amani na utakatifu wa maisha. Amemkumbuka Mtakatifu Yohane Paulo II aliponusurika kifo, 13 Mei 1981 na kwamba, 15 Mei 2019 ni Siku ya Familia Kimataifa na Utunzaji bora wa mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 13 Mei, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Fatima ambaye ameacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni siku ambayo Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, alisalimika katika jaribio la kutaka kumwondolea uhai kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican, kunako tarehe 13 Mei,1981. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, kuhusu Sala ya Baba Yetu, Jumatano, 15 Mei 2019, kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekazia kuhusu nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye alikuwa kweli ni mama mlinzi na mwongozi wa maisha yake.

Bikira Maria wa Fatima anawakumbusha waamini umuhimu wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili wasiendelee kumhuzunisha kwa kutenda dhambi! Anawasihi waamini kusali Rozari Takatifu muhtasari wa historia ya ukombozi, ili kweli watu waweze kutubu na kumwongokea Mungu pamoja na kuombea amani ulimwenguni. Kipindi cha Pasaka ni muda muafaka tena uliokubalika kwa ajili ya kuombea amani duniani. Mwezi Mei ni wakati muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, silaha za pambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na matendo ya huruma.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano wa Ufuatiliaji wa Familia Kimataifa “Family International Monitor” ulioandaliwa na Taasisi ya Yohane Paulo II kwa ajili ya Ndoa na Familia. Mkutano huu unafanyika wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Familia Duniani, changamoto kwa familia duniani, kujikita katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi hiki cha Pasaka anapenda kuwapatia baraka zake za kitume, upendo na huruma ya Mungu kwa wao binafsi pamoja na familia zao.

Papa: Fatima
15 May 2019, 15:15